Matumaini makubwa wakulima kuongeza thamani ya mazao Tanzania
- Serikali, wadu kuongeza kasi ya kuwapatia mikopo.
- Kuwaongezea maarifa na teknolojia kuzalisha kisasa.
Mwanza. Serikali mkoani Mwanza imesema itahakikisha inawasaidia wajasiriamali wadogo wa kilimo, uvuvi na ufugaji ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwemo kutumia teknolojia ya kisasa.
Akizungumza Mei 6, 2022 kwenye mkutano uliozikutanisha sekta hizo ambao umeandaliwa na taasisi ya kuwezesha sekta binafsi ya kilimo (PASS TRUST), Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Mhandisi Robert Gabriel amesema wakulima wengi wadogo bado wanatumia teknolojia duni za kilimo.
Pia sekta ya uvuvi na ufugaji bado hawana zana muhimu zinazowasaidia kufuga au kuvua kisasa.
Amesema kupitia taasisi ya PASS, Serikali itaweza kuwafikia wadau wengi kwenye sekta hizo, kundi ambalo kwa muda mrefu limekua haliwezi kuzifikia taasisi za kifedha kwa ufanisi.
“Serikali mkoani Mwanza itashirikiana na PASS ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma hizo muhimu lakini niiombe iendelee kupanua wigo kujenga uelewa kwa kufanya mikutano katika ngazi mbalimbali ili kuwafikia wakulima wengi zaidi,” amesema Gabriel.
Awali akizungumza kwenye mkutano huo, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa PASS TRUST, Adam Kamanda amesema jumla ya wajasiriamali milioni 1.7 wamefaidika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh1.2 trilioni katika kipindi cha miaka 22 iliyopita.
Kwa kutambua unyeti wa sekta ya kilimo nchini, amesema mpaka kufikia mwaka jana jumla ya biashara 532,798 zinazojihusisha na mazao na huduma kwenye kilimo zimenufaika kupitia dhamana zao za huduma za maendeleo ya biashara katika mikoa yote nchini.
“Takwimu za hivi karibuni zinaonesha kuwa takribani asilimia 31 ya mikopo yote ya kilimo nchini imewezeshwa kwa udhamini wa PASS ambapo Kanda ya Ziwa ni moja ya kanda muhimu katika sekta ya kilimo,” amesema Kamanda.
Yanayokuhusu:
- Rasmi:Tabora ndiyo makao ‘makuu ya kuku wa kienyeji Tanzania’
- PASS kuwawezesha vijana sekta ya kilimobiashara
Takwimu za mwaka jana pekee zinabainisha kuwa jumla ya wakulima na wajasiriamali 37,717 ambao kati yao 12,277 ni wanawake walinufaika na huduma za PASS sawa na asilimia 25 ya mikopo.
Kutokana na maboresho yanayoendelea kufanywa na wadau mbalimbali zikiwemo benki, juhudi za Serikali na huduma ya kidijitali wanatarajia kuwafikia na kuwahudumia wakulima, wafugaji, wavuvi na wajasiriamali wengi zaidi katika mnyororo wa thamani.
Venance Barandaje ni mmoja wa wanufaika wa taasisi hiyo amesema awali changamoto ilikuwa ni upatikanaji wa mbegu bora lakini pia elimu kuhusu chakula bora kwa ajili ya malisho ya nguruwe.
“Wakati naanza ufugaji sehemu kubwa niliyokuwa natumia mshahara, mwaka 2018 nikaunganishwa na PASS TRUST ambayo imenisaidia kukua na kupanua mradi wangu baada ya kufahamu mahitaji ya chakula na kuzalisha wanyama kiasi gani,” amesema Barandaje.
Latest
