Mauzo ya kahawa kufikia Sh2.5 trilioni 2030

February 19, 2025 7:10 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Yalenga kuongeza uzalishaji hadi kufikia tani 300,000 ifikapo mwaka 2030.
  • Yajipanga kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa.

Arusha. Serikali ya Tanzania imesema inajipanga kuongeza uzalishaji wa zao la kahawa hadi tani 300,000 ifikapo mwaka 2030 ili kuongeza mapato ya zao hilo hadi Sh2.5 trilioni.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa aliyekuwa akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam kuelekea mkutano wa kahawa (g25) leo Februari 19, 2025 amesema kuwa mauzo hayo yataongezeka kutoka Sh617.5 bilioni.

“Sisi mauzo yetu ya kahawa yameshafika dola milioni 240 (sawa na Sh617 bilioni) na ni kazi kubwa imefanyika miaka mitatu hii tangu mheshimiwa Rais ametoa maelezo mahususi ya kuinua sekta ya kilimo Tanzania,” amesema Msigwa.

Mkutano huo wa wanahabari na Msigwa ni sehemu ya maandalizi ya mkutano mkubwa wa kahawa utakaofanyika Februari 21 na 22 jijini Dar es Salaam katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere (JNICC).

Rais Samia Suluhu Hassan ndiye anayetarajiwa kuwa mgeni rasmi wa mkutano huo akiwaongoza wakuu wa nchi, mawaziri, mamlaka na taasisi za kahawa, pamoja na wadau wa sekta binafsi kutoka nchi 25 za Afrika zinazozalisha kahawa (G25), ili kujadili na kutekeleza mikakati ya kubadilisha sekta ya kahawa.

Msemaji Mkuu wa Serikali Gerson Msigwa akiwa kwenye picha ya pamoja na baadhi ya wanahabari waliohudhuria mdahalo maalum kuelekea mkutano wa kahawa wa G25.Picha Crown Media.

Malengo makuu ya mkutano huo ni pamoja na kufungua fursa za ajira kwa vijana na wanawake, kukuza ufadhili wa sekta ya umma na binafsi, kutoa msaada wa kifedha kwa wakulima, kuanzisha kituo cha ubora cha kanda, na kuoanisha viwango vya kahawa barani Afrika ili kuimarisha biashara ya kahawa ndani ya bara.

Mbali na ajenda hizo mkutano huo unatarajiwa kuja na azimio la Dar es Salaam litakalosainiwa na viongozi wa nchi kutoka barani Afrika, huku ukitoa nafasi kwa wazalishaji na wauzaji wa bidhaa hizo kuonesha bidhaa zao katika mabanda ya maonesho.

Kupitia mkutano huo Msigwa amesema Tanzania inatarajia kuongeza uzalishaji wa ndani wa zao hilo kutoka tani 55,000 zilizokuwepo mwaka 2022/23 hadi kufikia tani 85,000 mwaka 2024/25 ikitarajiwa kuongezeka zaidi hadi tani 300,000 mwaka 2030.

Ili kufikia uzalishaji huo Msigwa amesema Serikali imejipanga kujihakikishia utoshelevu wa mbegu kupitia taasisi za utafiti wa mbegu zilizopo nchini pamoja na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya tabia nchi.

“Mabadiliko ya hali ya hewa tunakabioliana nayo kwa kuhamasisha kilimo cha umwagiliaji, tumeanza na vijana wa BBT (Jenga Kesho iliyobora) tunapowakabidhi ‘polt’ za mashamba tunawachimbia na visima ili wawe na maji ya kutosha..

…Pia tunahamasisha uchimbaji wa mabwawa ili wakulima wa Tanzania taratibu waanze kuondoka kwenye kilimo cha kutegemea mvua waanze kufanya kilimo cha umwagiliaji, kwa kweli mwitikio ni mkubwa,”amesema Msigwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks