Mfumo wa ‘Ajira Portal’ kudhibiti ajira katika taasisi za umma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika akisisitiza umuhimu wa Waajiri kutumia mfumo wa Tehama katika kutangaza nafasi za ajira ’Ajira Portal’ wakati akizindua mfumo huo ulipo chini ya Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Jijini Dodoma. Picha| Idara ya Habari-Maelezo.
- Utasaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika kutangaza nafasi za ajira kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari.
- Ni muarobaini kwa vitendo vya rushwa, utashi na upendeleo katika sekta ajira.
Dar es Salaam. Serikali imewataka waajiri katika taasisi za umma kutumia mfumo wa kidijitali wa maombi ya kazi (Ajira Portal) uliopo chini ya Ofisi ya Rais Sekretarieti ya Ajira ili kuondoa changamoto mbalimbali ikiwemo vitendo vya rushwa na gharama za kutangaza ajira katika vyombo vya habari.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni George Mkuchika aliyekuwa akizungumza wakati akifungua mafunzo kwa waajiri Jijini Dodoma amesema kuwa waajiri wote wanapaswa kutumia mfumo wa pamoja ili kuondoa changamoto za upatikanaji wa ajira katika taasisi za umma.
“Hakuna sababu ya kila Taasisi kujenga mifumo ya kuendesha michakato ya ajira wakati tayari Serikali imeshawekeza katika ‘ Recruitment Portal’ kupitia Sekretarieti ya ajira.
“Mfumo huu ni muarobaini dhidi ya vitendo vya rushwa, utashi na upendeleo kwa kuwa utakuwa na uwezo wakuchagua waombaji wa ajira kulingana na sifa zao na nafasi walizoomba,” amesema Mkuchika
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Habari-Maelezo, mfumo huo utasaidia kupunguza gharama zilizokuwa zikitumika kutangaza nafasi za ajira kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari.
Kupitia mfumo huo, mchakato wa kuendesha zoezi zima la kutangaza nafasi za ajira hadi kukamilisha usaili litafanyika kwa muda mfupi tofauti na ilivyokuwa awali na kuchelewesha upatikanaji wa majibu kwa waombaji wa nafasi za ajira.
Zinazohusiana:
- Mikakati inayoweza kuwasaidia vijana kuepuka ukosefu wa ajira.
- Wahitimu vyuo vikuu wakumbushwa kuchangamkia fedha za halmashauri.
- Vijana waanika fursa zilizojificha katika matumizi ya mitandao ya kijamii.
Taasisi zilizopo chini ya Msajili wa Hazina nazo zimetakiwa kutumia mfumo wa maombi ya kazi kuendesha michakato ya ajira ili kuwa na uhakika na takwimu sahihi, kumbukumbu na uhakika kwamba wanaoajiriwa Serikalini ni wale waliohakikiwa kupitia Mamlaka ya Vitambulisho (NIDA) na Baraza la Mitihani (NECTA).
Kwa upande wake, Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma, Xavier Daudi amesema kuwa mfumo huo una maeneo makuu matatu la kwanza likiwa ; eneo la mwombaji wa kazi (Applicant), Eneo la Mwajiri (Employer); na eneo la Sekretarieti ya Ajira ( Handling Interview Process and Placement/ Administrator).
Amesema mfumo huo unaongezeka uwazi kwa waombaji wa kazi na pia mifumo ya Tehama imerahisisha utunzaji wa taarifa na nyaraka mbalimbali za waombaji kazi.
Latest