Mambo yanayochangia penati, riba kwa walipa kodi
- Kukosa kukadiria kodi ndani ya mipaka inayoruhusiwa.
- Kuchelewa kuwasilisha ritani za kodi kwa kipindi husika.
- Kutoa taarifa za uongo kuhusu kodi.
Huenda wewe ni mfanyabiashara na umekuwa ukilipa kodi katika shughuli zako za kawaida, lakini bado hufahamu kwa undani namna Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inavyofanya kazi.
Kutokana na uelewa mdogo, umejikuta ukipigwa penati au kulipa faini mara kwa mara. Ndiyo ni kwa sababu haufahamu makosa unayofanya katika biashara yako hasa unapotakiwa kuwek p a sawa suala la kodi.
Kushindwa au kukosa kufuata masharti mbalimbali na sheria za kodi za mamlaka hiyo kunaweza kukusababisha kupewa adhabu na riba.
Makala haya yatakufungua macho kuhusu riba na adhabu zinavyosimamiwa na TRA. Huu ni mwendelezo wa makala zilizopita zilizoangazia mfumo mpya wa kidijitali wa kodi Tanzania na undani wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT).
Tuanze safari yetu na riba zinazotozwa na TRA.
1. Riba ya makadirio ya chini (Interest for underestimating tax payable)
Walipaji malipo ya awamu wanaokadiria kodi ya mapato inayolipwa kwa mwaka wa mapato (Statement of Estimate of Tax Payable by Instalments on Behalf of Entity) wanatarajiwa kuonyesha kiwango cha juu cha usahihi wa makadirio.
Kukosa kukadiria kodi ndani ya mipaka inayoruhusiwa husababisha ukadiriaji wa chini, ambao utavutia riba.
Hii inatumika pale makadirio ya mlipaji wa awamu au makadirio yaliyosahihishwa ya kodi ya mapato inayolipwa kwa mwaka wa mapato chini ya kifungu cha 88 cha Sheria ya Kodi ya Mapato ni chini ya asilimia 80 ya kiasi sahihi.
Riba ambayo mlipaji wa awamu atalipa kwa kila kipindi itakokotolewa kwa kiwango cha kisheria na kuunganishwa kila mwezi, ikitumika kwa ziada ya:
- Jumla ya kiasi cha mapato ambacho kingelipwa kwa awamu katika mwaka wa mapato hadi mwanzo wa kipindi kama makadirio ya mtu au makisio yaliyorekebishwa yangelingana na kiasi sahihi.
- Kiasi cha ushuru wa mapato unaolipwa kwa awamu katika mwaka wa mapato hadi mwanzo wa kipindi.
Kumbuka: Mlipaji wa awamu atawajibika kwa riba kila mwezi au sehemu ya mwezi kuanzia tarehe ambayo awamu ya kwanza ya mwaka wa mapato inalipwa hadi tarehe ya kukamilisha ambayo mtu atawasilisha marejesho ya mapato kwa mwaka wa mapato chini ya kifungu 91(1) cha Sheria ya Kodi ya Mapato.
2. Riba ya kushindwa kulipa kodi
Iwapo kiasi chochote cha kodi kilichowekwa chini ya sheria yoyote ya kodi kitasalia bila kulipwa baada ya tarehe husika za kukamilisha inavyotakiwa na sheria au kanuni husika ya kodi, itasababisha kua na riba.
Riba itatozwa kwa kiwango cha kisheria kwa kiasi cha kodi iliyosalia kwa wakati fulani.
Iwapo, wakala wa zuio (VAT registered taxpayer) atashindwa kulipa kodi ya zuio inayodaiwa, atatakiwa kulipa riba kutokana na kodi ya zuio atakapowasilisha
Riba inayolipwa chini ya kifungu hiki au chini ya sheria nyingine yoyote ya kodi haitaathiriwa au kuondolewa kwa sababu ya kucheleweshwa kwa sababu ya taratibu za mahakama au mchakato mwingine wowote wa utatuzi wa migogoro.
