Jinsi ya kuvumilia udhaifu wa mwenza wako katika ndoa

April 20, 2026 7:11 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni pamoja na kujifunza namna ya kumtunzia heshima na kupunguza matarajio.

Dar es Salaam. Ndoa ni safari ndefu na ya kipekee inayowakutanisha watu wawili wenye historia tofauti, wakiwa na ndoto ya kujenga mahusiano ya kudumu kwa mujibu wa misingi ya imani au misingi waliyonayo.

Licha ya uwepo wa ndoto hiyo, mara nyingi safari hiyo hukumbwa na milima na mabonde ambayo huweza kuitishia au kuitamatisha mapema kuliko ilivyotarajiwa.

Takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita) zinaonyesha kuongezeka kwa idadi ya talaka nchini Tanzania hali inayoweza kuwakatisha tamaa mamia ya wanawake na wanaume wanaotamani kuianza safari ya ndoa.

Kwa mujibu wa Rita , talaka zimeongezeka kwa asilimia 59.1 ndani ya mwaka mmoja kutoka talaka 447 zilizokuwepo mwaka 2022 hadi talaka 711 zilizorekodiwa mwaka 2023.

Mwanasaikolojia wa mahusiano, ndoa na malezi Deo Sukambi, ameiambia Nukta Habari kuwa miongoni mwa sababu za ndoa hizo kuvunjika ni wanandoa kushindwa kuchukuliana madhaifu waliyonayo pamoja na kushindwa kuheshimiana.

“Ndoa nyingi huvunjika pale heshima inapopotea. Na pale heshima inapopotea, hata jambo dogo hugeuka kuwa kubwa kuliko uhalisia wake,” anafafanua Sukambi.

Hata hivyo, kuvumilia si kukubali maumivu yasiyo na mwisho, bali ni uwezo wa kujenga daraja la uelewa katikati ya mapungufu ya mwanadamu.

Kwa kuona umuhimu wa suala hilo Nukta habari inakuletea mbinu saba zitakazokuwezesha kuvumilia  udhaifu wa mwenza wako katika ndoa.

Mbali na talaka mgogoro ndani ya ndoa huweza kuwa chanzo cha matatizo ya afya ya akili na magonjwa yasiyoambukiza. Picha| Free Pik.

Kupunguza matarajio

Matarajio makubwa yasiyo halisi ndiyo chanzo kikubwa cha maumivu katika ndoa nyingi. Watu wanapotarajia wenza wao wawe wakamilifu au wabadilike haraka, huishia kuvunjika moyo.

Sukambi anafafanua kuwa ni muhimu kuelewa kuwa baadhi ya tabia ni sehemu ya mtu, na hubadilika kwa muda. 

Hivyo, kupunguza matarajio kunasaidia kupunguza msongo wa mawazo na kuongeza utulivu ndani ya uhusiano.

“Kadiri unavyoongeza matarajio yasiyo halisi, ndivyo unavyoongeza maumivu moyoni mwako. Lakini unapojifunza kupunguza matarajio, unafungua nafasi ya kuona uhalisia wa mtu na kumkubali alivyo,” anasema Sukambi.

Kuzingatia mazuri badala ya mabaya 

Ni rahisi sana kuzama kwenye madhaifu tisa ya mwenza wako na kusahau uzuri mmoja mkubwa alionao.

Ukijifunza kuangalia mazuri, thamani ya mwenza wako itaanza kuonekana upya, jambo ambalo huongeza shukrani na kupunguza malalamiko.

Fatma Shame (60), aliyedumu katika ndoa kwa miaka 38 anasema ni vyema kuelewa mapungufu ya mwenza (kama vile kutokuwa msafi sana) huku ukizingatia upendo na huduma nyingine nzuri anazotoa.

“Unaweza kuolewa na mwanaume mchafu na hata ukimrekebisha vipi habadiliki unafanyaje ukiangalia anakupenda, anakuhudumia vizuri, ni basi tu ndio kasoro yake unafanyaje sasa zaidi ya kumvumilia,” anaeleza Shame mkazi wa jijini Tanga.

Kukubali kwamba hakuna mkamilifu 

Viongozi wa dini na wanasaikolojia wanakubalina kuwa hakuna binadamu mkamilifu, hivyo katika ndoa ambayo kimsingi huundwa na watu wawili hapatakuwa na mkamilifu pia.

Kukubali hali hiyo kunakusaidia kuwa na subira na uelewa zaidi. Badala ya kulazimisha mabadiliko, unajifunza kuishi na tofauti zenu kwa amani.

“Ukikubali kwamba hakuna mkamilifu duniani, utaacha kupigana vita visivyo na mwisho ndani ya ndoa yako. Na hapo ndipo utapata nafasi ya kujenga upendo unaovumilia, unaoelewa na unaokua kila siku.” ameongeza Sukambi.

Ili kudumu katika ndoa kwa muda mrefu ni vyema wanandoa wakajifunza kusameheana na kuacha kutunza hasira kwa muda mrefu. Picha| Free Pik.

Kuondoa fikra kwamba anakukosea makusudi

Mara nyingi watu huumia zaidi kwa kuamini kwamba wenza wao wanawakosea kwa makusudi. Fikra hii huongeza hasira na kuharibu mawasiliano.

Lakini Sukambi anaeleza kuwa baadhi ya tabia ni sehemu ya malezi au uzoefu wa mtu. Hivyo ukiondoa fikra hii, unapata nafasi ya kuelewa badala ya kuhukumu.

Kujenga tabia ya kuamini na kusamehe

Kuamini na kusamehe ni nguzo muhimu katika ndoa. Bila haya, mahusiano hubeba mzigo mkubwa wa maumivu ya zamani na mashaka ya mara kwa mara.

Kumpa mwenzi nafasi nyingine ni ishara ya kuchagua kuendelea mbele. Hata hivyo, ni muhimu kufanya hivyo kwa hekima na kuweka mipaka inayolinda utu wako.

 Kubadili mtazamo (cognitive reframing)

Tovuti ya National Library of Medicine (NIH) inaeleza kuwa namna unavyotafsiri tabia ya mwenza wako huathiri moja kwa moja hisia zako. 

Badala ya kuona udhaifu kama tatizo lisilobadilika, jaribu kuutazama kama changamoto anayoweza kuboresha. Kwa mfano, badala ya kumwita mwenza “mvivu,” unaweza kusema “ana changamoto ya kupanga muda”. 

Pia, ondoa fikra kuwa anakukosea kwa makusudi mara nyingi tabia hizo hutokana na malezi au uzoefu wa nyuma.

Ndoa yenye furaha hutengeneza mazingira mazuri kwa ajili ya ustawi na ukuaji wa watoto.Picha|Free Pik.

Fikiria kwanini madhaifu fulani yanakukera sana
Kwa mujibu wa tovuti ya psychology today, wakati udhaifu mmoja wa mwenza wako unakukera, mara nyingi ni kwa sababu unampa maana zaidi 

Tovuti hiyo inaongeza kuwa, chunguza kwa makini maana ya ziada unayoipa hisia zako za kuchukizwa kuhusu madhaifu ya mwenza wako. 

Ikiwa una tabia ya kuwa na wasiwasi (anxiety), madhaifu yao yanaweza kuchochea wasiwasi huo kwako. Ikiwa mara nyingi unahisi kutopendwa au kutojaliwa (kwa kawaida kutokana na uzoefu wako wa zamani), basi madhaifu yao yanaweza kuchochea hisia hizo. 

Marufuku kuvulimia unyanyasaji

Kulingana Sukambi uvumilivu wa jambo hutegemea na namna mtu anavyoweza kupokea kila jambo, ingawa iwapo kuna mambo ambayo yanahatarisha utu na uhai wako hayapaswi kuvumiliwa. Miongoni mwa mambo hayo kwa mujibu wa Sukambi ni pamoja na  unyanyasaji wa kimwili.

Kupigwa au kuumizwa kimwili ni jambo hatari sana ambalo halipaswi kuvumiliwa kwa hali yoyote. Sukambi anaeleza kuwa hili si suala la uvumilivu bali ni suala la usalama wa maisha yako.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA)

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI OFISI YA MAKAMU WA RAIS (MUUNGANO NA MAZINGIRA)

Nukta TV

Yaliyojiri Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana ikisomwa kwa mara ya kwanza

Yaliyojiri Bajeti ya Wizara ya Maendeleo ya Vijana ikisomwa kwa mara ya kwanza

Nukta TV

Maendeleo ya Vijana yaomba kuidhinishiwa Sh35.9 bilioni bajeti 2026/27

Maendeleo ya Vijana yaomba kuidhinishiwa Sh35.9 bilioni bajeti 2026/27

Nukta TV

BENEFIT FROM
Nukta ADS
Advertise with us to reach a wider audience with high conversion rates.
Other Nukta Africa Products
Nukta Habari
Stories that matter
Topics
Inuldge yourself with the topics in Nukta
All
Business
Africa
Contact
Tel
+255 750 881 888
Mail
newsroom@nukta.co.tz
Address
Mwananyamala kwa Kopa Dabe House Dar es Salaam TZ, 14108
Social Media

© 2024 Nukta Africa. All Rights Reserved.