Matatizo ya mgongo yanavyowatesa madereva wa bodaboda
- Kukaa muda mrefu kwatajwa kama sababu.
- Watakiwa kuishughulisha miili yao na kupata tiba.
Mwanza. Aman Mashashiwa (38), mkazi wa Mtaa wa Nyegezi jijini Mwanza, alianza kuhisi maumivu ya mgongo tangu mwaka 2022 wakati akiendelea na kazi yake ya kusafirisha watu kwa kutumia pikipiki (bodaboda).
Mwanzoni alidhani kuwa ni maumivu ya kawaida lakini kadiri siku zilivyokuwa zinaenda hali ilizidi kubadilika kiasi cha kuathiri majukumu yake ya kila siku.
“Awali sikujua kama tatizo limekuwa kubwa hivi, niliendelea kutumia dawa za maumivu huku nikiendelea na kazi zangu lakini kadiri siku zinavyoenda ndio tatizo linazidi kuwa kubwa hali inayosababisha kushindwa kuendelea na shughuli zangu,” amesema Mashashiwa.
Siku moja aliamu kwenda katika Hospitali ya Kanda ya Rufaa ya Bugando jijini hapa. Baada ya vipimo aligundulika kuwa ana tatizo la mgongo.
Licha ya kuanza kupata matibabu, hawezi kufanya kazi ngumu za kujipatia kipato kama ilivyokuwa awali na anatakiwa kupata muda mrefu wa kupumzika.
Ni baba wa watoto watatu, kwa sasa amegeuka kuwa tegemezi.
Mashashiwa hana matumaini makubwa kuwa siku moja ataimarika na kurejea katika hali ya kawaida na kuendelea na kazi ya bodaboda ambayo ameifanya kwa miaka 20.
Tatizo la mgongo la baba huyo limetokana na kukaa muda mrefu kwenye pikipiki, jambo ambalo limedhoofisha utendaji wa mgongo wake.
Kwa sasa mkewe Martina Ferdinand ndiyo amebeba jukumu la kulea na kuhudumia familia.
Mashashiwa ni miongoni mwa madereva wengi wa bodaboda ambao wanakabiliwa na matatizo ya mgongo wakati wakitekeleza majukumu yao huku baadhi hawajui kiini cha tatizo hilo.
Baadhi ya wananchi wakisikilizwa na watoa huduma za afya kutoka hospitali ya Rufaa ya Bugando wakati walipojitokeza kwenye viwanja vya Nyegezi kwa ajili ya upimaji wa magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza ikiwemo mgongo. Picha | Mariam John.
Kwa nini maumivu ya mgongo?
Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba amesema chanzo cha maumivu ya mgongo ni uwiano usiofaa wa misuli ya mwili ambao husababishwa na aina za kazi zinazofanywa, ukaaji mbaya, ubebaji mbaya wa vitu au ulegevu.
Mgongo kitaalamu umegawanyika katika sehemu ya shingo (cervical), kifua (thoracic), kati na kiuno (lumbar) na mkia (sacral and coccygeal). Sehemu ya chini ambayo ni kiuno, pingili zake pamoja na diski huwa ni pana na hii ni kwa sababu zinabeba uzito mkubwa katika eneo hili.
Pia mgongo haujanyooka. Una mikunjo yake ambayo kibaiomekaniki sasa husaidia kusawazisha na kuleta uwiano wa mgandamizo kutoka kichwani hadi chini na ile kutoka chini kurudi juu (ground reaction forces)
Uwiano wa mgongo pia huathiriwa na kiuno na nyonga. Ukaaji mbaya eneo la nyonga hupelekea mabadiliko ambayo huelekea moja kwa moja hadi kwenye mgongo. Mtu akikaa vibaya kwenye nyonga basi mabadiliko huja mpaka kwenye mgongo.
Hali hiyo inaweza kusababisha maumivu ya mgongo.
Soma zaidi:
Akizungumza kwenye zoezi la upimaji wa magonjwa mbalimbali yasiyo ya kuambukiza, Afisa Mfiziotherapia kutoka hospitali ya Bugando, Samson Alponary amesema tatizo la mgongoni kubwa kwenye jamii.
Dk Alponary anakiri kuwa hospitali hiyo kupitia kitenge hicho cha fiziotherapia kwa siku hupokea wagonjwa 100 wa matatizo mbalimbali ya mgongo huku idadi kubwa ikiwa ni wanawake.
“Tafiti zinaonyesha kuwa mtu akikaa kwa muda mrefu zaidi ya saa moja inaweza ikasababisha maumivu ya mgongo huku wale wanaokaa kwa muda huo huku wakiendelea kula vyakula vyenye mafuta mengi, sukari nyingi nao husababisha kupata shinikizo la damu na kisukari,” amesema Dk Alponary.
Afisa huyo amesema wameamua kuwalenga waendesha bajaji, bodaboda na waendesha magari makubwa kwa kuwa wapo hatarini kupata ugonjwa huo kutokana na asili ya kazi yao lakini pia kiasili wao ndio wamelengwa na ajali za mara kwa mara.
“Unapougua ugonjwa huo, kwanza utendaji kazi unapungua lakini pia unashindwa kuzalisha hivyo kubaki kuwa tegemezi lakini kupararaizi,” amesema Dk Alponary.
Amewashauri watu kupima afya mara kwa mara na kutambua viashiria vyovyote vya maumivu ya mgonjwa ili wapate tiba mapema.
“Kitakwimu wanawake ndio wengi wanaobainika kukumbwa na tatizo hilo hiyo ni kutokana na asili ya mwanamke ameumbwa kuwa na kazi nyingi za kuinama, lakini kwa upande wa wanaume ni wachache kwa kuwa hawana tabia ya kwenda hospitali kupima,” amesema Dk Alionary.
Awali baadhi ya wananchi waliojitokeza kupima ugonjwa huo wamepongeza jitihada za hospitali ya Bugando kuwapelekea huduma hiyo mtaani kwa kuwa imepunguza muda na foleni.
“Hii kwetu ni fursa na tunatakiwa kuitumia vizuri ili kujua afya zetu,” amesema Gilbert Mloso.