Mbinu za kuepuka tabia zinazoathiri maisha yako

August 12, 2021 10:18 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Urahibu au tabia hatarishi huanza na mtu kutaka kujaribu kitu fulani na kujikuta ana mazoea nacho.
  • Hali hiyo humfanya mtu kuwa mtumwa wa tabia au kitu fulani.
  • Urahibu unaweza kuvunjwa kwa mtu kuweka nia na kusimamia msimamo wake.

Dar es Salaam. Unaweza kuwa mwepesi kunyooshea watu wengine vidole kwa kuwa  mto waliouvuka wenzio bado haujauvuka.

Unaweza kuwa mto wa matumizi ya pombe ya kupindukia, dawa za kulevya, ngono na manunuzi yasiyofaa ya fedha na mwili.

Tovuti ya habari za afya ya Medical News, imeandika, tabia yoyote ambayo imekuwa ni urahibu kwa mtu huanza na uamuzi wa kuchagua. Mfano, mtu anakuwa na uchaguzi wa kunywa pombe au kutokunywa ama kutumia dawa za kulevya au kutokutumia.

Kituo cha kusaidia kuondoa (detox) sumu inayotokana na madawa ya kulevya na pombe cha nchini Marekani (Ascendant)  kimeandika urahibu una hatua kuu tano ambazo ni majaribio, matumizi ya mara kwa mara, utegemezi, urahibu na hatua ya mwisho ikiwa ni tiba na kupona.

Pale mtu anapochagua kutumia kitu na kupata matokeo anayoyafurahia, ataendelea kukitumia mara kwa mara hivyo akili yake itaanza kujenga tabia ya uhitaji wa kitu hicho na muda mwingine kujihisi hajakamilika bila kutumia au kufanya kitu hicho.

Wapo ambao bila kunywa pombe hawawezi kulala, na wengine mawazo yao hupoa wanapovuta sigara au kula. Ni urahibu ambao ni matokeo ya tabia kuwa mazoea.

Tabia hizo huwa na athari kama mtu hawezi tena kujisimamia au zinaathiri maisha yake ya kawaida.

Urahibu unaweza kuwa wa matumizi ya simu na kwa wengine, upweke.Picha| Google Images.

Njia za kukabiliana na urahibu ni zipi?

Kuna mtu niliwahi kumsikia akisema, “kama ni pombe si unaacha tu kunywa?” lakini ni wazi kuwa alikuwa hajavuka mto ambao mtumiaji wa pombe aliyekuwa anamuongelea ameuvuka.

Kuondokana na urahibu siyo  kitu chepesi kama baadhi wanavyodhani. Kunaambatana na changamoto za kimwili, kiakili na za kisaikolojia ambazo zinasababisha kuuvunja urahibu kuwa jambo gumu. 

Hata hivyo, kwa mpango na rasilimali sahihi, urahibu unaweza kuvunjwa na mtu aliye tayari.

Kupata nasaha

Licha ya kuwa hii siyo tamaduni ya Kitanzania lakini tafiti mbalimbali zinaeleza kuwa inasaidia watu kuvunja urahibu wao. Muda mwingine, urahibu wako unaweza kukoma kwa kupata mtu wa kukusikiliza na kukupatia mawazo yanayoweza kukujenga.

Wapo wataalamu waliosomea masuala ya saikolojia ambao wana uwezo wa kumsaidia mtu kwa njia za kitaalamu kuvunja urahibu wake.

Unaweza kuongea na watu wako wa karibu pia na kuwaeleza mpango wako wa kuvunja urahibu ili wakusaidie pia kwa kukuwekea mazingira rafiki ili kuvunja tabia usizozipenda.

Endapo unatumia pombe na unataka kuacha, rafiki zako wa karibu unaweza kuwaambia ili nao wasitumie wakiwa na wewe. Itakusaidia kukuepushia kiu ya pombe hiyo.


Tangazo


Tafuta vitu vya kukushughulisha

Wakati mwingine inaweza kuwa ni kwa sababu una muda mwingi kiasi cha kupata nafasi ya kupata vishawishi. Mfano, endapo mtu hana ajira, ni rahisi kuona matumizi ya dawa za kulevya kama lango la kupotezea muda hivyo kujikuta akitumia mara kwa mara.

Kwa mtu ambaye ameathirika na urahibu, anaweza kutafuta vitu vya kumshughulisha ikiwemo kufanya mazoezi, kucheza michezo au kujiunga na vilabu vya kijamii (social clubs) ambako atakuwa anatumia muda wake zaidi.

Badilisha mazingira yako

Kwa mfano mtumiaji wa sigara, atawezje kuacha kuvuta sigara kama mazingira yake yametawaliwa na watu wanaovuta sigara? Au mtu mwenye urahibu wa ngono, atawezaje kuvunja tabia hiyo endapo amezungukwa na watu wanaoongelea ngono muda wote ama yupo kwenye makundi ambayo kutuma video na picha za utupu siyo changamoto? 

Hayo ni mazingira yanayochochea mtu kushindwa kuvunja urahibu wake.

Unaweza kutafuta mazingira rafiki zaidi kwa kujenga tabia mpya ikiwemo kusoma vitabu badala ya kuangalia video za ngono, kutembelea fukwe badala ya kuvuta sigara na washikaji na kutumia muda na familia yako ambao watakusaidia kubaki kwenye tabia njema.

Tovuti ya Verywell Mind inashauri kuwa wakati mwingine inaweza kukulazimu kubadili hata njia unayoipita ili kuepukana na mazingira chochezi.

Unaweza kuongea na watu unaowaamini ili wakusaidie katika juhudi zako za kuvunja urahibu. Picha| Metamorphosis Life Revitalizing Center.

Punguza au acha kwa malengo

Kuacha kufanya kitu kilichozoeleka siyo rahisi kama kuchukua peremende kwa mtoto. Inahitaji maandalizi na utayari kwa mujibu wa tovuti ya shule ya afya ya Havard.

Havard inashauri kuweka tarehe ya kuacha tabia hiyo. Inaweza kuwa siku ya kumbukizi ya kuzaliwa, ndoa na hata msiba wa mtu unayempenda. Itakusaidia kuweka msisitizo kwenye kuachana na tabia hiyo.

Unaweza kupunguza kidogo kidogo tabia hiyo na kupunguza siku za kufanya au kutumia kitu ulichozoea.

Pia inashauriwa kufikiria vitu vilivyokufelisha kama uliwahi kujaribu kuvunja mnyororo wako wa urahibu.

Changamoto za kuchana na urahibu

Mara nyingi watu hushindwa kuachana na tabia zao za mazoea kwa sababu ya vitu vidogo vidogo ikiwemo “kujaribu mara ya mwisho”. Mfano mtu anaweza akawa ameanza mpango wa kutokujihusisha na matumizi ya sigara kwa siku 30 mfululizo lakini wazo la kujaribu kwa mara ya mwisho likampata kwenye siku ya 10. 

Hiyo itamfanya kushindwa kuvunja mnyororo wake wa tabia. Watu wenginne hulazimisha tabia zao kuwa sahihi kwa kusema “sifanyi peke yangu” na wengine kusema “kama kufa tutakufa siku ikifika” hivyo kujikuta wakiendelea na tabia zao.

Muhimu ni kuweka mpango wako, na kusimamia maamuzi yako kwani kama ulivyokuwa na uwezo wa kuanza kufanya kitu fulani, una uwezo pia wa kuacha.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW