Tabia zitakazokusaidia kuepuka madhara ya unywaji wa pombe uliopitiliza
- Tabia nzuri za kunywa pombe ni kuitumia bila kuwa na shinikizo lolote iwe furaha au huzuni.
- Kwa baadhi wakizidisha hujikuta katika matatizo ikiwemo ajali za barabarani.
- Inashuriwa kuwa na ndugu au rafiki wa kukusaidia mahala pote unapokunywa pombe mbali na nyumbani.
Dar es Salaam. Kwa popote ulipo, bila shaka itakuwa jambo la kawaida kuona watu wakiwa peke yao au kwa makundi katika sehemu za starehe au migahawa wakitumia “ulabu” kama sehemu ya kujiburudisha na kupitisha muda.
Hata hivyo, matumizi ya pombe siyo kesi bali matokeo yake kwa wale ambao huzidisha kipimo cha unywaji ndiyo huibua mjadala kwenye jamii hasa kuhusu tabia, maadili na uadilifu wa mtu.
Baadhi hunywa pombe kwa ajili ya kujistarehesha au kupoteza mawazo lakini wanaposhindwa kujisimamia, pombe huwaacha katika hali ya aibu huku baadhi wakisababisha maumivu yasiyofutika kwa wawapendao.
Pombe inaweza kuwa chanzo cha ajali, ukatili wa kijinsia na kuvunjika kwa mahusiano kwenye jamii.
Ili kuepukana na matatizo ya unywaji wa pombe uliopitiliza, haya ni mambo baadhi ya kuzingatia kabla na wakati ukitumia kichwaji hicho:
Kunywa pombe pale unapokuwa umemaliza majukumu
Muda gani unafaa kunywa ulabu? Baadhi hupendelea kunywa kinywaji hicho wakati wa jioni lakini wengine mchana, asubuhi, muda wowote ni “kanyaga twende”
Mchambuzi wa masuala ya kijamii, Rama Msangi ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa ni vyema kunywa pombe kwa kusudi na unapoamua kwenda kunywa pombe, ni muhimu kujiwekea kiasi cha pombe ambazo utakunywa na kuheshimu maamuzi hayo.
“Ni vyema pia kujenga mazoea ya kuongozana na mtu au watu ambao wanaweza kuchukua hatua pale unapozidiwa. Mathalan, ndugu au rafiki wa karibu ambaye ikitokea umezidiwa anaweza kukukataza kuendelea kunywa, kuendesha gari na kufanya fujo na akakufikisha nyumbani salama,” amesema Msangi.
Baadhi ya watu wamekuwa na tabia ya kunywa pombe na kisha kuendesha magari. Jambo hilo ni sababu la baadhi ya ajali za barabarani. Picha| Businesstech.
Kutokunywa pombe kwa muongozo wa hisia
Kwa baadhi ya watu, pombe huwa faraja pale wanapokuwa na huzuni na hata wanapokuwa kwenye furaha, kinywaji hicho ni sehemu ya sherehe zao.
Ni katika nyakati hizo za furaha na huzuni ambapo watu hao hujikuta wakizidisha kiwango cha matumizi yake na kujikuta katika aibu na changamoto za maisha.
Mfanyabiashara wa mkoani Dar es Salaam, Peter Mashauri amesema pombe ni sehemu ya sherehe na hata huzuni hivyo watumiaji wanatakiwa kuwa makini ili kuepuka mambo yasiyofaa.
“Watu wengi wameaibika wakiwa mashereheni kama harusi na wengine kutokana na huzuni, wamejikuta wakinywa pombe kupita kiasi na kujisababishia matatizo ikiwemo ajali za barabarani na hata kupata magonjwa,” amesema Mashauri.
Kutokunywa pombe kwa mashindano
Kuna baadhi ya sehemu watu hutaka kuonyeshana “umwamba” wa nani anaweza kunywa pombe nyingi zaidi au nani anakunywa pombe kali zaidi.
Ni mazingira hayo ambayo huwaacha baadhi ya wanywaji wakiwa wamelewa tofauti na walivyotarajia.
Mkazi wa Morogoro, Irene Mshumbusi amesema hilo huwa ni jambo la kawaida kwenye makundi rika na mara nyingi, “huwatokea puani”.
Mama huyo amesema kuna kesi nyingi zimesikika za watu kushindana kunywa pombe wakiwa sehemu za starehe ikiwemo ufukweni na kisha watu hao kuzama kwa kushindwa kuogelea.
“Mtu unashindana kunywa pombe kali kisha unaingia kwenye maji kuogelea au unaendesha gari, ni sababu ya vifo vingi vya vijana wanaotumia pombe,” amesema Mshumbusi.
Matumizi ya pombe huambatana na madhara mbalimbali. Usiache kuendelea kufuatilia sehemu ya pili ya makala haya kupata ushauri wa kitaalamu wa madhara ya matumizi ya pombe na jinsi ya kuacha.