Majaliwa mgeni rasmi maombi ya kitaifa dhidi ya Corona
- Yatakayofanyika kesho katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
- Maombi hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Viongozi wa madhehebu ya Dini nchini.
Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa atakuwa mgeni rasmi katika maombi ya kitaifa ya kuombea nchi dhidi ya janga la Corona (#COVIDー19) yatakayofanyika kesho katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Maombi hayo yameandaliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na Viongozi wa madhehebu ya Dini nchini.
Wizara ya afya katika taarifa yake iliyotolewa leo imesema maombi hayo yatakayoongozwa na viongozi wakuu wa madhehebu ya dini nchini, yatafanyika kesho Aprili 22, 2020 katika Viwanja vya Karimjee.
“Hatua hii ni utekelezaji wa maazimio ya mkutano wa viongozi wa dini na Serikali uliofanyika tarehe 9 Aprili, 2020 Jijini Dar Es Salaam kuwa yafanyike maombi ya kitaifa yanayojumuisha madhehebu yote nchini kuomba dhidi maambukizi ya Corona,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Zinazohusiana
- Mikakati ya Tanzania kukabiliana na virusi vya Corona
- Picha, sauti ya uzushi virusi vya corona zinavyojipenyeza mtandaoni Tanzania
- Unayotakiwa kufahamu kuhusu virusi vya Corona
Aidha,maombi haya ni mwendelezo wa maombi ya siku tatu mfululizo yaliyotangazwa na Mhe. Rais John Magufuli kuanzia Aprili 17-19, 2020.
“Viongozi wachache watahudhuria maombi haya kuwakilisha wananchi ikiwa ni katika hali ya kuchukua tahadhari ya maambukizi hivyo, wananchi mnasisitizwa kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya Corona na kufuatilia maombi haya mkiwa katika maeneo yenu kupitia vyombo mbalimbali vya habari,” inaeleza taarifa hiyo.