Majaliwa asisitiza utunzaji chakula kukabiliana na mvua zisizotabirika Tanzania

September 6, 2024 5:02 pm · Davis Matambo
Share
Tweet
Copy Link
  • Ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotarajiwa kuathiri mvua.
  • Wakulima wahimizwa kulima mbegu zinazokomaa kwa muda mfupi na kustahimili ukame.
  • Serikali yaahidi kuendelea kutoa ruzuku ya pembejeo kuchochea uzalishaji.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania Kasim Majaliwa ametoa wito kwa wananchi kuchukua tahadhari za mapema za utunzaji wa chakula sambamba na kuendelea kutumia chakula kilichopo sasa kwa uangalifu kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa yanayotegemewa kuathiri upatikanaji wa mvua za vuli. 

Wito wa Majaliwa umetolewa siku chache baada ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) kutoa utabiri wa mvua za vuli kwa kipindi cha Oktoba hadi Desemba 2024 unaoonesha mvua hizo zitakuwa na mtawanyiko usioridhisha na vipindi vya ukame katika baadhi ya maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua, ikiwemo mikoa ya Kagera, Geita, Mwanza, Mara, Simiyu, na Kaskazini mwa Kigoma.

Mikoa mingine ni Manyara, Arusha, Kilimanjaro, Tanga, Pwani, Dar es Salaam na Kaskazini mwa mkoa wa Morogoro. 

Majaliwa aliyekuwa akizungumza katika hotuba ya kufunga mkutano wa 16 wa Bunge la 12, leo Septemba 6, 2024 bungeni jijini Dodoma amesema kutokana na mwenendo wa mabadiliko ya hali ya hewa katika nchi yetu ni vyema tukachukua tahadhari mapema ikiwemo kuzalisha mazao yanayokomaa kwa muda mfupi.

“Hivyo basi nitumie fursa hii kuwahimiza wananchi kupanda aina ya mazao mbalimbali yanayokomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame. Kwa upande mwingine maafisa ugani wawaelimishe wananchi wetu kuhusu mazao yanayopaswa kupandwa katika maeneo yao,” amesema Majaliwa.

Uhifadhi wa chakula

Kuhusu uhifadhi wa chakula, Waziri Mkuu amebainisha kuwa Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Uhifadhi wa Chakula (NFRA) inaendelea kununua ziada ya mavuno kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kukihifadhi na kutumika kuongeza upatikanaji katika maeneo yatakayokumbwa na upungufu wa chakula.

Waziri Mkuu pia amewataka wananchi kutumia vizuri mavuno yaliyopatikana katika msimu wa kilimo wa 2023/24 kwa kutunza chakula cha kutosha kuanzia ngazi ya familia kwa kuzingatia kanuni bora za uhifadhi wa mazao ili kuepuka upotevu na kuhakikisha chakula kinadumu kwa muda mrefu.

“Vilevile nitoe wito kwa wananchi kutumia vizuri mavuno yaliyopatikana katika msimu wa kilimo 2023/24 kwa kutunza chakula cha kutosha katika ngazi ya kaya kwa kuzingatia kanuni bora za uhifadhi mzuri wa mazao ya chakula,” amesema Waziri Mkuu.

Wito kwa wananchi

Waziri Mkuu Majaliwa amesisitiza wananchi kuendelea kutumia chakula walichonacho kwa uangalifu mkubwa na kuhifadhi cha kutosha katika ngazi ya familia akionya dhidi ya matumizi mabaya ya chakula au yasiyokuwa ya lazima, kama hatua muhimu ya kuhakikisha usalama wa chakula kwa wote.

Katika juhudi za kupambana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa, Serikali pia imeahidi kuendelea kutoa ruzuku ya mbolea na mbegu bora kwa wakulima kwa msimu wa kilimo wa 2024/25, ili kuongeza uzalishaji wa mazao yanayokomaa kwa muda mfupi na yanayostahimili ukame.

“kwa kutambua mwenendo wa uzalishaji wa zao la mahindi na ongezeko la mahitaji yake ndani na nje ya nchi katika msimu wa 2024/25 serikali itatoa ruzuku ya mbegu bora  za mahindi kwa wakulima,” ameongeza Waziri Mkuu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks