Ongezeni kasi ya matumizi fasaha ya Kiswahili- Majaliwa

January 27, 2022 1:36 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu wa Tanzania. Mhe, Kassim Majaliwa Majaliwa leo Januari 27, 2022 ametoa Tuzo ya Kiswahili ya Mabati -Cornell ya Fasihi ya Afrika kwa washindi wa mwaka 2021 jijini Dar es Salaam. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Aagiza kiwepewe kipaumbele katika maeneo mbalimbali iiwemo ya utoaji wa huduma za jamii.
  • Watalaama watakiwa kuweka mikakati kukiendeleza kimataifa.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza matumizi fasaha ya lugha ya Kiswahili yapewe kipaumbele katika maeneo mbalimbali nchini yakiwemo ya utoaji wa huduma za jamii, mikutano, mahakamani, warsha na makongamano yatakayofanyika ndani na nje ya nchi.

Kutekeleza agizo hilo, Majaliwa ameagiza wataalam wa lugha ya Kiswahili kutoka vyuo vikuu na kutoka Mabaraza ya Kiswahili Tanzania (Bakita) watumike kikamilifu katika kushauri na utekelezaji wa mikakati ya kuendeleza lugha ya kiswahili nchini. 

“Matumizi ya lugha ya Kiswahili yaimarishwe katika kutoa huduma za kimahakama na uandishi wa nyaraka za kisheria pamoja na kutafsiri sheria mbalimbali yafanyike kwa lugha ya Kiswahili ili kuwawezesha Watanzania kutambua haki zao lakini kuijua sheria yenyewe.”

Majaliwa ametoa maagizo hayo leo (Januari 27, 2022) katika hafla ya kutoa tuzo kwa washindi wa uandishi katika Shindano la Tuzo ya Kiswahili ya Mabati- Cornell ya Fasihi ya Afrika 2021 katika ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City, jijini Dar Es Salaam.

Pia ameziagiza Wizara za Elimu, Sayansi na Teknolojia, Wizara ya Sanaa, Utamaduni na Michezo na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki zishirikiane kujenga uwezo wa wataalam wa ndani wa kutafsiri lugha mbalimbali za kigeni.

“Wizara ya elimu iendelee kufanyia kazi mkakati wa kukitumia Kiswahili kufundishia katika ngazi mbalimbali za elimu na kuongeza wataalam wa lugha hiyo katika ngazi ya uzamivu. 

“Mafunzo ya lugha ya Kiswahili yaimarishwe kwa kutoa programu maalum kwa ajili ya kuzalisha wataalamu na wakalimani wa Kiswahili wenye kukidhi viwango vya Kimataifa,” amesema Majaliwa. 


Soma zaidi:


Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji imeagizwa hakikisha kuwa  bidhaa zote zinazozalishwa katika viwanda vya ndani na zile zinazoingizwa nchini kutoka nje zinakuwa na maelekezo yaliyotolewa kwa lugha ya kiswahili. 

“Kufanya hivyo, kutawafanya watumiaji wa bidhaa hizo wazitumie wakiwa wanafahamu vyema maelekezo yaliyomo katika bidhaa hizo,” amesema.

Lugha ya Kiswahili ambayo ina wazungumzaji zaidi ya milioni 100 duniani.

Akizungumzia maagiza hayo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohammed Mchengerwa ametoa wito kwa wataalamu wa lugha ya Kiswahili wasilale na badala yake wachangamkie fursa zitokanazo na matumizi ya lugha hiyo katika Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Afrika kama ukalimalini.

“…tutaendelea na jukumu hili kwa jitihada na kasi kubwa ya kuhakikisha Kiswahili kinaendelea kukua zaidi na pia dunia itambue kuwa nchi ya Tanzania ndiyo chimbuko la lugha ya kiswahili na ipewe kipaumbele cha kufundisha lugha hiyo. Tuandae kanzidata ya kuwatambua wataalamu wote wenye ufahamu wa kwenda kufundisha lugha ya kiswahili kwenye nchi mbalimbali,” amesema Mchengerwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya Alaf, Ashish Mistry ambao ndiyo wadhamini wa mashindano hayo amesema kampuni yao inatambua umuhimu wa lugha ya kiswahili katika mchango wake mkubwa kukuza uchumi. 

Amesema wamedhamini wanafunzi sita kusomea shahada ya uzamili ya lugha ya Kiswahili na kati yao watatu wameshahitimu.

Enable Notifications OK No thanks