Maumivu: Bei ya petroli, dizeli yapanda miezi mitatu mfululizo

May 5, 2021 7:12 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 
  • Bei hizo zimepanda kwa viwango tofauti kati ya Machi na Mei.
  • Bei ya petroli mkoani Dar es Salaam sasa yavuka Sh2,000 kwa lita.

Dar es Salaam. Bei ya petroli na dizeli zimeedelea kupanda kwa miezi mitatu mfululizo nchini Tanzania, habari ambayo huenda ikawaumiza vichwa wamiliki wa vyombo vya moto wanaotumia nishati hizo katika shughuli mbalimbali. 

Kuongezeka kwa bei hizo ambazo zimekuwa zikipanda kwa viwango tofauti tangu mwezi Machi mwaka huu kunatokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ya bei mpya kikomo za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mwezi Mei zinazoanza kutumika leo, inaeleza kuwa bei ya rejareja za petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 2.17.   

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalipia Sh2,169 kwa lita ikiwa ni Sh46 zaidi katika bei ambayo walikuwa wananunulia petroli mwezi Aprili. 

Kwa watumiaji wa dizeli, wao watanunua lita moja kwa Sh2,038 ikiwa ni ongezeko la Sh43 kwa lita, kutoka Sh1,996 bei waliyotumia mwezi uliopita.

Tofauti na mwezi uliopita, bei za mafuta ya taa pia zimepanda kwa asilimia 5.1 sawa na ongezeko la Sh94 katika bei zilizotumika mwezi Aprili na hivyo kufikia Sh1,957 kwa lita moja.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje katika taarifa iliyotolewa na Ewura jana. 

Aidha,  ikilinganishwa na mwezi Aprili, bei za jumla za petroli zimeongezeka kwa asilimia 2.3, dizeli (asilimia 2.3) sawa na mafuta ya taa yakiongezeka kwa asilimia 5.4 sawa na Sh93.3 kwa lita moja.


Soma zaidi:


Maumivu hayo  hayataishia kwa wakazi wa Dar es Salaam tu bali mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, inayotumia mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa mwezi Mei bei za rejareja za petroli imeongezeka kwa Sh90 sawa na na dizeli ni Sh174 kwa lita moja.

“Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe 7 Aprili 2021. Hii ni kwa sababu, kwa Aprili 2021 hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” imeeleza Ewura.

Kwa Mikoa ya Mtwara, Lindi, na Ruvuma bei pia zimeongezeka  ikilinganishwa na bei za mwezi uliopita. 

Bei za rejareja za petroli imeongezeka kwa Sh147 kwa lita (asilimia 6.84) na dizeli imeongezeka kwa Sh42 kwa lita moja sawa na asilimia 2.07.

Kisheria, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura  itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. 

Ewura katika taarifa hiyo imesema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo.

Enable Notifications OK No thanks