Mambo 10 ya kuzingatia unapoanzisha biashara mtandaoni
- Hakikisha unafahamu taratibu na miongozo ya mtandaoni.
- Jenga jina, uaminifu na kuwa karibu na wateja wako.
Matumizi ya mitandao ya kijamii siyo tu yamerahisisha mawasiliano ya watu bali yamefungua fursa kwa watu kujiingizia kipato ili kuboresha maisha.
Mitandao ya kijamii ni majukwaa muhimu ya kuwafikia watu kwa bidhaa na huduma mbalimbali. Kwa sasa, mtu ana nafasi kubwa ya kuendesha biashara yake mtandaoni bila hata kuwa na duka ambalo wateja watamfuata.
Hata hivyo, kabla hujafanya uamuzi wa kuendesha biashara yako mtandaoni, yapo mambo muhimu ya kuzingatia ili uwe na ufanikiwe:
1. Chagua jina la biashara
Jina la biashara ndio kila kitu katikashughuli zako. Hakikisha unakua na jina ambalo litakua rahisi kwa mteja kufikia biashara yako, na ambalo linaendana na biashara yako.
Hakikisha jina linakua fupi na rahisi kusomeka ili kuvuta wateja kirahisi kununua bidhaa. Jiulize jina nililochagua linahusiana na kitu nachouza? Je , hili jina nikitafuta linatafutika?, Je, hili jina ni rahisi mteja kulishika/kukumbuka?
2. Chagua mtandao unaokufaa
Mitandao ya kijamii ipo mingi. Chagua mmoja au zaidi ambayo utajikita huko kufanya biashara yako ya bidhaa au huduma. Kila mtandao una watumiaji ambao tabia zao hutofautiana.
Kabla ya kufungua biashara yako hakikisha unafanya utafiti wa kina kuhusu matumizi ya mitandao ya kijamii. Ukipata basi moja kwa anza kufanya biashara.
Ukitumia vizuri mtandao inaweza kuwa sehemu sahihi ya kuingiza kipato. Picha | Daniel Samson/Nukta.
3. Kumbuka uaminifu
Uaminifu ni jambo muhimu kwenye biashara. Unaweza kukuza au kuangusha biashara. Hakikisha kila ukitoa ahadi unaitimiza. Hakikisha bidhaa zako zinakidhi viwango vya ubora ili wateja waziamini.
4. Taarifa za biashara
Hakikisha unaweka taarifa muhimu zinazohusiana na biashara yako ili kumwezesha mteja kukutafuta kwa urahisi, ikiwa ni sehemu ya mauzo. Taarifa za mfanyabiashara kama namba za simu, ni aina gani ya biashara, bei, na taarifa nyingine muhimu zinazohusiana na biashara yako.
5. Usalama wa kaunti zako
Kutokana na ukuaji wa teknolojia, baadhi ya watu wamekuwa wakidukua akaunti za mitandao ya kijamii za wafanyabiashara na hata kuingili mifumo ya kifedha ili kufanya utapeli.
Ukiweka biashara mtandaoni hakikisha umeweka mifumo imara ya ulinzi ili kuifanya biashara kuwa salama wakati wote. Unaweza kuajiri wataalam wa kuzimamia akaunti zako na hata wakakushauri namna ya kuifanya iwe salama ili usipoteze wateja.
Soma zaidi
-
Ripoti: Watanzania 9 kati ya 10 wanatumia miguu kama nyenzo ya usafiri
-
Faida za kampuni ndogo kutunza kumbukumbu za kifedha
6. Fungua makundi sogozi
Kama unatumia WhatsApp au Facebook, unaweza kufungua makundi maalum kwa ajili ya kutangaza na kuuza bidhaa zako. Makundi haya yatakusaidia kuwafikia kwa urahisi wateja wako na kuwahudumia kulingana na mahitaji yao.
7. Kuwa karibu na wateja wako
Kama mitandao ya kijamii ni jukwaa la kuuzia bidhaa au huduma zako, hakikisha unakuwa “active”. Hii itakuwasaidia kujibu maswali au kutoa baadhi ya taarifa za bidha zako kwa wateja.
Pia itajenga uaminifu na kuwafanya wateja wajisikie huru kutoa maoni yao na kujiona ni sehemu ya biashara yako. Ni njia pia ya kujifunza mabadiliko ya tabia za manunuzi za wateja wako mtandaoni.
8. Toa suluhu
Hakikisha bidhaa au huduma unazotoa zinatatua changamoto za wateja wako kwa ukamilifu bila kuacha mashaka. Hili linawezekana tu kama bidhaa zako zina ubora na zimekidhi viwango vya kuwepo sokoni.
Fanya maboresho ya bidhaa zako kila inapohitajika ili kutowapoteza wateja wako.
9. Tumia mbinu nyingine kujitangaza
Licha ya kuwa unatumia mitandao ya kijamii kuuza bidhaa au huduma, usisahau kutumia mbinu nyingine kama watu maarufu mtandaoni kujitangaza zaidi na kuwavuta wateja kuja kwenye duka lako la mtandaoni.
10. Jifunze lugha nzuri ya biashara
Hakikisha unatumia lugha nzuri ya biashara ili kuweza kuwasiliana kabla na baada ya kuingia katika biashara.
Mathalan, unaweza kugundua kwamba mteja anataka kuchukua au kuhudumiwa bidhaa fulani lakini anaonekana hajatosheka, tumia lugha ya staha kumshawishi kuendelea kuhudumiwa na wewe. Hii inajenga kumbukumbu kwa mteja.
Hakuna biashara usiyokua na ushindani. Tafuta namna yako ya kuweza kuonyesha upekee kwenye biashara yako na kujitofautisha na watu wengine, ili kumpa mteja sababu ya kutumia bidhaa zako.
Doreen Audax ni Mtaalamu wa masuala ya fedha na uhasibu nchini Tanzania aliyejikita kutoa ushauri wa kitaalamu kusaidia ukuaji wa biashara ndogo ndogo na za kati (SMEs). Wasiliana naye kupitia dorineaudax@gmail.com au Instagram @dorineaudax.
Latest



