Majaliwa atoa maagizo mazito upandaji bili za maji, ununuzi wa pamba Maswa

August 9, 2019 6:38 am · Mwandishi
Share
Tweet
Copy Link

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama pamba  wakati alipotembelea ghala la Chama cha  Ushirika cha Msingi cha Kumalija cha wilayani Maswa Agosti  8, 2019. Waziri Mkuu alikuwa katika ziara ya kukagua ununuzi wa pamba katika mkoa wa Simiyu. Picha|Ofisi ya Waziri Mkuu.


  • Amekerwa na kitendo cha mamlaka hiyo kupandisha bili za maji kutoka Sh5,000 hadi Sh28,000 jambo ambalo amesema halikubaliki.
  • Aagiza wakulima wa pamba kulipwa malipo yao kupitia benki kuanzia mwaka ujao.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu,  Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka kukutana na watendaji wa Mamlaka ya Maji wilayani Maswa ili kujadili na kutafuta suluhisho la kupanda kwa bili za maji kwa asilimia 82.1 kitendo ambacho hakikubaliki kwa wananchi wa wilaya hiyo. 

Majaliwa amekerwa na kitendo cha mamlaka hiyo kupandisha bili za maji kutoka Sh5,000 hadi Sh28,000 kwa sababu inamuumiza mwananchi wa kawaida.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana (Agosti 8, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Kumalija, wilayani Maswa mkoani humo mara baada ya kutembelea ghala la pamba la Chama cha Msingi cha Kumalija.

“Haiwezekani bili ikapanda kwa kiasi hicho. Hapo utakuwa unamsaidia mwananchi myonge au utakuwa unamnyonga. Bili haiwezi kupandishwa kwa asilimia kubwa kiasi hicho yaani imetoka Sh5,000 hadi Sh28,000,” amesema Majaliwa. 

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali inatekeleza kampeni  kumtua mama ndoo kichwani, inayolenga kuwaondolea wananchi tatizo la upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama, hivyo upandishaji huo wa bili hauna tija kwa wananchi wanyonge.


Zinazohusiana:


Katika hatua nyingine, Majaliwa ameagiza kuwa kuanzia mwaka ujao wa 2020 malipo yote ya wakulima wa pamba yawe yanapitia benki ambapo wakulima wataingiziwa fedha kupitia akaunti zao.

Amewataka wakulima wafungue akaunti katika benki mbalimbali zilizopo kwenye maeneo yao ili waweze  kufanikisha mkakati huo na pia kuhifadhi fedha zao kwa ajili ya matumizi ya baadaye.

“Ni vizuri malipo ya wakulima yapitie benki ili kuwawezesha kupanga matumizi mazuri ya fedha zao na pia watapa fursa ya elimu ya matumizi mazuri ya fedha,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW