Jinsi matapeli wanavyopora mamilioni ya Watanzania mtandaoni – 3

January 7, 2026 1:39 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Katika sehemu hii ya tatu na ya mwisho ya uchunguzi wetu, tunaangazia athari za utapeli wa bidhaa za mtandaoni, madhara kwa waliotapeliwa, uchumi na mustakabali wa biashara ya mtandaoni nchini na hatua inazochukua Serikali kukabiliana nazo.

Dar es Salaam, Mwanza, Arusha.

Sehemu kubwa ya watu tuliozungumza nao baada ya kununua bidhaa mtandaoni wametapeliwa kwa mfumo wa utapeli unaofanana licha ya kutapeliwa na matapeli tofauti waliopo mikoa tofauti. 

Idadi ya wanaotapeliwa hapana shaka inazidi kuongezeka pia na kwa mujibu wa uchambuzi wa maoni (comments) wa watumiaji wa mitandao katika baadhi ya akaunti zinazotuhumiwa kutapeli kwa kuwa hakuna taarifa sahihi za namna ya kuwabaini na kukabiliana nao. 

Hata baada ya kutapeliwa, sehemu kubwa hawaripoti polisi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo wanachodai mlolongo mrefu wa kuandikisha jalada na watuhumiwa kutochukuliwa hatua kwa haraka jambo linafanya mamlaka zikose taarifa sahihi na kuwachukulia hatua wahusika. 

“Aliniambia nimtumie nusu ya bei halisi ya simu (Sh150,000) lakini baada ya kutuma akaniblock kila mahali…nilijiona kama mjinga fulani hivi sikuchukua hatua zozote (hakumripoti polisi),” anaeleza Mkazi wa Mwanza, Fredrick Chibunga.

Miongoni mwa bidhaa zinazouzwa kwa bei ndogo licha ya kuonekana na ubora wa hali ya juu katika ukurasa wa mfanyabishara freedelivery89 anayehusishwa na utapeli mtandaoni.

‘Sheria kali, utekelezaji butu’

Utapeli wa mtandaoni ni kosa la jinai na lenye madhara makubwa kwa wanaotapeliwa na uchumi wa nchi kwa ujumla. 

Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015 inazuia matumizi haramu ya mtandao kufanya utapeli wa mali na iwapo mtu atakutwa na hatia atapigwa faini isiyopungua Sh20 milioni au mara tatu ya thamani ya faida iliyopatikana kinyume cha sheria au kifungo kisichopungua miaka 7 au vyote kwa pamoja.

Baadhi ya wanasheria wanaeleza kuwa vitendo vya utapeli vinaendelea kwa kuwa kuna udhaifu mkubwa katika utekelezaji wa Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Wakili wa kujitegemea Moses Basila, ameiambia Nukta Habari kuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao ina adhabu kali lakini haijadhibiti kikamilifu makosa ya mtandao kutokana na changamoto kubwa zikiwemo za mamlaka za kisheria (Jurisdiction), utekelezaji na kasi ya mabadiliko ya teknolojia. 

“Hivyo udhibiti wa asilimia 100 wa makosa ya mtandao bado ni changamoto, si Tanzania pekee bali kwa nchi nyingi duniani,” anasema Basila.

Kutokana na uwepo wa mianya hiyo ya kisheria, Basila anashauri Serikali kuimarisha matumizi ya mbinu za kidijitali katika kuwatambua na kuwakamata wahalifu.

Aidha, anawahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari wanapofanya manunuzi kupitia mitandao ya kijamii, hususan kuepuka akaunti zinazolazimisha malipo kabla ya kupokea bidhaa.

Utapeli unaua biashara halali mtandaoni

Kuongezeka kwa utapeli wa biashara za mtandaoni kunaathiri Watanzania wengi wanaotegemea mtandao kuuza bidhaa zao kupitia mitandao ya kijamii au tovuti (e-commerce) ili kujiingizia kipato. 

Uaminifu ni moja ya kigezo muhimu kinachochea utayari wa watu kununua bidhaa mtandaoni na kuchochea uchumi wa kidijiti. Tatizo hili si tu linaikumba Tanzania bali mataifa mengi duniani. 

Utafiti uliofanywa na Mhadhiri Dewi Puspitarini na wenzake wa Chuo Kikuu cha Catur Insan Cendekia mwaka 2021 nchini Indonesia ulibaini kuwa kuongezeka kwa udanganyifu kunashusha utayari wa watu kununua bidhaa na huduma mtandaoni.

“Kuongezeka kwa tovuti za kununua bidhaa mtandao kumefanya watu wengi watumie vibaya fursa hiyo…sehemu kubwa ya utapeli unaofanyika ni wauzaji kutopeleka bidhaa au kupeleka bidhaa yenye ubora hafifu tofauti kabisa na inayoonekana kwenye picha,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ijulikanayo kama “Hatari ya utapeli na imani katika nia ya kununua bidhaa mtandaoni (Fraud risk and trust on the intention to buy of e-commerce).

Iwapo utapeli huu hautadhibitiwa, Watanzania wengi hususan vijana watapoteza mali na ajira, hali itakayoathiri uchumi wa nchi hususan katika kipindi ambacho nchi nyingi duniani zinatumia fursa ya uchumi kidijiti. 

Sauti ya Emmy Zuberi mkazi wa Arusha akielezea jinsi utapeli ulivyomuachia madeni na kuua biashara yake.

Kalebu Gwalugano, Mwanzilishi wa kampuni ya Neurotech Africa inayomilki jukwaa la bidhaa mtandaoni linatumia akili unde kupitia WhatsApp la Ghala, anasema uwepo wa matapeli wa mtandaoni umesababisha kupungua kwa uaminifu miongoni mwa wateja, hali inayodidimiza wafanyabiashara wachanga.

“Kwa mfano, unamuona mfanyabiashara na kumtumia ujumbe wa WhatsApp ukimweleza kuwa tunataka kumuunganisha na mfumo wa kuuza kupitia WhatsApp, anakutukana kwa kudhani wewe ni tapeli, wakati nia yetu ni kusaidia kuuza bidhaa zao. Takribani asilimia 70 ya watu tunaowasiliana nao hutujibu kwa matusi,” anaeleza Gwalugano.

Kwa sasa, anasema, mfumo pekee unaoaminika zaidi na wateja wengi ni ule wa kulipia bidhaa baada ya mzigo kufika, utaratibu unaongezeka gharama za uendeshaji iwapo wateja watarudisha bidhaa au kutopokea tena simu baada ya kupelekewa mzigo. 

Hata hivyo, Gwalugano anasema mfumo huo unachukua muda mrefu kwa wateja wengi kukamilisha malipo, hali inayochelewesha mzunguko wa biashara.

Nchini Tanzania licha ya kutokuwepo Takwimu za moja kwa moja kuhusu kiwango cha utapeli wa bidhaa mtandaoni, Ripoti ya Takwimu za Uhalifu na Matukio ya Usalama Barabarani ya mwaka 2024 inabainisha kuwa utapeli wa mtandaoni (Computer related fraud) umeongezeka kwa zaidi ya mara mbili ndani ya mwaka mmoja kutoka matukio 57 mwaka 2023 hadi matukio 137 mwaka jana. 

Ripoti hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) na Jeshi la Polisi inaeleza kuwa matukio ya utapeli wa fedha kwa kutumia mitandao ya simu au kutoa fedha kutoka benki na kwenye mashine za kutolea pesa (ATMs) nayo yaliongezeka kwa asilimia takriban 10 ndani ya mwaka mmoja.

Utapeli unagharimu mabilioni

Kwa mujibu wa Ripoti ya Takwimu za Uhalifu na Usalama Barabarani ya mwaka 2024 matukio ya utapeli wa fedha yameongezeka hadi 4,091 Desemba 2024 kutoka 3,731 yaliyoripotiwa kipindi kama hicho mwaka 2023 na kusababisha watu kutapeliwa Sh5.3 bilioni huku watuhumiwa 465 wakitiwa mbaroni. 

Mkuu wa Mawasiliano na Uhusiano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania TCRA, Rolf Kibaja anasema wananchi wote wanaotapeliwa wanapaswa kuripoti kesi zao kwa Jeshi la Polisi kwa ajili ya hatua zaidi za kisheria.  

Jeshi la Polisi linaeleza kuwa utapeli wa bidhaa mtandaoni na mwingine kama huo unaongezeka Tanzania na duniani kote kutokana na mabadiliko ya haraka ya teknolojia yanayoleta mbinu mpya za kihalifu.

Mkurugenzi wa Kitengo cha Uhalifu na Makosa ya Mtandao cha Jeshi la Polisi, Joshua Mwangasa aliiambia Nukta Habari kuwa wanafanya jitihada mbalimbali kukabiliana na utapeli huo ikiwemo kujenga uwezo wa wataalamu wa ndani kuhusu mbinu mpya za uhalifu pamoja na kutoa elimu kwa wananchi kupitia kanda za kipolisi ikiwemo Dar es Salaam na Mwanza.

Miongoni mwa njia wanazotumia kuwajengea uwezo wataalamu hao ni pamoja na kuwapa ujuzi wa namna ya kuitumia teknolojia vyema na kuijua kwa kushirikiana na wadau wengine muhimu kama TCRA. Kuhusu takwimu za matapeli na wale waliofikishwa mahakamani, alieleza kuwa takwimu hizo zitapatikana baada ya ripoti ya mwaka 2025 kukamilika.

Pamoja na hayo, Mwangasa anasema wanafanya doria mtandaoni ili kubaini mapema vitendo vya uhalifu na kuwachukulia hatua kwa mujibu wa sheria wale wanaokutwa na hatia.

“Tunapoona viashiria inakuwa rahisi kuweza kuzuia au kuwataarifu ‘counterparts’ (wadau wetu)  kuwa kuna hiki na hiki kinaendelea hivyo tunajaribu kuzuia mapema,” anasema Mwangasa bila kuweka bayana kesi za utapeli mtandaoni zilizofikishwa mahakamani na kupatiwa hukumu kwa mujibu wa sheria.

Hivi karibuni Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, aliliagiza Jeshi la Polisi kuelekeza nguvu zaidi mtandaoni ambako kumekithiri vitendo vya utapeli akiwataka kuchukua hatua za mapema 

“Mahala ambapo wananchi wetu wanaumizwa zaidi ni kwenye makosa ya kimtandao, ambapo kwa nguvu yao wao hawana uwezo wa kupeleleza, hawana uwezo wa kumjua aliyemuibia isipokuwa sisi kama Serikali,” alisisitiza Waziri Simbachawene Januari 5, 2025 wakati akizungumza na viongozi wa Jeshi la Polisi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks