Mambo ya kuzingatia kabla, baada ya kupanda Mlima Kilimanjaro
- Ni pamoja kujiandaa kimwili, kiakili na kiuchumi.
- Inashauriwa kuchagua wakala sahihi anayeendana na bajeti yako.
- Baada ya kupanda mlima, unashauriwa kumpuzika na kula vyakula vya kuongeza nguvu.
Dar es salaam. “Siku hizi kupanda mlima Kilimanjaro imekuwa rahisi kuliko zamani, miaka ya nyuma kulikuwa na changamoto kidogo hivi sasa Serikali kwa kiasi fulani imefanyia kazi.”
Ni Harold Mndewa, Mtanzania anayefanya kazi ya kuongoza watalii kupanda mlima Kilimanjaro ambaye hivi karibuni amewashangaza wengi baada ya kuweka rekodi ya kuupanda Mlima Kilimanjaro mara 300.
Pamoja na urahisi huo anaoueleza Harold mtandao unaochapisha habari za utallii wa Traaasgpu unaeleza kuwa ni asilimia 65 tu ya watu ndiyo wanafanikiwa kufika kilele cha Mlima Kilimanjaro.
Huenda na wewe ni miongoni mwa watu wanaotamani sana kupanda mlima huo na kuingia katika orodha ya waliowahi kuupanda mlima huo mrefu zaidi barani Afrika lakini haufahamu namna gani unaweza kufanikisha hilo.
Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imefanya mahojiano na Harold pamoja na kufanya tafiti katika kampuni zinazojihusisha na kuongoiza watalii kuandaa makala haya ambayo yanaweza kukusaidia kutimiza ndoto ya kufika kwenye kilele cha Mawenzi kilicho umbali wa mita 5,895 kutoka usawa wa bahari.
Kupanda milima kuna faida nyingi ikiwemo kuimarisha afya ya mwili. Picha | Ian Taylor Trekking.
Maandalizi mazito
Ili kupanda Mliima Kilimanjaro kwa urahisi yakupasa kujiandaa kimwili, kiakili, pamoja na kifedha. Mazoezi ya mwili ni yale yatakayokusaidia kuwa na pumzi ya kutosha pamoja na kujenga misuli ya mwili.
Harold anabainisha kuwa watu wanaofanya kazi zisizohushisha matumizi ya nguvu mara nyingi hupata changamoto wakati wa kupanda hivyo inashauriwa kufanya mazoezi kabla ya kupanda mlima huo.
Sambamba na kuweka mwili sawa, unatakiwa pia kujiandaa kiuchumi kwani kupanda Mlima Kilimanjaro kunahitaji fedha ambapo gharama zinatofautiana kulingana na kampuni inayokuhudumia licha ya kuwa wazawa wana ahueni kuliko raia wa kigeni.
“Gharama zinatofautiana kulingana na siku unazotumia, huduma utazopata, njia unayotumia, utaifa pamoja na wakala unayemtumia. Kwa Mtanzania gharama inaweza kuanzia Sh1.2 milioni na kwa wageni inaweza kuanzia Dola za Marekani 1,800 sawa na Sh4.1 milioni zaTanzania,” anasema muongoza watalii huyo.
Gharama hiyo inahusisha kupata kibali cha kuingia na kutoka kwenye hifadhi, vyakula,malazi, wapagazi, muongoza njia, maji pamoja na huduma nyingine zinazoainishwa na wakala husika.
Soma zaidi:
- Ijue milima 10 mirefu zaidi Tanzania
-
Tanapa yaendelea kuchunguza chanzo cha moto Mlima Kilimanjaro
-
Siri Mtanzania kupanda mlima Kilimanjaro mara 300
‘Usisahau mavazi maalum’
Wakati wa kupanda Mlima kilimanjaro unaweza kukabiliana na hali zote za hewa kutegemeana na msimu wa kipindi hicho, ingawa haishauriwi kupanda mlima kipindi cha mvua.
Mavazi yanayotakiwa ni yale ya kuvaa kwenye baridi kali, wastani na hali ya kawaida pamoja na viatu vya kupandia mlima.
Baadhi ya vifaa kama fimbo za kupandia mlima hutolewa na mawakala ingawa hauzuiwi kununua za kwako.
Chagua wakala sahihi
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro hairuhusu upandaji binafsi hivyo ni lazima uwe na wakala ambaye anakuwa amesajiliwa na mamlaka husika kuifanya kazi hiyo.
Orodha ya mawakala inapatikana katika tovuti ya hifadhi pamoja na mitandao ya kijamii.
Unashauriwa kuzingatia bajeti yako pamoja na uhalali wa wakala kabla hujalipia kupata huduma hiyo kwani wakala unayemchagua ana mchango mkubwa katika kufanikisha au kutofanikisha safari yako.
Tangazo:
‘Na njia utakayopita ni muhimu’
Kwa mujibu wa tovuti ya kampuni ya kuongoza watalii ya Good deeds, kuna njia rasmi sita za kufika katika kilele cha Mlima Kilimanjaro na njia nane za kushuka ambapo kila njia ina gharama zake pamoja na ugumu au urahisi wa kufika kileleni.
Njia hizo ni pamoja na Machame, Marangu, Rongai, Lemosho, Umbwe, Shira, pamoja na Mweka. Njia ya Marangu ndiyo inatajwa kuwa njia fupi zaidi ambapo mtu anaweza kutumia siku tano hadi sita kupanda na kushuka hivyo inawafaa watu wenye bajeti ndogo.
Baada ya kupanda fanya haya
Mara baada ya kumaliza kazi ngumu ya kupanda mlima kwanza Inashauriwa kufurahia mafanikio hayo hata kama haukufika kileleni. Wataalamu wanashauri baada ya hapo kupata muda wa kupumzika.
Kwa mujibu wa tovuti ya utalii na safari ya Missadventure ya nchini Marekani baada ya kupanda mlima inashauriwa kupumzika kwa muda wa wiki moja bila kufanya kazi ngumu. Kunywa maji ya kutosha pamoja na vyakula vya kuupa mwili nguvu.