Maoni mchanganyiko Latra ikitangaza njia mpya za daladala Dar
- Wapo waliofurahishwa na ujio wa njia mpya kwani utawasaidia kuwahi maeneo yao ya kazi.
- Wengine wasema njia hizo zitapunguza tabia ya baadhi ya wamiliki kujaza abiria kupita kiasi.
Dar es Salaam. Ikiwa imepita siku moja tangu Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra) itangaze njia mpya za daladala katika jiji la Dar es Salaam, baadhi ya wakazi wa jiji hilo wametoa maoni tofauti ikiwemo kufurahishwa na ujio wa njia hizo.
Latra ilitangaza ujio wa njia hizo 10 za mabasi ya daladala (jana) Januari 4, 2024 kupitia taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano cha mamlaka hiyo na kuwakaribisha wasafirishaji kuomba leseni.
“Mamlaka ya Usafiri Ardhini inawakaribisha wasafirishaji kuomba leseni kwenye njia mpya za daladala jijini Dar es Salaam, ili kufikisha huduma karibu na wananchi…,” imesema taarifa iliyotolewa na mamlaka hiyo.
Soma zaidi:Jela miaka 100 kwa kukutwa na meno ya tembo, Mwanza
Njia hizo 10 zilizotangazwa zote zinaanzia katika kituo kipya cha mabasi Mwenge kuelekea maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam ikiwemo Tabata Kimanga, Tabata Segerea, Mbande Kisewe, Sigara Sokoni, Buza, Kigogo Sokoni,Madale, Stesheni na Mnazi Mmoja.
Ili wamiliki wa vyombo vya usafirishaji waweze kusajiliwa katika njia hizo mpya Latra imeweka vigezo vitatu ikiwemo uvaaji wa sare ya suruali nyeusi na shati la mikono mifupi la bluu bahari.
Vigezo vingine vya kuzingatia wakati wa kuomba leseni ni kuhakikisha gari lina usajili kuanzia namba DXA kwa njia ya kuanzia na kuishia stendi mpya ya Mwenge pamoja na wamiliki wa magari mapya ambayo hayasajiliwa katika mfumo wa utoaji wa leseni wa PRIMS kuthibitishwa na Latra.
Wananchi watoa maoni mchanganyiko
Vaileth Amen, Makazi wa Tabata Segerea jijini hapa ameiambia Nukta Habari kuwa kuanzishwa kwa njia hizo mpya kutapunguza changamoto ya usafiri na tabia ya baadhi ya wamiliki kujaza abiria kupita kiasi.
Amesema kwa sasa ili afike Mwenge kwa ajili ya shughuli mbalimbali ikiwemo kuhudhuria ibada analazimika kupanda daladala zinazofaya safari kati ya Tabata na Kawe ambazo zinajaza sana na kusababisha abiria wengine kusimama.
“Hiyo ruti inaweza kusaidia…magari ya Kawe huwa yanajaa sana tukifika pale Tabata relini kuna watu wengine kuwa wanapanda kwa sababu huko kwao hakuna hayo magari…sisi tunaoshuka njiani ndio tunaoteseka,” amesema Vaileth.
Naye Juma Mkwizu, Mkazi wa Buza na mfanyabiashara katika soko la Mwenge amefurahishwa na ujio wa safari hizo kwani kutamrahisishia kufika eneo lake la biashara kwa haraka.
“Nimefurahishwa na ujio wa ruti (njia) hii…kawaida kama nina haraka ya kuwahi kazini basi ni lazima nipande magari mawili, la kwanza kutoka Buza mpaka Manzese kisha nichukue lingine la kunifikisha Mwenge au nipande yale ya moja kwa moja ya Buza mpaka Makumbusho,” anasema Mkwizu.
Latest