Vifahamu visiwa 10 vikubwa zaidi duniani

September 20, 2024 5:39 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kisiwa cha Greenland, Honshu, Bornea na Sumatra.

Duniani kuna visiwa vingi vyenye uzuri wa kipekee na umuhimu wa kihistoria. Baadhi vinahamika na vingine havifahamiki au hata si mashuhuri kama ilivyo Zanzibar na Maldives. 

Visiwa hivyo, ambavyo ni vipande vya ardhi vilivyozungukwa na maji, vinatofautiana kwa ukubwa, mandhari na hali ya hewa.

Ingawa visiwa vingi ni vya asili ila kuna vingine vimejengwa na binadamu kwa madhumuni mbalimbali.

Kutokana na umuhimu wa visiwa hivi, Nukta Habari imefanya uchambuzi wa visiwa vikubwa duniani kwa kutumia vyanzo mbalimbali vya habari vya kuaminika zikiwemo tovuti za mamlaka za visiwa husika na toleo la tatu la Kamusi ya Kiswahili lililotolewa na Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita). 

Vifuatavyo ndiyo visiwa 10 vikubwa zaidi duniani. Je, Zanzibar imo au kisiwa kingine unachokifahamu?

10. Ellesmere

Ellesmere ndio kisiwa cha 10 kwa ukubwa duniani kikiwa katika Visiwa vya Malkia Elizabeth, Nunavut na Canada.

Kisiwa hiki kina eneo la kilomita za mraba 183,965 na kina mandhari yenye mwinuko mkubwa pamoja na nyanja kubwa za barafu.

Kisiwa cha Ellesmere kiliingia kwenye ramani na umaarufu mnamo 1616 na mpelelezi William Baffin na kilipewa jina mnamo 1852 na Msafara wa Sir Edward A. Inglefield kwa heshima ya Francis Egerton, Earl wa kwanza wa Ellesmere.

Katika kisiwa hiki kuna aina kumi na tatu za buibui ingawa hali ya hewa ni kali, “oasi ya joto” ya pekee katika Ziwa Hazen inatoa majira ya joto yenye joto la kushangaza.

 Kipindi kisicho na baridi katika Fiord ya Tanquary kina wastani wa siku 55.

Kisiwa cha 10 kwa ukubwa duniani na kisiwa cha kaskazini katika Aktiki ya Canada. Picha|Tripadvisor.

9. Victoria

Victoria ni kisiwa kilichopo Canada, katika jimbo la Nunavut kikiwa kisiwa cha tisa kwa ukubwa duniani chenye ukubwa wa kilomita za mraba 220,548 sawa na maili za mraba 85,154. 

Kina historia ndefu inayohusisha jamii za Inuit, ambao wameishi katika maeneo hayo kwa muda mrefu wakitegemea uvuvi na uwindaji.

Kisiwa hiki kilipewa jina la Malkia Victoria wa Uingereza mnamo karne ya 19 wakati wa safari za utafiti za kizungu katika Aktiki. 

Wakati huo, wapelelezi kama Sir John Franklin walijaribu kutafuta njia ya kuvuka Bahari ya Aktiki kwenda Bahari ya Pasifiki kupitia kile kilichojulikana kama njia ya Kaskazini yaani kwa kimombo Northwest Passage.

 Hii ni sehemu ya muonekano wa kisiwa  cha Victoria kilichopo Canada, katika jimbo la Nunavut. Hiki ni kisiwa cha tisa kwa ukubwa duniani. Picha/Tourline.

8. Great Britain

Great Britain ndicho kisiwa kikubwa zaidi barani Ulaya na cha nane kwa ukubwa duniani, kikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 229,957 (80,823 mi²). 

Ni kisiwa kikuu cha Uingereza (United Kingdom) na kinazungukwa na visiwa vingine vidogo vidogo na visuku elfu moja ndani ya Bahari ya Atlantiki, Bahari ya Kaskazini, Bahari ya Ireland, Bahari ya Keltiki na Mkanada wa Kiingereza.

Ufalme wa Uingereza ambao ulikuwa na nguvu kubwa zamani,ulichukua jukumu kubwa la kukifanya kisiwa hiki kuwa moja ya vituo vya ushawishi mkubwa zaidi katika maendeleo ya kitamaduni duniani. 

Eneo la kisiwa linaloonesha uzuri wa asili ya kipekee na mvuto wa Kisiwa cha Great Britain. Picha|Pixel.

7. Honshu

Nafasi ya saba inashikwa na kisiwa cha Honshu kilichopo nchini Japan.

Kisiwa hiki kina eneo la kilomita za mraba 225,800 na kisiwa kina miji mikubwa kama Tokyo, Kyoto na Osaka.

Tabianchi ya kisiwa hiki huwa ni baridi katika maeneo ya kaskazini (chini ya Hokkaido) na yenye unyevunyevu na ya subtropiki katika kusini magharibi (kabla ya Kyushu).

Hata hivyo, kwa sababu kisiwa hiki kiko katikati ya mfululizo wa visiwa vya Japani, sehemu kubwa ya Honshu bado ina misimu minne tofauti.

Hii ina maana kwamba kupanga safari ya kwenda Honshu ili kupata hali fulani ya hewa inaweza kufanyika kwa urahisi.

Ni vizuri kujua baadhi ya mifumo ya hali ya hewa ya msimu, kama msimu wa mvua wa kila mwaka ( Juni hadi katikati ya Julai) na tufani (zinapokuwa mbaya zaidi kati ya Agosti na Septemba).

Honshu ni kisiwa kikubwa zaidi kati ya visiwa vinne vikuu vya Japan, kilichopo kati ya Bahari ya Pasifiki (upande wa mashariki) na Bahari ya Japan. Picha/Moto Japan.

6. Sumatra

Sumatra ni kisiwa kikubwa zaidi nchini Indonesia na cha sita kwa ukubwa duniani, kikiwa na eneo la kilomita za mraba 443,066.

Tabianchi yake ya kitropiki na maeneo tofauti ya ikolojia yameunda makazi yanayo hifadhi maelfu ya spishi za kipekee.

 Spishi za wanyama hao ni kama Simba wa Sumatran, Nyani wakubwa waitwao Orangutans na tembo wa Sumatran.

Mnamo mwaka 1942–1945 wakati wa vita ya pili ya dunia kisiwa hiki kilikuwa kinamilikiwa na Wajapani mpaka 1950 ndio kisiwa hiki kikarudishwa kuwa sehemu ya Indonesia.

Simba wa Sumatran anayepatika katika kisiwa cha Sumatra. Huyu ni miongoni mwa wanyama adimu wanaopatikana katika eneo hilo. Picha/Pixbay.

5. Baffin

Katika nafasi ya tano kwa ukubwa duniani ni kisiwa cha Baffin. Hiki ndiyo kisiwa kikubwa zaidi nchini Canada kikiwa na kilomita za mraba 503,944 karibu kidogo sawa na ardhi ya Kenya.

Baffin kipo kati ya Greenland na Canada, na kina mandhari ya kuvutia kama vile milima, barafu na mifereji ya maji safi.

Shughuli za kiuchumi katika Kisiwa cha Baffin zinajumuisha uvuvi, ambapo samaki kama vile Salmon na krabu ni sehemu muhimu ya biashara.

Ingawa pia kuna uchimbaji wa madini hasa dhahabu na bati, ambayo yanachangia katika maendeleo ya kiuchumi ya eneo hili.

Muundo wa pekee kwenye mandhari inayopigwa na upepo kaskazini mwa makazi ya Pangnirtung. Eneo hili linaonyesha uzuri wa mwamba na umbali wa Kisiwa cha Baffin. Picha /Acacia Johnson.

4. Madagascar

Madagascar ni kisiwa cha nne kwa ukubwa duniani kikiwa na kilomita za mraba 587,713. Kisiwa hiki kipo katika Bahari ya Hindi, Kusini-magharibi mwa pwani ya Afrika. 

Madagascar inajulikana kwa wanyama na mimea yake ya kipekee na sehemu kubwa ya viumbe wa kisiwa hiki hawapatikani sehemu nyingine yoyote duniani. Ni miongoni mwa visiwa mashuhuri kwa utalii na kilimo cha Vanilla duniani. 

Watu wa kisiwa hiki hawajichukulii kama wa Afrika badala yake wao hujiona kuwa ni watu wa Indonesia na hii ni kutokana na kuwepo baadhi ya tafiti zinazohusishwa na kisiwa hicho kutawaliwa na kundi Waindonesia miaka ya nyuma. Pia, kisiwa hicho kina uhusiano wa kudumu na Ufaransa uliofanyika kutokana na utawala wa kikoloni wa zamani.

Hata hivyo, kisiwa hiki kimekuza uhusiano wa kisiasa, kiuchumi, na kitamaduni na nchi zinazozungumza Kifaransa katika Afrika Magharibi.

Wanawake wa Kiafrika wakiwa katika shughuli zao za kujiitafutia kipato katika kisiwa cha Madagascar. Picha|Pixel.

3. Borneo

Borneo ni kisiwa cha tatu kwa ukubwa duniani na tofauti na visiwa vingine vingi chenyewe kinamilikiwa na nchi tatu za Indonesia, Malaysia, na Brunei. 

Sehemu ya Malaysia inajulikana kama Malaysia Mashariki, ikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 748,168.

Borneo ni moja wapo ya maeneo yenye bioanuwai zaidi kwenye sayari, ikiwa na takriban spishi 15,000 tofauti za mimea.

Kwa ujumla udongo wa Borneo hauna rutuba, isipokuwa kwa baadhi ya maeneo yenye rutuba ya volkano. Kwenye misosi, wali ndio chakula kikuu katika kisiwa hiki sanjari na mahindi, mihogo, matango na maboga.

Mpunga unalimwa kwenye mashamba madogo ya asili wakati pilipili inalimwa kwa kiwango kikubwa na Wachina waliopo katika kisiwa hiki.

 Ikitokea ukawa ni mpenzi wa michezo ya kwenye maji basi kisiwa hiki cha Borneo kinakufaa kwa utalii. Picha /alphacoders.com.

2. New Guinea

New Guinea ni kisiwa cha pili kwa ukubwa duniani, kikiwa na urefu wa takriban kilomita 2,400 na upana wa kilomita 650.

Kisiwa hiki kipo kati ya Indonesia na Papua New Guinea, na kina ukubwa wa kilomita za mraba 821,400, pungufu kidogo kwa ukubwa wa Tanzania yenye kilomita za mraba zaidi ya 945,000. 

Visiwa vinavyounda Papua New Guinea vilikaliwa kwa kipindi cha miaka 40,000 na mchanganyiko wa watu waliojulikana kama Wamelanesia. 

Hali ya hewa ya New Guinea ni ya kitropiki, ambapo joto la wastani la kila mwaka linaanzia kati ya 86 na 90 °F (30 na 32 °C) katika maeneo ya chini joto la mchana katika maeneo ya milimani kwa kawaida linazidi 72 °F (22 °C) mwaka mzima.

Ukitembea katika kisiwa hiki unaaminika kuwa umetembelea pepo ya mwisho iliyopo duniani. Picha.islander.io.

 1. Greenland

Greenland ndio kisiwa kikubwa zaidi duniani chenye eneo linalozidi kilomita za mraba milioni moja (km²). Ukubwa wake unafikia takriban theluthi moja ya bara la Australia ambalo ni bara dogo zaidi duniani. 

Kisiwa hiki kipo kati ya Bahari ya Atlantiki Kaskazini na Bahari ya Aktiki, kikiwa na ukubwa wa kilomita za mraba 2,175,600 au sawa na maili za mraba 840,004. 

Wainuiti ndio jamii ya watu waishio katika kisiwa hiki, kulingana na maeneo yao ya asili wanayotoka. Hupenda kujiita Kalaallit (Watu wa Greenland ya Magharibi),  Inugguit (kutoka wilaya ya Thule) au ILt (Watu wa Greenland ya Mashariki) na hupendelea kuita nchi yao kwa jina la Kalaallit Nunaat.

Mabadiliko yasiyotabirika ya hali ya hewa ya kisiwa hiki kutoka kwa jua hadi vimbunga visivyo na kipimo ni ya kawaida yanayotokana na mivuke ya hewa yenye shinikizo la chini juu ya tabaka la kudumu la hewa baridi ndani ya kisiwa hicho.

Muonekano wa vipande vya barafu vinavyoyeyuka vilivyotoka kwenye Glacier ya Jakobshavn vinaelea katika Ghuba ya Disko karibu na Ilulissat katika kisiwa cha Greenland. Picha /Life On Thin Ice.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks