Zifahamu nguzo tano zinazoibeba ilani ya vijana kuelekea Uchaguzi Mkuu 2025
- Ni pamoja na uongozi, elimu, teknolojia pamoja na ajira
Dar es Salaam. Huenda jamii na Serikali zikapata mbinu mpya za kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana katika nyanja za kiuchumi, kijamii na kisiasa mara baada ya wadau wa maendeleo kuzindua ilani ya vijana.
Tofauti na ilani za vyama vya siasa, nyaraka hii ni matokeo ya mchakato wa kukusanya maoni ya vijana kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania yenye lengo la kutoa dira ya pamoja juu ya masuala ambayo vijana wanataka yazingatiwe na kupewa kipaumbele na vyombo vya maamuzi.
Matokeo ya mchakato huo yamekusanywa na kuratibiwa ili kuunda sauti moja ya kundi hilo ambalo ni takribani asilimia 34 ya watu waliopo Tanzania kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022.
Ilani hii imeainisha maeneo ya kipaumbele ambayo vijana wanataka yaingizwe katika sera na mipango ya maendeleo ya Taifa yaliyobeba mahitaji ya kijamii, kiuchumi, kisiasa na kimazingira ambayo vijana wanaamini vitakuwa msingi bora wa nchi.
Vijana na uongozi
Ilani hiyo inalenga kuongeza nafasi na ushiriki wa vijana katika maamuzi muhimu ya Taifa, kuanzia ngazi za kijiji hadi Serikali kuu.
Inahimiza kuwapa vijana nafasi katika mabaraza ya maamuzi, kamati za maendeleo na nafasi za uongozi wa kisiasa na kijamii.
Afisa Maendeleo, Miradi ya Vijana kutoka Taasisi isiyo ya Kiserikali ya ActionAid Tanzania, Arif Fazel amesema vijana wanapaswa kushiriki kikamilifu katika uongozi na kutumia ubunifu wao ili kutengeneza suluhisho za changamoto zinazowakabili.
“Mimi nimewahi kuthubutu kuchukua fomu na kujaribu kugombea nafasi ya uongozi, japokuwa sikufanikiwa, naamini huo ni mfano wa namna kijana anavyoweza kutafuta suluhisho na kuonyesha kuwa ushiriki wetu si lazima upimwe kwa kushinda tu, bali kwa ujasiri wa kusimama na kuchukua hatua,” amesema Fazel

Ilani hiyo inalenga kuongeza nafasi na ushiriki wa vijana katika maamuzi muhimu ya Taifa, kuanzia ngazi za kijiji hadi Serikali kuu. Picha| Jukwaa la Ajenda ya Vijana
Elimu na teknolojia
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Jukwaa la Ajenda ya Vijana Rajabu Mpilipili amesema ilani hiyo imeweka kipaumbele kuhakikisha vijana wanapata elimu bora, jumuishi na yenye kuendana na mabadiliko ya dunia ya sasa.
Mpilipili ameongeza kuwaiIlani inasisitiza umuhimu wa mitaala inayokidhi mahitaji ya soko la ajira ya karne ya 21 Ikiwa ni pamoja na maarifa ya kidijitali, ujuzi na ubunifu, pamoja na upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati.
“Ilani hii inahimiza upanuzi wa miundombinu ya TEHAMA ili kuwapa vijana fursa sawa za kielimu, mijini na vijijini,” amesema Mpilipili.
Hata hivyo, tayari Serikali ya Tanzania imeshafanya maboresho ya mitaala ya elimu kuanzia shule ya msingi mpaka sekondari ambapo sehemu ya maboresho hayo ni kuwepo kwa mikondo ya amali katika shule za sekondari.
Ajira na fursa za kiuchumi
Ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, ilani hiyo inatoa msukumo wa sera na miradi inayokuza ujasiriamali, stadi za kazi na uvumbuzi.
Tanzania ni miongoni mwa nchi ambazo vijana wake wanakabiliwa na changamoto ya ajira kutokana na ongezeko la wahitimu katika elimu ya juu na ya kati huku Serikali na sekta binafsi zikishindwa kuendana na kasi ya ongezeko hilo.
Takwimu za Serikali zinabainisha kuwa vijana milioni 1.7 sawa na asilimia 12.2 ya vijana wenye uwezo wa kufanya kazi hawana ajira.
Ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira Mpilipili amewashauri vijana kutumia fursa za biashara ndogondogo, teknolojia mpya na miradi ya kilimo cha kisasa ili kujitegemea kiuchumi na kuchangia pato la Taifa.

Ili kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira, ilani hiyo inatoa msukumo wa sera na miradi inayokuza ujasiriamali, stadi za kazi na uvumbuzi. Picha| Jukwaa la Ajenda ya Vijana
Mabadiliko ya tabia nchi
Ilani inatambua wajibu wa vijana katika kulinda na kuhifadhi mazingira ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi yanayoendelea kuuathiri ulimwengu ambapo imependekeza mikakati ya elimu ya mazingira, kampeni za kupanda miti, uvumbuzi wa nishati mbadala, na usimamizi wa taka kwa njia rafiki kwa mazingira.
Pia imeweka mikakati ya kuwajengea vijana uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi katika jamii zao.
Afya na Ustawi
Ilani hii inalenga kuhakikisha huduma bora za afya ya mwili na akili zinapatikana kwa vijana wengi, sambamba na kuhakikishi ustawi wa jamii kwa ujumla.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), takribani asilimia 70 ya matatizo ya kiafya barani Afrika yanahusiana na lishe duni, afya ya akili na maradhi yanayoweza kuzuilika kupitia kinga na elimu sahihi.
Aidha, tafiti nchini Tanzania zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 60 ya vijana chini ya miaka 25 wanakabiliwa na changamoto za afya ya akili, lishe duni, na ukosefu wa huduma rafiki.
Hivyo ilani imependekeza kuimarishwa kwa vituo vya afya, elimu ya lishe, huduma rafiki kwa vijana, na program za michezo, afya ya akili na burudani ili kukuza maisha yenye afya njema.
Kwa mujibu wa waratibu wa Ajenda ya Vijana, ilani hii inalenga kuwa dira ya ushiriki wa vijana katika Uchaguzi Mkuu wa 2025 na miaka inayofuata, huku ikitoa wito kwa vyama vya siasa, watunga sera na taasisi mbalimbali kuingiza vipaumbele hivyo katika mipango yao ya kitaifa.
Latest