Soma zaidi:
Penati unazoweza kupigwa
1. Kushindwa kutunza nyaraka
Kushindwa kuhifadhi nyaraka zitakazotumika au kuhitajika wakati wa kulipa kodi kila mwezi au ndani ya mwezi husika zitasababisha kupata adhabu.
Ikiwa ni mtu binafsi, pointi 5 za sarafu, na kwa shirika kubwa ni pointi 15 za sarafu. Kiwango cha kodi husika kitatakiwa kutajwa na kamishna wa kodi kwa mengine zaidi.
2. Penati ya kushindwa kuwasilisha ritani za kodi
Kukosa kuwasilisha ritani au kulipa kodi baada ya muda uliowekwa kwa kila mwezi au baada tarehe husika kutakufanya kupata adhabu ya juu zaidi kati ya yazifuatazo:
- Asilimia 2.5 ya kiasi cha kodi iliyokadiriwa kuhusiana na ritani ya kodi kutoka kodi ilivyoanza kulipwa ,mwanzoni mwa kipindi husika au
- Ikiwa ni mtu binafsi, pointi 5 za sarafu, na kwa shirika kubwa ni pointi 15 za sarafu.
Kumbuka: Adhabu hutumika tofauti na kushindwa kuwasilisha makadirio ya ritani za kodi kwenye ritani ya mwisho.
3. Penati ya kuwasilisha taarifa za uongo
Adhabu ya kutoa taarifa za uwongo au za kupotosha zinaweza kusababisha TRA kupata kodi pungufu. Adhabu ni kama ifuatavyo:
- Pale ambapo taarifa na mtu binafsi au taasisi kwa nia ya kudanganya au kupotosha, adhabu itakuwa asilimia 50 ya kodi inayotakiwa kulipwa.
- Pale ambapo taarifa au upungufu umefanywa kwa kujua au kwa kutojali, adhabu itakuwa asilimia 100 ya kodi inayotakiwa kulipwa.
Adhabu itaongezwa kwa asilimia 10 iwapo makosa yatajirudia na itapunguzwa kwa asilimia 10 ikiwa utajitolea kutoa taarifa kabla ya kugunduliwa na afisa ushuru au ukaguzi wa kodi unaofuata.
Mtu atahesabika katoa taarifa ya uongo au ya kupotosha ikiwa atatoa taarifa kwa afisa wa ushuru ambayo ni ya uongo au ya kupotosha katika nyenzo fulani au anaacha kujumuisha katika taarifa iliyotolewa au jambo lolote au kitu ambacho bila hiyo taarifa hiyo, inapotosha katika nyenzo fulani.
4. Penati kwa watu wanaosaidia wengine kukwepa kodi
Hii ni adhabu inayo/itakayompata mtu/kampuni inayosaidia, kushawishi, kumshauri au kumshawishi mtu/kampuni nyingine kutenda kosa kukiuka masharti ya sheria. Baada ya kutiwa hatiani, mtu/kampuni itawajibika kwa adhabu ya asilimi 100 ya upungufu wa kodi.
Makosa mengine
Kukiuka masharti ya sheria za ushuru kunaweza kusababisha makosa. Hii inaweza kusababisha mtu kuwekwa hatiani kwa taratibu husika za kurejesha kodi kwa makosa mbalimbali zilizotolewa na Sheria ya Usimamizi wa Ushuru, 2015 (Tax Administration Act).
Doreen Audax ni Mtaalamu wa masuala ya fedha, kodi, uhasibu na biashara nchini Tanzania aliyejikita kutoa ushauri wa kitaalamu kusaidia maswala yotr ya fedha, kodi, uhasibu, na biashara kiujumla. Wasiliana naye kupitia dorineaudax@gmail.com au Instagram @dorineaudax.