Maelfu waaga miili ajali ya ghorofa Kariakoo
- Familia zaendelea kugubikwa na huzuni pamoja na majonzi ya kuwapoteza wapendwa wao.
- Baadhi bado hawajui mahali walipo ndugu zao.
Dar es Salaam. Maelfu ya watu wakiwemo viongozi wa Serikali na dini wamejitokeza kuaga miili ya watu 15 waliofariki dunia katika ajali ya kuporomoka kwa ghorofa eneo la Kariakoo jijini Dar es Salaam.
Watu 16 walifariki dunia baada ya kufukiwa na kifusi cha jengo hilo lililoporomoka mapema Novemba 16 huku wengine 86 wakiokolewa katika ajali hiyo iliyobua mjadala wa usalama wa majengo jijini Dar es Salaam.
Kati ya watu hao waliofariki dunia, miili 15 ikiwa kwenye majeneza iliwasili Saa saba mchana katika viwanja vya Mnazi Mmoja kwa ajili ya kuagwa rasmi na wapendwa wao.
Mwandishi wa Nukta Habari ameshuhudia makundi mbalimbali ya waombolezaji ikiwemo ndugu, jamaa na marafiki wa karibu wakijitokeza kuwaaga ndugu zao licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha mahali hapo.
Maaskari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) wakiwa wamebeba majeneza yenye miili ya marehemu kuiingiza uwanjani kwa ajili ya kuagwa. Picha /Fatuma Hussein/Nukta.
Katika tukio hilo lililoongozwa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, mmoja wa waombolezaji katika eneo hilo aliyejitambulisha kwa jina moja la Jacky, amesema ameenda kutoa heshim za mwisho kwa waliopoteza maisha licha ya kuwa yeye bado hajafanikiwa kuwapata ndugu zake waliofukiwa na kifusi katika jengo hilo.
“Mimi nina watu wangu wawili walitoka tangu siku tukio limetokea, hatuna mawasiliano nao, siku ile tulikuwa tunawapata kwenye simu wanalalamika lakini jana simu zao zikawa hazipatikani japo tuna tumaini wanaweza wakawa salama,” amesema Jacky.
Licha ya sintofahamu, amesema familia yao bado inaendelea na jitihada za kuwatafuta ndugu hao japo ameona ni vyema kujumuika na waombolezaji wengine kutoa heshima za mwisho.
“Hatujui wako wapi lakini tunaomba kwa Mwenyezi Mungu atatufanyia wepesi, na Mwenyezi Mungu atawafanyia wepesi wote waliopo kule chini watatoka salama na tutakuwanao tena,” ameeleza Jacky wakati akitokwa na machozi.
Tukio hilo lililoandaliwa na Serikali liliambatana na vilio pamoja na na simanzi huku ndugu, jamaa na marafiki wakianguka kwa kupoteza fahamu kutokana na machungu ya kuwapoteza wapendwa wao.
Viongozi mbalimbali walizungumza kuwatia moyo wafiwa hasa katika kipindi hiki kigumu wanachokipitia.
Majaliwa amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia ambaye kwa sasa yuko nchini Brazil, akiwataka wananchi, pamoja na wafiwa kuwa wavumilivu na Mungu awatie nguvu hasa katika kipindi hichi kigumu ambacho wamewapoteza wapendwa wao.
Pia majaliwa amewataka viongozi wa Serikali kushiriki kikamilifu katika shughuli zote za mazishi zitakazofuata kwa ajili ya mazishi ikiwa ni ndani au nje ya jiji la Dar es Salaam.