Nidhamu: Tunu iliyobeba siri za mafanikio yako

April 3, 2021 7:02 am · Neema
Share
Tweet
Copy Link

                               


  • Nidhamu ni tunu iliyobeba hatma ya maisha yako.
  • Ukiitumia vizuri itakupa heshima na mafanikio unayotaka.

Huna nidhamu wewe! Huenda ni neno ambalo umewahi kuambiwa na watu wa karibu au unaofanya nao kazi. Labda ulijisikia vibaya kuambiwa hivyo kwa sababu umeshindwa kuwajibika katika kile unachofanya.

Huenda bado hujapata majibu kuhusu nidhamu ni nini? Nidhamu ni utaratibu au sheria anayojiwekea mtu au anayowekewa katika kufanya jambo au kutokufanya jambo fulani ili kutimiza malengo fulani.

Mara nyingi nidhamu humuongoza mtu au kumuwekea mipaka ya kufanya au kutofanya vitu fulani kwa kupenda au kutokupenda.

Mpaka hapo umefahamu kwa undani kuhusu nidhamu. Jiulize tena, una nidhamu kwa kila kitu unachofanya? Unaelewa madhara ya kutokuwa na nidhamu?

Nidhamu ni kiungo muhimu katika kuleta mabadiliko ya mtu binafsi na jamii. Nidhamu ni ulinzi wa safari ya mafanikio yako  na  ufunguo wa kukutambulisha  na kukuheshimisha kwa watu wanaokuzunguka.  

Unapokuwa na nidhamu  binafsi  na mwili wako na maisha yako, utazingatia una kula nini, una vaa nini, unafanya  nini na kwa nini. Utazungatia  unasema nini, unakunywa nini   na unautumiaje muda wako kufika kule unakotaka kufika.


Soma zaidi:


Nidhamu huleta matokeo chanya  unapoheshimu kazi yako au jambo unalofanya. Itakulinda, itakujengea imani na heshima mbele ya watu na kukufanya kuwa wa pekee zaidi.

Haijalishi uko wapi umeamua nini na una fedha kiasi gani kama hakuna nidhamu kutoka ni hadimu sana. Uaminifu umefungwa na unaenda sambamba na nidhamu.  

Kila kiwango kipya cha maisha kinahitaji kiwango kipya cha kujitoa. Uko tayari kuacha baadhi ya vitu na kutoka hapo ulipo ili ufike sehemu nzuri ya maisha? Ni nidhamu ndiyo itakutoa hapo.  

Mwenye kalamu ya maisha yako ni wewe mwenyewe  unachoamua kukiandika ndicho kitakachosomwa.

Nidhamu ni ulinzi, ni nauli, ni alama isiyofutika. Nidhamu ni taji isiyovulika na ni utambuisho wenye sifa ya aina yake ya kipekee.

Tafakari leo kama una nidhamu kwa kila unalofanya na amua kubadilika.  

Enable Notifications OK No thanks