Jinsi mafanikio ya vijana yalivyofungwa kwenye matumizi ya muda

March 15, 2021 1:08 pm · Neema
Share
Tweet
Copy Link
  • Matumizi sahihi ya muda katika mambo sahihi, ndiyo mafanikio yao.
  • Kila sekunde inayopita ina thamani yake.

Muda ni kitu cha thamani alichopewa mwanadamu kuliko vitu vyote duniani. Mambo yote yamefungwa ndani ya muda unaotumia kila siku. 

Katika shughuli zote unazofanya za kijamii, kiuchumi na hata katika maisha ya kawaida nyumbani, muda ndiyo unatawala utekelezaji wa kazi zako.

Unautumia vipi muda wako? Ni kweli unataka kufanikiwa na kuwa na maisha mazuri kama kijana, lakini umewahi kujiuliza kuhusu matumizi ya talanta ya muda ambayo umepewa? Unazingatia muda kwa kila jambo unalofanya? Au umekuwa ni mtu wa kufanya tu mambo ili yaende pasipo kujali yanatatekelezwa kwa muda sahihi.

Jitafakari kijana mwenzangu, tangu unaamka asubuhi mpaka jioni unaenda kulala, umetumiaje muda wako? 

Jiulize zaidi, ni jambo gani linalotumia muda wako zaidi? Una faida na jambo hilo!? Ni jambo la kukuimarisha, kukuelimisha, kukufaidisha? 


Soma zaidi:


Hiyo ndiyo thamani ya muda katika maisha, ukipita hauwezi kuurudisha nyuma. Huenda kutofanikiwa katika baadhi ya mambo yako kunasababishwa na tabia yako ya kutokupangilia vizuri mambo yako kulingana na muda ulionao. 

Mara ngapi umevunja miadi na watu, umekosa kazi au biashara ambayo ingebadilisha maisha yako kwa sababu tu umeshindwa kuzingatia muda?.

Tafakari leo kuhusu muda. Siku moja yenye saa 24 unaweza kufanya mambo mengi mazuri ambayo yatakupatia fursa nzuri katika maisha. 

Kufanya jambo sahihi kwa wakati sahihi kutakupa matokeo sahihi na nafasi ya kuweka mambo sawa kama umekosea. Kimsingi kuishi nje ya muda ni gharama kubwa.

Hatari iliyopo ni kuwa tunafahamu muda mwingi tuliotumia au kupoteza kuliko muda tuliobaki nao katika maisha yetu.

                               

Nini cha kufanya?

Jifunze kutumia muda wako vizuri hasa wakati huu wa ujana ukiwa na nguvu ya kufanya maamuzi sahihi. Kuishi nje ya muda ni gharama ambayo wengi tunailipa hata sasa.Wakati wowote unaweza kuamua kutumia muda wako vizuri haijalishi uko wapi na unafanya nini,  nguvu ya maamuzi iko kwako.

Amua kubadili matumizi yako ya muda ili kuleta maendeleo yako binafsi na ya wale wanaokutazama.

Wote tunahitaji kuwa na nidhamu ya muda ili kupata matokeo mazuri. Heshimu muda uyafurahie matunda yake.


Neema Simbo ni mjasiriamali na mwandishi wa vitabu vya watoto na vijana. Amejikita katika kuwahamasisha vijana kuwekeza katika ndoto zao ili kupata matokeo mazuri. Unaweza kumpata kwa Instagram: @eden_kush_ au barua pepe: alphakush8@gmail.com  

Enable Notifications OK No thanks