Mmiliki wa ghorofa Kariakoo, Niffer kukamatwa

November 18, 2024 5:42 pm · Waandishi Wetu
Share
Tweet
Copy Link
  • Waziri Mkuu aagiza mmiliki wa jengo ambaye hajafahamika na mfanyabiashara mashuhuri mtandaoni, Niffe wakamatwe.

Dar es Salaam. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameliagiza Jeshi la Polisi kumtafuta na kumshikilia mmiliki wa jengo lililoanguka Kariakoo jijini Dar es Salaam na kusababisha vifo vya watu wasiopungua 16 na majeruhi 86 siku tatu baada ya kutokea ajali hiyo. 

Jengo hilo la ghorofa nne liliopo Mtaa wa Agrey na Mchikichi liliporomoka Novemba 16 mwaka huu majira ya Saa 3 asubuhi na kuwafunika wafanyabiashara na wanunuzi waliokuwemo ndani. 

Tangu itokee ajali hiyo kumekua na maswali mengi juu ya taarifa sahihi za mmiliki wa jengo hilo na mahali alipo. Hata hivyo, baadhi ya viongozi nyakati zote walipoulizwa na wanahabari walieleza kuwa kwa wakati huo kipaumbele kilikuwa ni kuokoa watu walioathirika na tukio hilo. 

Katika hotuba yake wakati wa tukio la kuaga miili ya watu 15 waliofariki katika ajali hiyo katika viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam, Majaliwa amelitaka Jeshi la Polisi kumtafuta na kumshikilia mmiliki wa jengo hilo ili aweze kusaidia Serikali kubaini chanzo cha ajali hiyo. 

Jengo liloporomoka ambalo Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameagiza mmiliki wake kukamatwa. Picha/Nukta.

Kwa mujibu wa Majaliwa watu watatu zaidi wamefariki dunia kutoka idadi ya watu 13 walioripotiwa na Rais Samia Suluhu Hassan jana. 

“Nimeagiza Jeshi la Polisi kumtafuta mwenye jengo popote alipo ili aweze kulisaidia jeshi la polisi kujua kwa nini jengo limeanguka,” amesema Majaliwa.

Jana katika hotuba yake kwa taarifa kuhusu ajali hiyo, Rais Samia alitaka polisi wachunguze kwa kina tukio hilo ikiwemo kumhoji mmiliki wa jengo hilo ambaye hafahamiki mpaka sasa. 

Hii si mara ya kwanza kwa jengo kubwa kuporomoka katikati mwa jiji huku sababu kubwa zikiwa ni ujenzi wa chini ya kiwango. Machi 2013, jengo la zaidi ya ghorofa 10 lililokuwepo makutano ya barabara ya Morogoro na Indra Gandhi liliporomoka na kukatisha maisha na watu na wengine kuwajeruhi.

Niffer naye akamatwe

Mbali na kukamatwa kwa mmiliki wa jengo hilo, Majaliwa amegiza kukamatwa kwa mfanyabiashara mashuhuri mtandaoni, Jennifer Jovin maarufu kama Niffer kwa tuhuma za kuchangisha michango kwa ajili ya waathirika wa ajali hiyo bila kibali. 

Majaliwa amesema kuna binti mmoja kwenye mitandao amechangisha watu kupitia namba yake ya simu bila kibali na tayari ameshakusanya fedha kutokana na michango hiyo. 

Tangu Jumapili iliyopita Niffer alikuwa akichangisha michango kutoka kwa wasamaria wema kiasi cha kufikia Sh37 milioni. 

“Huyu nimeagiza atafutwe na jeshi la polisi aje aeleze nani alimpa kibali? Amekusanya Shilingi ngapi? Amezipeleka wapi na kwa nini alifanya hivyo bila kibali kwa sababu hatutaki kuruhusu kuwa na mianya ya kuwasumbua Watanzania wakiwa kwenye huzuni,” ameeleza Majaliwa.

Rais Samia atoa pole

Majaliwa amewasilisha salamu za pole kutoka kwa Rais Samia kwa waombolezaji waliofika kuaga ndugu zao leo (Novemba 17, 2024) ambaye kwa sasa yuko nchini Brazil huku akiwataka wananchi, pamoja na wafiwa kuwa wavumilivu hasa katika kipindi hichi kigumu ambacho wamewapoteza wapendwa wao.

Katika kuhakikisha Serikali inashiriki kikamilifu, Majaliwa amewataka viongozi wa Serikali kushiriki katika shughuli zote za mazishi ndani au nje ya jiji la Dar es Salaam.

Hadi sasa vikosi vya uokoaji vinaendelea kuwatafuta watu walionasa katika vifusi vya jengo hilo huku Serikali ikiahidi kuwa inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha kuwa watu wote wanaokolewa haraka iwezekanavyo.

Habari hii imeandikwa na Calvin Makwinya na Fatma Hussein.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks