Matengenezo barabara zilizoharibiwa na mvua yashika kasi

May 16, 2023 10:38 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Tarura yatenga fedha kuzikarabati ili kuwapatia unafuu wananchi. 

Mwanza. Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura), Wilaya ya Ilemela imetenga Sh67.4 milioni katika mwaka wa fedha 2023/24 kwa ajili ya matengenezo ya dharura ya barabara mbalimbali zilizoharibiwa na mvua.

Akizungumza kwenye Baraza la Madiwani kwa ajili ya utekelezaji wa bajeti ya robo ya tatu 2022/23, Meneja wa Tarura, Mhandisi Sobe Makonyo, amesema tayari bajeti hiyo imeshapitishwa na Bunge la Tanzania.

Meneja huyo pia amesema kupitia ofisi ya Mbunge, Tarura imepokea kiasi cha Sh15 milioni  kwa ajili ya kuchonga barabara mbalimbali zilizoathiriwa na mvua hasa zinazotumiwa na daladala kama vile Buswelu -Nyamadoke-Nyamh’ongolo, Kahama-Isela, Buswelu -Lukobe, Nyafla-Igumamoyo, Mihama-Zahanati na tayari utekelezaji wa kazi hizo unaendelea.

“Barabara ya Mbogamboga-Nyamadoke-Nyamh’ongolo ni miongoni mwa barabara zilizotengwa kwa ajili ya kuchongwa kwa kutumia fedha za ofisi ya Mbunge na tayari kazi hiyo imeshaanza kutekelezwa ili kuifanya ipitike baada ya kuharibiwa na mvua nyingi zilizonyesha,” amesema Mhandisi Sobe.

Katika bajeti hiyo pia wataweka alama za barabara na matuta pale inapobidi huku  barabara ya lami shughuli zitakazofanyika ni pamoja na  matengenezo ya barabara zinazofanyika kila mwaka kupitia bajeti za mwaka.

“Katika mwaka wa fedha 2023/24 kiasi cha Sh120 milioni zimetengwa kwa ajili ya matengenezo hayo ikiwemo na kuziba viraka,” amesema Mhandisi Sobe.


Soma zaidi:


Awali Diwani wa Viti Maalum Sara Manyama akiuliza maswali kwa Tarura alitaka ufafanuzi wa kufahamu kuwa ni lini wakala huo utatengeneza barabara ya Sunrise Kata ya Pasiansi ambayo kwa sasa imeharibika na kuwa kero kubwa kwa wananchi.

Pia alitaka kufahamu mpango wa kutengeneza barabara za mitaa katika halmashauri hiyo ambazo nyingi zimeharibiwa na mvua zilizonyesha kwa kiasi kikubwa.

Meya wa Manispaa ya Ilemela, Renatus Mulunga amesema Serikali imetoa zaidi ya Sh61.3 bilioni kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ndani ya manispaa hiyo.

Fedha hizo zitatumika kutekeleza miradi katika sekta ya afya, elimu na miundombinu mbalimbali.

Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Ilemela, Mhandisi Modest Apolinary amesema mpaka sasa manispaa yake imekusanya kiasi cha Sh12.1 bilioni sawa na asilimia 90 ya makisio ya bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/23.

Kati ya fedha hizo mapato halisi ni Sh11.9 bilioni sawa na asilimia 92 ya bajeti.

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

🔴LIVE: ULEGA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA UJENZI BUNGENI

Nukta TV

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

🔴LIVE: HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA ULINZI NA IKISOMWA BUNGENI

Nukta TV

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Fahamu kuhusu Virusi vya ‘Hantavirus’ na nini chanzo chake ?

Nukta TV