Serikali yatangaza nafasi za kazi 2,611, zaidi ya nusu ni za walimu wa biashara

February 12, 2025 1:42 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Nafasi 2,316 ni za walimu wa somo la biashara.
  • Nyingine 295 ni walimu wa masomo 9 ya amali. 

Arusha. Serikali ya Tanzania imetangaza nafasi mpya mpya za ajira 2,611 za ualimu wa masomo mbalimbali ikiwemo masomo ya biashara na amali kiwemo ushonaji na uchomeleaji.

Taarifa iliyotolewa na Katibu wa Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma Februari 10, 2025 kwa niaba ya Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa inabainisha kuwa kati ya nafasi hizo 2,316 ni za walimu wa somo la biashara.

Nafasi hizo za walimu wa biashara daraja III C ni asilimia 98 ya nafasi zote za ajira zilizotangazwa na Serikali huku ualimu wa masomo mengine tisa ya ufundi zikiwa asiilimia 2 pekee sawa na nafasi 295.

Kati ya nafasi hizo walimu ushonaji wanaohitajika ni 18, uselemala (33), upakaji rangi na uandikaji maandishi (6), umeme wa magari (3),uchomeleaji na utengenezaji vyuma (13) na nafasi tatu za ualimu wa nishati ya jua.

Masomo mengine yanayohitaji walimu ni uzalishaji wa chakula nafasi 14, muziki (nafasi 2) pamoja na nafasi 28 za ualimu wa somo la huduma ya chakula, vinywaji na mauzo.

Vigezo na sifa za muombaji vimeainishwa katika kila nafasi ambapo ni lazima muombaji awe amehitimu chuo ngazi ya stashahada au shahada katika kada ya ualimu pekee au isiyo ya elimu.

Kwa waombaji wasio na shahada ya elimu wanatakiwa kuwa tayari kupewa mafunzo ya ualimu mara baada ya kuajiriwa.

Itakumbukwa, Novemba 23, mwaka huu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia Prof Adolph Mkenda alidokeza kuwa Serikali ipo mbioni kutoa kibali cha ajira 4,000 za walimu wa masomo ya biashara jambo linalochochea utolewaji wa ajira kwa kada hiyo.

Mbali na walimu wa masomo ya biashara, huenda utolewaji wa ajira za walimu katika masomo ya ufunzi ni maandalizi ya Serikali katika kuwanoa wakufunzi watakaosadia utekelezaji wa Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 iliyozinduliwa hivi karibuni.

Katika sera hiyo mpya elimu ya msingi (ya lazima) itatolewa kwa miaka 10 tofauti na miaka saba ya awali na baada ya hapo mwanafunzi ataenda elimu ya sekondari ya upili (advanced education) ambapo atatakiwa kuchagua kati ya mkondo rasmi au mkondo wa amali.

Kwa upande wa elimu ya amali mwanafunzi atachagua kozi moja kati ya kozi 15 zitakazotolewa ambazo ni pamoja na uhandisi umeme na mitambo, ushoni, kilimo, ufugaji na usindikaji chakula na akimaliza atapata cheti kitakachomuwezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks