Majaliwa aikalia kooni TPA

August 2, 2021 11:50 am · Mariam John
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza mabadiliko yaliyofanyika katika taasisi hiyo yanakuwa na tija.
  • Ataka ameiagiza meli za Mv Ruvuma na Mv Njombe kuanza kazi ya kutoa huduma mara moja.

Mwanza. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kufuatilia kwa karibu utendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA) ili kuhakikisha mabadiliko yaliyofanyika yanakuwa na tija.

Pia Waziri Mkuu ameiagiza TPA kuhakikisha meli za mizigo na abiria za Mv Ruvuma na Mv Njombe zianze kazi ya kutoa huduma mara moja.

Majaliwa  ametoa maagizo hayo  leo Agosti 2, 2021 wakati alipotembelea bandari ya Itungi wilayani Kyela mkoani Mbeya na  kukuta meli hizo zikiwa zimeegeshwa katika bandari hiyo iliyopo Ziwa Nyasa.

Amesema Serikali imetumia fedha nyingi katika ujenzi wa meli hizo kwa lengo la kutoa huduma za kusafirisha mizigo katika ukanda wa Ziwa Nyasa.

“TPA imefanya mabadiliko na tunataka kuona mabadiliko hayo yanakuwa na tija ikiwa ni pamoja na matumizi mazuri ya bandari zilizo kwenye ukanda wa Ziwa Nyasa na Tanganyika,” amesema Majaliwa.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikagua meli za  MV Mbeya II, MV Ruvuma na MV Njombe katika bandari ya Kyela mkoani Mbeya, Agosti 2, 2021. Picha| Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kiongozi huyo amesema meli hizo zikianza kufanya kazi hata kama zitakuwa zinabeba mizigo michache zinaweza kuanza na faida ndogo kuliko kuziegesha.

“Meli zimekaa hapo zimeshindwa  kwenda kubeba makaa ya mawe kwa kushindwa kukubaliana bei nyie mnataka shilingi ngapi na zinapokaa hapo mnapata kiasi gani?,” amehoji Majaliwa.

Pia, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi ifuatilie kwa karibu utendaji wa mamlaka hiyo pamoja na bandari zake ili kuhakikisha mabadiliko yaliyofanyika yanakuwa na tija.

Machi 28 mwaka huu, Rais Samia Suluhu Hassan aliagiza Mkurugenzi Mkuu wa TPA, Deusdedit Kakoko asimamishwe kazi mara moja ili kupisha uchunguzi wa ubadhirifu dhidi ya taasisi hiyo ikiwemo upotevu wa Sh3.6 bilioni. 

Baadaye Kakoko aliondolewa kazini na nafasi yake kwa sasa inashikiliwa na Erick Hamis ambaye awali alikuwa  Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya Huduma za Meli Nchini (MSCL), Erick Hamis.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW