Majaliwa: Waandishi wa habari mko salama
- Asema Serikali ina nia njema ya kufanya kazi pamoja na waandishi wa habari.
- Vyombo vya habari vizingatie maadili ya tasnia ya habari.
Dar es salaam. Serikali ya Tanzania imewahakikishia uhuru na usalama waandishi wa habari katika kutekeleza majukumu huku ikiwataka kuzingatia maadili ya taaluma yao katika kusimamia maslahi ya umma.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema hayo jijini Dar es salaam leo (Mei, 28, 2022) katika utoaji Tuzo ya Umahiri wa Uandishi wa Habari (EJAT2021) na Tuzo ya Mafanikio katika Uandishi wa Habari mwaka 2022 ambazo hutolewa na Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuimarisha uhusiano mwema na vyombo vya habari na itaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha vyombo vya habari vinawahudumia wananchi kwa kuwapa taarifa za uhakika na kwa haraka.
“Serikali inatambua kuwa katika tasnia ya habari kuna changamoto kadhaa hata hivyo nina hakika nanyi ni mashahidi wa hatua ambazo zimekuwa zinachukuliwa na Serikali kutafuta ufumbuzi,” amesema Majaliwa.
Majaliwa amesema hivi sasa Serikali inaendelea kuzifanyia marekebisho kanuni za miundombinu ya utangazaji ya kidigitali na kanuni za leseni za mwaka 2018, kanuni za maudhui ya utangazaji na maudhui ya mtandaoni.
Soma zaidi:
Waandishi zingatieni maadili
Hata hivyo, Waziri Mkuu Majaliwa amewataka waandishi wa habari kuhakikisha wanatetea maslahi ya umma na uhuru wa vyombo vya habari lakini kwa kuzingatia maadili na weledi ambavyo ndiyo msingi katika tasnia ya habari.
“Ni muhimu sana katika kuhabarisha umma hivyo ni matarajio yetu kuwa wanahabari wote mtatafuta taarifa sahihi ili kusiwepo na upotoshaji wa aina yoyote ile tunawategemea sana katika kuhabarisha umma wa watanzania.
“Nisisitize vyombo vya habari kuzingatia miiko ya nchi yetu, tamaduni na maadili ya waandishi wa habari, Serikali nayo kwa upande wetu tutaendelea kuwahakikishia usalama na uhuru wenu katika kutimiza majukumu yenu,” amesema Majaliwa.
Waziri wa Habari na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye amesema kuwa Serikali ina nia njema ya kufanya kazi pamoja na waandishi wa habari kwa kuhakikisha inatengeneza mazingira rafiki nchini.
“Tunatambua kiu ya wanahabari katika kuhakikisha wanajengewa mazingira mazuri ya kufanya kazi zao, yako maelekezo mahususi yaliyotolewa Mheshimiwa Rais ya kupitia upya sera na sheria ya habari na kanuni zake.
“Niliahidi bungeni mwaka huu fedha kazi hiyo itakamilika tunaomba ushirikiano wenu tuikamilishe kwa ukamilifu wake, tutengeneze sheria itakayodumu muda mrefu lakini itakayosaidia tasnia ya habari kukua.” amesema Waziri Nape.
Latest



