MCT: Serikali iboreshe sera ya habari na utangazaji

February 13, 2025 5:40 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Maboresho ya sera hiyo yataharakisha  marekebisho ya sheria na kanuni nyingine  zinazoathiri uendeshaji wa sekta ya habari. 

Arusha. Wakati dunia ikiadhimisha siku ya redio duniani Baraza la Habari Tanzania (MCT) limeitaka Serikali kuharakisha mchakato wa kuboresha sera ya habari na mawasiliano ili kuchochea ukuaji wa sekta hiyo muhimu nchini.

Taarifa ya Ernest Sungura ambaye ni Katibu Mtendaji wa MCT iliyotolewa leo Februari 13, 2025 imeitaka Serikali kuboresha sera hiyo ya mwaka 2003 ili kuharakisha marekebisho ya sheria nyingine zinaoathiri sekta ya habari,

“Katika kuadhimisha siku ya redio duniani, MCT inatoa wito kwa Serikali kukamilisha maboresho ya Sera ya Habari na Utangazaji ya mwaka 2003 ambayo iliuanzisha Oktoba mwaka 2023 kwa kuita wadau kupeleka maoni yao ambapo MCT iliwasilisha maoni yake. ..

…MCT inaamini kwamba kukamilika kwa uboreshaji wa Sera hiyo kutaharakisha marekebisho ya sheria na kanuni nyingine ambazo kwa sasa zinaathiri uendeshaji wa sekta ya habari na utangazaji, ikiwemo redio,” imesema Taarifa ya Sungura.

Kwa nyakati tofauti Serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeeeleza kuwa marekebisho ya Sera ya Habari na Utangazaji ni moja vipaumbele vyake kama njia mojawapo muhimu ya kuimarisha uhuru wa kujieleza na wa Habari

Disemba 18, 2024 Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Prof Palamagamba Kabudi, aliyekuwa akizungumza na wadau wa habari alitaja marekebisho ya Sera hiyo kama moja ya vipaumbele vyake na kwamba atasimamia mchakato wa uboreshaji wa Sera hiyo. 

Ahadi ya Waziri Kabudi imekuja baada ya kuonekana kusua sua kwa mchakato huo kwa kipindi kirefu huku baadhi ya mawaziri wa wizara hiyo waliopita wakiwataka wadau wa sekta hiyo kuwa wavulimilivu.

“Huwezi kwenda kubadilisha sheria wakati sera ina msimamo huo. Ndiyo maana tukasema, badala ya kusubiri mabadiliko ya sera, Rais Samia akasema kwa kuwa sheria inapigiwa kelele sana fanyeni mabadiliko ya sheria yale yanayohitaji mabadiliko ya sera yatasubiri. 

Nataka nikuhakikishieni nia ya Rais Samia ni kuhakikisha tunapata uhuru kamili wa vyombo vya habari. Na huko ndiko tunakokwenda tuvumiliane, tukamilishe sera”, alisema Waziri Nape Mei 03, 2024 wakati wa maadhimisho ya Kilele cha Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani.

Watangazaji zingatieni matumizi ya lugha

Aidha, MCT pia inatoa rai kwa watangazaji wa redio kufuata maadili ya utangazaji kwa kuzingatia matumizi ya lugha fasaha na kuhakikisha kutangaza maudhui yaliyojikita kwenye mambo muhimu yanayoihusu jamii kama elimu, afya, maendeleo, siasa, umuhimu wa jamii kuwashirikisha wanawake na masuala ya usalama. 

“Redio ziache kuwa vijiwe vya kujadiliana mambo binafsi na ya mtaani na badala yake kujikita kwenye taarifa yenye maslahi kwa umma. Aidha, MCT inahamasisha ubunifu katika kutengeneza maudhui ya vipindi yaliyofanyiwa utafiti unaolenga kuangazia na kujibu kero za jamii,” imesema taarifa ya Sungura.

Pamoja na hayo MCT inatoa wito kwa redio kuandaa maudhui yatakayoelemisha wananchi kuhusu mchakato wa uchaguzi ambao unatarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu ili kuiwezesha jamii kufanya maamuzi wakati wa kupiga kura. 

Kwa upande wa wamiliki wa vyombo vya habari MCT imewakumbusha kuacha kuajiri watangazaji kwa kufuata umaarufu na badala yake wafuate taaluma ya uandishi wa habari na utangazaji pamoja na mafunzo kwa wasio na taaluma hiyo wanapoajiriwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks