Fahamu undani wa kodi ya ongezeko la thamani (VAT)

March 18, 2023 6:49 am · Dorine
Share
Tweet
Copy Link
  • Huu ni ushuru wa bidhaa, huduma na mali isiyohamishika.

Huu ni mwendelezo wa makala iliyopita iliyoangazia mfumo mpya wa kidijitali wa kodi Tanzania. Katika makala hii nitagusia masuala ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kwa undani zaidi.

Ijue Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT)

Huenda umesikia mara nyingi kuhusu VAT.  VAT ni kifupi cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kwa kimombo. 

Huu ni ushuru wa matumizi unaotozwa kwa bidhaa zinazoweza kutozwa ushuru, huduma, mali isiyohamishika ya shughuli yoyote ya kiuchumi wakati wowote thamani inapoongezwa katika kila hatua ya uzalishaji na katika hatua ya mwisho ya mauzo. 

VAT inatozwa kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini na zile kwa zinazoagizwa kutoka nje ya nchi. VAT inatozwa na watu waliosajiliwa kutoza VAT pekee.

 

Uwasilishaji wa rejesho la VAT (VAT return) ni nini?

Uwasilishaji wa rejesho la VAT ama kwa kimombo ‘VAT return’ ni utaratibu uliowekwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ajili ya kuwasilisha kodi ya ongezeko la thamani. 

Wafanyabiashara na walipa kodi wengine wote wanatakiwa kufanya marejesho kwa TRA mtandaoni kupitia mfumo wa kieletroniki wa Taxpayer Portal (TRA Online services).

VAT inalipwa siku ya 20 ya mwezi unaofuata wa biashara ambayo ni tarehe ya kuwasilisha marejesho. Iwapo siku ya 20 itakuwa Jumamosi, Jumapili, au siku ya mapumziko rejesho litakuwa la kulala katika siku ya kwanza ya kazi baada ya siku hizo. 

VAT ni chanzo muhimu cha kodi kwa Serikali. Picha | The Guardian.

Je, upeo wa VAT ni upi?

Kodi ya Ongezeko la Thamani inatozwa kwa usambazaji wowote wa bidhaa, huduma na mali zisizohamishika za shughuli zozote za kiuchumi Tanzania Bara ambapo ni malipo yanayotozwa kodi yanayotolewa na mtu anayetozwa kodi wakati wa shughuli za kiuchumi anazozibeba. 

Uagizaji wa bidhaa zinazotozwa ushuru kutoka sehemu yoyote nje ya Tanzania Bara utatozwa VAT na sheria na taratibu za kawaida za Forodha zitatumika. Ugavi wote unaotumiwa au kufurahia nje ya Tanzania Bara utakadiriwa sifuri baada ya uthibitisho. VAT inatozwa kwa bidhaa na huduma zinazotozwa ushuru. Viwango hivyo ni asilimia 18, asilimia 15 na asilimia 0.

  • 18%-VAT inatozwa kwa bidhaa na huduma zote zinazotozwa ushuru  zinazotolewa au kuingizwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Tanzania Bara.
  • 15%-VAT inatozwa kwa bidhaa na huduma zote zinazotozwa ushuru  zinazotolewa au kuingizwa ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa Tanzania Zanzibar.
  • 0%- Kwa mauzo ya bidhaa na huduma zinazotoka nje ya nchi.


Najisajili vipi kwenye huduma ya VAT?

Usajili wa VAT ni wa lazima kwa kila mtu anapofikia kiwango cha usajili cha Sh100 milioni katika kipindi cha miezi na zaidi au Sh50 milioni katika kipindi cha miezi sita inayoishia mwishoni mwa miezi iliyopita. 

Sharti hili linatumika kwa aina zote za usajili isipokuwa watoa huduma za kitaalamu, taasisi au taasisi ya Serikali inayojishughulisha na shughuli za kiuchumi na wafanyabiashara wanaokusudia kufanya biashara baada ya kutimizwa kwa ushahidi wa kutosha kama vile mikataba, zabuni, mipango ya majengo, mipango ya biashara na ufadhili wa benki.

Mtu anayetaka kusajiliwa atapeleka maombi kwa Kamishna Mkuu wa TRA ndani ya siku 30 lakini mfanyabiashara anayetaka kufanya biashara anaweza kutuma maombi hayo wakati wowote.

Endapo Kamishna Mkuu ataridhika kwamba mtu anatakiwa kusajiliwa kwenye VAT na kuna sababu za msingi ikiwa ni pamoja na kulinda mapato ya Serikali lakini hajaiomba, atasajiliwa na kumtaarifu mtu huyo si zaidi ya siku 14 baada ya siku ambayo usajili unafanywa bila kujali mauzo.


Soma zaidi:



Cheti cha Usajili wa VAT

Baada ya kujiandikisha, mlipakodi atapewa cheti cha usajili kitakachoeleza jina na eneo kuu la biashara la mtu anayetozwa ushuru, tarehe ambayo usajili unaanza, namba yake ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN) na namba yake ya usajili wa VAT.

Mtu ataonyesha namba yake ya utambulisho ya mlipakodi na namba yake ya usajili wa VAT katika marejesho yoyote, notisi ya rufaa au hati nyinginezo zinazotumiwa kwa madhumuni rasmi ya VAT na kuonyesha cheti chake cha usajili katika nafasi inayoonekana kwenye eneo lake kuu la biashara. 

Hii ina maana cheti hicho kiwekwe ukutani maeneo kama ya mapokezi au mbele ya duka kwenye kaunta panapoonekana wazi.

 

Uwasilishaji wa ritani za VAT

Huu ni utaratibu wa kuwasilisha ritani za VAT kupitia mfumo mpya wa TRA. Kila mfanyabiashara ambaye amesajiliwa na VAT anatakiwa kuwasilisha kodi ya ongezeko la thamani kama ilivyozungumziwa pale juu.

Utaratibu umewekwa na TRA kwenye uwasilishaji wa VAT kwa njia ya Kielekroniki.

 Ili kuweza kuwasilisha ritani izo, mlipakodi (Mtu binafsi na Shirika)  aliesajiliwa na VAT kupitia yeye mwenyewe, au mwakilishi aliyemchagua anatakiwa kuwasilisha ritani ya kila mwezi kwa wakati husika kwenye mfumo huo. 

Mfumo huo unaoitwa Taxpaye Portal unaotoa huduma za TRA mtandaoni utamwezesha mwakilishi aliechaguliwa na mlipakodi kuwasilisha ritani izo kila mwezi kwa kufuatia maelekezo yaliyoko kuweza kukamilisha uwasilishaji huo.

Ikumbukwe kuwa kila mwasilishaji wa ritani anatakiwa awe ana TIN number (Namba ya mlipa kodi wa kawadia) ili kuweza kupata huduma hizo kwenye mfumo.

 

Manufaa ya kuwasilisha ritani za VAT mtandaoni kwa wakati

Mfumo wa urejeshaji  ritani ni muhimu kuweza kurejesha kwa wakati uliowekwa na mamlaka iyo ili kuweza kuepuka kupata faida zifuatazo:

1.  Walipakodi watawasiliana na TRA wakiwa kwenye nyumba zao au ofisini wakati wowote.

2.  Kuepuka penati na riba zilizowekwa na mamlaka.

3.  Walipakodi wanaweza kuhifadhi rekodi zao kwenye mfumo huo na kuweza kuupitia wakati wowote sehemu yoyote watakapohitaji.

Usikose kusoma makala inayofuata ambayo itaangazia penati na riba ambazo zinatozwa na TRA.

Doreen Audax ni Mtaalamu wa masuala ya fedha, kodi, uhasibu na biashara nchini Tanzania aliyejikita kutoa ushauri wa kitaalam kusaidia masuala yote ya fedha, kodi, uhasibu, na biashara kiujumla. Wasiliana naye kupitia dorineaudax@gmail.com  au Instagram @dorineaudax. 

Enable Notifications OK No thanks