Majaliwa: Taasisi za Serikali nunueni bidhaa viwanda vya ndani

September 23, 2021 11:31 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Amesema hiyo itasaidia ukuaji wa viwanda na kinua uchumi.
  • Viwanda navyo vyatakiwa kutumia malighafi za Watanzania.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kwa sasa Serikali imeweka kipaumbele katika ununuzi wa bidhaa za viwanda vya ndani kwa ajili ya taasisi zake huku akivihimiza viwanda hivyo kutumia malighafi za Watanzania ili kuinua uchumi wa Tanzania.

Majaliwa amesema sekta ya viwanda ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi na kuondoa umaskini nchini pamoja na kuboresha maisha ya Watanzania.

Kutokana na umuhimu wa uchumi wa viwanda amesema Serikali itaendelea kununua bidhaa zinazotokana na viwanda vya ndani katika kutekeleza miradi mbalimbali ya kielelezo na kimkakati.

“Tumeshatoa maelekezo kwa taasisi zetu kununua sare zao za nguo na viatu, mabomba ya maji na gesi, mabati, nondo, saruji kutoka katika viwanda vya hapa nchini,” amesema Majaliwa leo Septemba 23, 2021 wakati wa akizindua upanuzi wa kiwanda cha bia cha Serengeti (SBL) tawi la Moshi mkoani Kilimanjaro. 

Aidha, ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuendelea kuhamasisha wizara na taasisi za umma na binafsi zinunue na kutumia bidhaa zinazozalishwa hapa nchini ili viwanda viendelee kuzalisha, kutoa ajira kwa vijana na pia Serikali itakusanya kodi na kuendelea kutoa huduma za jamii kwa wananchi.

“Duniani kote, sekta hii imekuwa chimbuko la maendeleo ya haraka ya nchi mbalimbali na ndiyo mhimili mkuu wa kutegemewa katika kuongeza thamani ya malighafi, kutoa ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali pamoja na fedha za kigeni, kuongeza na kuboresha teknolojia,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa na Mkewe Mary Majaliwa wakitazama mtambo wa kuzalisha pombe kali iitwayo Bongo Don wakati Waziri Mkuu alipofanya uzinduzi wa upanuzi wa Kiwanda cha Bia cha Serengeti (SBL) tawi la Moshi Septemba 23, 2021. Wa tatu Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai.

Amesema Serikali inaendelea kuhamasisha uwekezaji katika sekta za viwanda kwa kuboresha miundombinu muhimu na wezeshi kama reli ya uhuru, ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ili iweze kuchukua mizigo mizito na kuisafirisha kwa haraka kutoka sehemu moja hadi nyingine.

“Tumeongeza ufanisi wa utoaji mizigo bandarini sambamba na huduma za usafiri na usafirishaji kwa njia za anga, maji na barabara. Hatua nyingine ni uwekezaji mkubwa unaofanyika kwenye upatikanaji wa nishati ya gesi, umeme wa uhakika, unaotabirika na kutosha mijini na vijijini,” amesema.

Amesema ujenzi wa bwawa kubwa la kufua umeme wa maji la Mwalimu Nyerere, litakalozalisha umeme megawati 2,115 una lengo la kuhakikisha tatizo la nishati ya umeme linabaki kuwa historia kwa sababu uwepo wa bwawa hili, utasaidia siyo tu kuwa na umeme wa uhakika na ziada.

Ametoa wito kwa wawekezaji na wazalishaji kuchangia katika juhudi zinazofanywa na Serikali kuondoa changamoto zinazoathiri ukuaji wa sekta ya viwanda kwa kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa juu na kwa bei shindani ambayo hata mlaji wa kawaida atamudu kununua bidhaa hizo.

“Pamoja na kuwahimiza wazalishaji kuongeza ufanisi katika uzalishaji, pia ninapenda kuwasihi ndugu zangu Watanzania kupenda kutumia bidhaa zinazozalishwa nchini,” amesema Majaliwa.

Amesema kwa kufanya hivyo, Tanzania itaongeza wigo wa soko la bidhaa za viwanda na kuviwezesha kukua na kuajiri vijana wengi zaidi. 

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW