Mifuko kutoboka: Bei ya petroli, dizeli yapanda kwa miezi miwili mfululizo Tanzania

April 8, 2021 1:11 pm · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link
  • Zimepanda mwezi Machi na Aprili kutokana na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 
  • Bei hizo zimepanda kwa viwango tofauti isipokuwa kwa mafuta ya taa.
  • Bei ya petroli mkoani Dar es Salaam sasa yavuka Sh2,000 kwa lita.

Dar es Salaam. Bei ya petroli na dizeli imepanda kwa miezi miwili mfululizo nchini Tanzania, jambo linalowafanya wamiliki wa vyombo vya moto kutoboa zaidi mifuko yao ili kuipata nishati hiyo muhimu katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi. 

Bei hizo za mafuta zilizopanda kwa viwango tofauti tangu mwezi Machi mwaka huu ni kutokana na kupanda kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji. 

Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) ya bei mpya kikomo za mafuta ya petroli, dizeli na mafuta ya taa kwa mwezi Aprili zilizoanza kutumika Aprili 7 mwaka huu, bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 7.18.   

Kutokana na ongezeko la bei hiyo, watumiaji wa vyombo vya moto watalipia Sh142 kwa lita zaidi ya bei ambayo walikuwa wananunulia petroli mwezi Machi. 

Sasa, wakazi wa mkoa wa Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,123 ikiwa imepanda kutoka Sh1,981 iliyotumika mwezi uliopita. 

Kwa bei hiyo inayotumika mwezi huu wa Aprili ambayo imevuka Sh2,000 ni kiwango cha juu kuwahi kurekodiwa tangu Aprili mwaka jana ambapo iliuzwa kwa Sh2,087. 

Watumiaji wa dizeli wao watanunua lita moja kwa bei ya rejareja ya Sh1,996 kwa lita likiwa ni ongezeko la Sh85 kwa lita, kiwango ambacho kimesalia kidogo kufikia Sh2,000. 

Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la Machi 3, 2021 kwa sababu katika kipindi cha mwezi uliopita hakuna shehena ya mafuta ya taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Dar es Salaam.

“Mabadiliko haya ya bei yanachangiwa na kubadilika kwa bei za mafuta katika soko la dunia na gharama za usafirishaji,” amesema Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Godfrey Chibulunje katika taarifa iliyotolewa na Ewura.


Soma zaidi:


Vilevile, ikilinganishwa na toleo la mwezi uliopita, bei za jumla za petroli  zimeongezeka kwa Sh141.9 kwa lita huku dizeli ikiongezeka kwa Sh84.9 sawa na asilimia 4.7.

Maumivu hayo pia yatawagusa watumiaji wa nishati hiyo wa mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na Manyara, inayotumia mafuta yanayopitia Bandari ya Tanga ambako nako bei imepanda. 

Kwa mwezi Aprili 2021, bei ya rejareja ya petroli imeongezeka kwa Sh73 na dizeli imeongezeka kwa Sh105 kwa lita. 

“Bei za mafuta ya taa hazina mabadiliko na zitaendelea kuwa zile zilizotangazwa katika toleo la tarehe 3 Machi 2021. Hii ni kwa sababu, kwa mwezi Machi 2021 hakuna shehena ya Mafuta ya Taa iliyopokelewa kupitia bandari ya Tanga,” amesema Chibulunje katika taarifa hiyo. 

Pia kwa mwezi Aprili kama ilivyokuwa mwezi Machi mwaka huu, bei za rejareja na jumla kwa mafuta ya petroli na dizeli kwa mikoa ya Kusini ya Mtwara, Lindi na Ruvuma inayotumia mafuta yanayopitia bandari ya Mtwara zimeongezeka ikilinganishwa na bei zilizotolewa Machi 3, 2021. 

Kwa Aprili 2021, bei ya rejareja ya petroli na dizeli zimeongezeka kwa Sh92 kwa lita na Sh200 kwa lita, mtawalia.

Kutokana na kupanda kwa bei hizo za mafuta kwa miezi miwili mfululizo, watumiaji watalazimika kutoboa zaidi mifuko yao ili kupata nishati hizo kufanikisha shughuli mbalimbali za maendeleo. 

Kisheria, bei za bidhaa za mafuta ya petroli zitaendelea kupangwa na soko na Ewura  itaendelea kuhamasisha ushindani kwa kutoa taarifa za bei kikomo za bidhaa za mafuta. 

Ewura katika taarifa hiyo imesema kampuni za mafuta ziko huru kuuza bidhaa za mafuta ya petroli kwa bei ya ushindani mradi tu bei hizo zisivuke bei kikomo.

Enable Notifications OK No thanks