Lhrc yaeleza sababu kuendelea kwa mauaji ya wanawake, ikitoa suluhu

December 6, 2022 11:03 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ushirikina na kukosekana kwa uhuru wa kiuchumi wa kundi hilo muhimu nchini kwachangia.
  • Yataka mabadiliko ya sheria kuwalinda wanawake.

Dar es Salaam. Kufuatia mauaji ya wanawake yanaendelea Tanzania, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeeleza sababu mbalimbali za kushamiri kwa vitendo hivyo ikiwemo sheria kandamizi na kukosekana kwa uhuru wa kiuchumi wa kundi hilo muhimu nchini.

Hivi karibuni kumeripotiwa matukio kadhaa ya kikatili dhidi ya wanawake yakiwahusisha wenza wa ndoa, ukatili wa kingono pamoja na yale yasiyohusisha wenza wa ndoa.

Mathalan, Hamida Mussa, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St Augustine (SAUT) tawi la Mwanza alidaiwa kuuawawa kwa kunyongwa shingoni na mtandio akiwa nyumbani kwake Novemba 28, 2022.  Tukio hilo linadaiwa kutekelezwa na binti wa kazi aliyekuwa akiishi naye.

Kwa mujibu wa LHRC, matukio ya ukatili dhidi ya wanawake yamekuwa yakiongezeka nchini ambapo kimesema taarifa za Jeshi la Polisi zinaonyesha mwaka 2020 kulikuwa na matukio 531 na mwaka jana yakaongezeka hadi 554.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Wakili Anna Henga akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo Disemba 6, 2022, amesema ukatili wa kijinsia  ni moja ya kisababishi cha kuongezeka kwa mauaji ya makusudi ya wanawake.

“Kuongezeka kwa ukatili wa kijinsia  kumeendelea kutishia jamii zetu, mauaji ya makusudi ya wanawake yameendelea kuongezeka kila siku na kutishia usalama wa wanawake,” amesema Henga.

                    

Mambo mengine yaliyotajwa na kituo hicho yanayochangia kuongezeka kwa mauaji ya wanawake ni pamoja na uwepo wa sheria ambazo zinadaiwa kuwa kandamizi ikiwemo ya  Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 na Sheria ya Mirathi ya Kimila ya mwaka 1963.

“Kutokuwepo kwa sheria maalum ya ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani kumeendelea kuleta  changamoto katika kupambana na vita dhidi ya ukatili na mauaji ya makusudi ya wanawake,” amesema mkurugenzi huyo.

Kukosekana  kwa uhuru wa kiuchumi, elimu duni, mila na desturi zilizopitwa na wakati pamoja na ukosefu wa elimu, LHRC imesema kunachangia kuwakandamiza wanawake kwa ukatili wa aina mbalimbali.


Zinazohusiana


Mapendekezo ya kumaliza mauaji ya wanawake yatolewa

Serikali imeshauriwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu hali za wanawake, watoto, wasichana na haki za binadamu pamoja na kuboresha huduma za jamii, haki na kuhakikisha wanawake wanapata msaada pale wanapofanyiwa ukatili.

“Tunaitaka Serikali kutunga sheria mahususi ya kupinga ukatili wa kijinsia au ukatili wa majumbani kwa ajili ya kuhakikisha usalama zaidi wa wanawake dhidi ya ukatili wa kijinsia na ukatili wa majumbani,” amesema Henga mbele ya wanahabari.

Jeshi la Polisi, kituo hicho kimependekeza kuongeza vituo vya madawati ya jinsia pamoja na nyumba salama ili kuilinda jamii na mauaji ya wanawake hasa maeneo ya vijijini.

Kituo hicho kimewataka wanawake kuachana na mawazo mgando yanayoendelea kuwakandamiza wanawake bali kuendelea kuwa mashujaa dhidi ya ubaguzi na kushirikisha jamii kuondoa aina zozote za ukatili.

“Wanawake kutoa taarifa kuhusu ukatili hata pale wanapoona wenzao wanafanyiwa na kutoa msaada kwa wenzao kwa kuacha kusimamia mfumo dume na kandamizi,” amesisitiza Henga. 

Maoni ya LHRC, yametolewa wakati dunia ikiadhimisha siku  16 za kupinga ukatili wa kijinsia ambazo huadhimishwa kuanzia tarehe 25 Novemba hadi tarehe 10 Disemba.

Kwa mwaka maadhimisho hayo duniani yana kaulimbiu isemayo “Tuungane pamoja kuendeleza harakati za  ukatili dhidi ya wanawake na wasichana” huku  Ujumbe wa Tanzania ukisema “kila uhai una thamani komesha mauaji ya wanawake na ukatili dhidi ya wanawake na watoto”.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW