Ufahamu mfumo mpya wa kodi Tanzania
- Ni mfumo wa kidijitali uliozinduliwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni ili kuongeza ufanisi.
- Unamuwezesha mlipa kodi kukamilisha taratibu zote za kikodi katika eneo moja.
Dar es Salaam. Kama wewe ni mfabiashara au mfanyakazi, suala la kulipa kodi siyo geni kwako.
Hata hivyo, mchakato wa ulipaji kodi wakati mwingine umekuwa ukiibua changamoto kwa walipaji kutokana na ufanisi usioridhisha wa mifumo ya kidijitali ya kodi.
Kwa sasa huenda changamoto hizo zikapungua baada ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusasisha au kuboresha mfumo wa ulipaji kodi wa kidijitali na kuutambulisha rasmi mwanzoni mwa Februari 2023.
Mfumo huo umeunganisha huduma zote za kikodi kwenye jukwaa moja (TRA Online Service) ambao unamuwezesha mlipa kodi kukamilisha mambo yote kwenye jukwaa hilo, moja ya hatua kubwa katika kuongeza ufanisi wa ulipaji kodi nchini.
Awali mfumo wa kidijitali wa zamani wa kodi ulikuwa unamlazimu mlipa kodi awali na ujuzi wa msingi wa programu ya kompyuta ya Microsoft Excel na kuwa na nakala nyingi za programu hiyo ili kutumia mfumo wa kuwasilisha ritani.
Faida za mfumo huu mpya
Mfumo huu mpya unamuwezesha mlipa kodi kupata huduma zote kwenye mfumo mmoja kama zilivyoainishwa hapa:
- Maombi ya Namba ya Mlipa kodi (TIN) kwa Watanzania na raia wa kigeni.
- Kuwasilisha ritani za kodi kama kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na kodi ya kampuni na mshahara.
- Usajili wa malipo ya TRA na kutengeneza namba za malipo kupitia ‘control’ namba
- Mfumo wa Kufuatilia Mizigo (ECTS)
- Uhakiki wa risiti za malipo ya kielektroniki (EFD)
- Usajili wa leseni ya udereva
- Usajili wa magari
Mfumo huo umefanyiwa mabadiliko kadhaa ili kurahisisha utoaji wa huduma na kumpunguzia usumbufu mlipa kodi.
1. Kodi ya ongezeko la thamani
Uwasilishaji wa VAT umeboreshwa zaidi na unapatikana kwenye mfumo huo mpya ambao unakuepusha na usumbufu uliokuwepo hapo awali. Mlipa kodi alitakiwa kuwasilisha kwenye mfumo wa ‘E-filing system’ kisha kufanya usajili wa malipo kwenye mfumo mwingine. Sasa atafanya kwenye mfumo mmoja.
2. Ritani za kodi za kila mwaka (Annual Tax Returns)
Uwasilishaji wa ritani za kodi za kila mwaka huwasilishwa kwa kipindi tofauti tofauti kutegemeana na mwaka wa kibiashara. Biashara nyingi zinakua na kipindi cha Januari hadi Disemba.
Hivyo uwasilishaji wa ritani zake hufanyika tarehe ya mwisho ya mwezi Juni ya mwaka unaofuata.
Kwa kipindi cha miaka mitatu iliyopita, ritani za kodi zilikua zinawasilishwa kwenye ofisi za mikoa za TRA lakini baada ya kuanzisha kwa mfumo wa kodi wa awali zilikuwa zinakusanywa mtandaoni.
Hata baada ya ujio wa mfumo mpya, ritani hizi pia zinawasilishwa mtandaoni lakini kwa urahisi zaidi kwa sababu umeunganishwa moja kwa moja mfumo wa malipo pamoja na Kodi ya Zuio (Withholding Tax). Katika mfumo uliopita, mlipa kodi alikuwa akiwasilisha vyeti vya kodi hiyo ya zuio maarufu kwa kimombo kama Withholding tax certificates katika mkoa husika wa kikodi wa TRA.
Zinazohusiana:
- Ripoti: Watanzania 9 kati ya 10 wanatumia miguu kama nyenzo ya usafiri
- Mfumuko wa bei za vyakula Tanzania watarajiwa kushuka Machi 2023
- Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD
3. Usajili wa malipo ya kodi (Payment registration)
Huu ni mfumo unaomwezesha mlipa kodi kutengeneza fomu (Order Form) ambayo ili kufanya malipo ya kikodi. Kwa awali, mfumo huu ulikua unajitegemea wenyewe hivyo kumlazimu mlipa kodi kutumia mifumo tofauti tofauti mpaka kufikia kukamilisha zoezi.
Kwa sasa mfumo huu upo pamoja na mfumo mpya, hivyo haitomlazimu mlipa kodi kuingia kwenye mfumo mwingine ili kuweza kutengeneza fomu hii.
4. Kodi ya zuio (Withholding Tax)
Mfumo huu mpya umeunganishwa kumuwezesha mlipa kodi kuwasilisha kodi ya zuio na kisha kufanya usajili wa malipo. Hapo awali mfumo huu ulikua unapatikana kwenye mfumo wa ‘Payment Gateway.’
5. Kodi ya mshahara (PAYE) na Kodi ya Kuendeleza Ufundi Stadi (SDL returns)
Kodi hizi zinawasilishwa na mwajiri kila mwezi. Awali mlipa kodi alikuwa akitumia mfumo wa E-filing kisha kufanya usajili wa malipo kwenye mfumo mwingine.
Kwa mfumo huu mpya unamwezesha mlipa kodi kukamilisha kodi zote mbili katika kuwasilisha ritani na kutengeneza namba ya malipo ya kodi katika eneo moja.
6. Huduma nyingine zinazopatikana kwenye mfumo mpya
- Malipo ya kodi za biashara kwa awamu
- Usajili wa leseni ya udereva
- Kufungua Namba ya Mlipa Kodi (TIN)
- Uhakiki na ufuatiliaji wa risiti za EFD
- Usajili wa Magari
- Kujua kodi zilizolipwa na ambazo bado
- Usajili wa malipo yote (Assessed na Non-Assessed tax)
- Kuchagua wawakilishi wa mlipa kodi
- Kuingiza taarifa za kibenki
- Kuufikia mfumo wa zamani wa E-filing
Tukutane wiki ijayo katika uchambuzi wa mfumo huu mpya wa kodi Tanzania ili kukuongezea ufanisi wewe mlipa kodi.
Doreen Audax ni Mtaalamu wa masuala ya fedha, kodi, uhasibu na biashara nchini Tanzania aliyejikita kutoa ushauri wa kitaalamu kusaidia masuala yote ya fedha, kodi, uhasibu na biashara. Wasiliana naye kupitia dorineaudax@gmail.com au Instagram @dorineaudax.