Ghorofa laporomoka Kariakoo, kadhaa wahofiwa kujeruhiwa, kupoteza maisha

November 16, 2024 11:10 am · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link

Dar es Salaam. Watu kadhaa wanahofiwa kujeruhiwa au kupoteza maisha kutokana na ajali ya kuanguka kwa ghorofa iliyotokea leo Novemba 16, 2024 katika Mtaa wa Kongo, Manyema na Mchikichi Dar es Salaam.

Jengo hilo linaelezwa kuporomoka majira ya saa tatu asubuhi ambapo kwa mujibu wa mashuhuda waliozungumza na Shirika la Utangazaji Tanzania ( TBC) ndani ya jengo hilo la kibiashara, kulikuwa na watu kadhaa waliokuwa wakifanya ununuzi katika maduka ya jengo hilo.

Mashuhuda hao wameeleza kuwa ghorofa hilo limeanguka ghafla majira ya saa 3:05 asubuhi wakati mafundi wa ujenzi walipokuwa kazini wakitoboa kwa ajili ya kuongeza sehemu ya maduka chini ya jengo hilo.

“Tulianza kusikia kelele za mtingishiko, kisha kwa ghafla jengo zima likaanguka, wananchi wameshindwa kujiokoa na kazi ya  ujenzi ilianza tangu jana, hivyo angetaka urahisi angebomoa tu jengo lote,” amesema mmoja wa mashuhuda, Harrison Shayo.

Shughuli ya uokoaji inaendelea kwa wananchi wakishirikiana na vyombo vya dola ikiwemo Jeshi la Zimamoto na Ukoaji ambapo Hadi saa 5 asubuhi bado hakuna taarifa ya moja kwa moja juu ya athari zilizosababishwa na kuporomoka kwa jengo hilo.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert  Chalamila aliyekuwa akizungumza na wananchi na wanahabari katika eneo hilo amesema majeruhi waliookolewa wamefikishwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Hata hivyo, amesema hadi sasa idadi ya majeruhi haijafahamika wala waliopoteza maisha,  akisisitiza takwimu rasmi zitatolewa baadaye.

Jengo hilo  linaelezwa kuwa lilianguka  saa tatu asubuhi, huku likiwa na zaidi ya asilimia 90 ya wafanyabiashara katika maduka hayo ambao walikuwa wanaendelea na shughuli zao za biashara.

Pamoja na wananchi wa kawaida baadhi ya watu waliofika kusaidia juhudi za uokozi ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Profesa Mohamed Janabi na Naibu Spika, Mussa Zungu.

Wengi wameokolewa

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema idadi ya watu waliokolewa ni kubwa na wachache wamepata majeraha.

“Watu wengi wameokolewa na kazi kubwa inaendelea,” amesema Muliro huku akitoa wito kwa watu waliofurika eneo hilo kutoa nafasi kwa wataalamu kufanya majukumu yao.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks