Utafanya nini pale ndoto yako inapokuingiza matatani?
- Ni filamu ya ‘Happiness’ inayohusu kuenea kwa kirusi cha hatari kinachofanya watu kugeuka ‘mazombie’.
Dar es Salaam. Kisa cha filamu hii kimebebwa na wahusika wakuu wawili, kijana ‘handsome’ Jung Hi Hyun pamoja na mrembo Yoon Sae Bom.
Wawili hawa walisoma katika shule moja’ high school’ japo hawakuwa na ukaribu kiviiile, hadi siku ambayo Hyun anapata shida na Bom anakuwa msaada wake.
Siwezi kukusimulia yote yaliyotekea hapo lakini baada ya miaka kupita wawili hawa wanafanikiwa kujiunga na jeshi la polisi katika vitengo tofauti huku wakiendelea na urafiki wao kwa kusaidiana majukumu ya hapa na pale ya kikazi.
Licha ya kuwa na kazi, wawili hawa maisha yao hayapo vizuri sana, kwani mahitaji ni mengi na mshahara wao unawabinya kufanya mambo mengine.
Kwa upande wa Hyun hilo halimpi shida kwani amesharidhika na anavyoishi, ila Bom yeye maisha hayo hayamridhishi na amekuwa na ndoto ya kukaa kwenye apartment nzuri yenye kila kitu.
Nahisi hii ni ndoto ya wengi, hata mimi ni mmoja wapo.
Unaweza kusema ndoto ya binti huyu inakaribia kutimia, kwani mkuu wao anawatangazia kuwa wamenunua apartment za maana kwa ajili ya wafanyakazi ambao watakidhi vigezo ikiwemo kuwa umeoa au kuolewa.
Bom anamwambia Hyun waandae ndoa ‘fake’ ili waweze kukidhi kigezo cha kupata ‘apartment’. Picha|Soompi
Pozi linamuisha binti huyu kwani hata boyfriend wa kusingiziwa hana…lakini mtihani wa kukubali kushindwa binti huyu alipata F, na kwa mantiki hiyo anakuja na wazo lake.
Anamuomba Hyun waandae ndoa fake ili wakizi kigezo cha kupata apartment hiyo.
Wazo hilo linafanikiwa na baada ya siku kadhaa wanakabidhiwa apartment yao. Furaha ilioje! kupata kile ambacho kilikuwa kama ndoto tu.
Mwanzo wa maisha ya ‘mikiki mikiki’
Maisha ya kwenye apartment ni mazuri, japo kila siku wawili hawa walikuwa wanasikia mlio wa ‘kudum kudum’ kama watu wanapigana hivi kutoka kwenye floor ya juu yao, lakini wakienda kuwauliza wahusika wanasema hakuna tatizo.
Hilo lilikuwa kero lakini wakaamua kulipotezea.
Siku moja Bom akiwa katika shughuli za kikazi, anaona wafanyakazi wenzie wawili wanapigana, lakini anaposogea kwa karibu anakutana na kitu tofauti.
Mfanyakazi mmoja ametapakaa damu usoni na anapomtazama kwa karibu anagundua kuwa mtu huyo amebadilika na kuwa kama ‘Zombie’.
Macho yamebadilika na kuwa meupe, mishipa mieusi imetapakaa usoni, huku kucha zikiwa ndefu na za kutisha.
Akiwa katika bumbuwazi anajikuta akishambuliwa na mtu huyo na katika harakati za kujiokoa Bom anaparuriwa mkononi mwake.
Kwa tuliozoea kutazama filamu za mazombie basi tunajua kuwa ni suala la muda tu Bom nae ataanza kushambulia watu.
Bom anabebwa na kwenda kufanyiwa vipimo kama huenda na yeye ameathirika, cha ajabu ni kuwa anapofika huko anagundua kuwa eneo hilo ambalo lilikuwa ni mabweni ya shule limejaa mamia ya watu kama yule aliyemshambulia.
Kumbe kuna kirusi cha hatari kinasambaa nchini humo ambacho kinafanya watu kuwa mazombie kwa kushambuliwa wengine na kuwanyonya damu na baada ya muda wanafariki dunia.
Lakini cha ajabu wananchi hawana taarifa yoyote kwa kinachoendelea.
Uchunguzi wa siri unaendelea kujua chanzo cha kirusi hicho, na baadae inakuja kugundulika kuwa moja ya sababu ya kirusi hicho ni kidonge cha ‘Next’ maalum kwa kupunguza maumivu kwa watu wa mazoezi.
Kimbembe ni kuwa kidonge hicho kinatumika sana kwenye gym ya apartment wanayokaa wakina Bom, na ubaya ni kuwa mamia ya wakazi wa jengo hilo wameshakitumia.
Kwa kulifahamu jambo hilo, daktari mwanajeshi Han Tae ambaye amekabidhiwa mamlaka ya kushugulikia kirusi hicho anaweka uzio wa kulitenga jengo hilo na watu wengine, huku umeme na maji vikikatwa kwa muda wa wiki moja ili kuona mabadiliko yatakayotokea kwa wakazi wa jengo hilo.
Maisha ya taabu, hofu, njaa, na kuuana kwa wakazi wa jengo hilo yanaanza, na huenda hata hiyo wiki moja ikawa ndefu kwa wote kuteketea.
Bila shaka ungekuwa Bom, ungejuta na kujilaani siku ulipoamua kuhamia kwenye jengo hilo, lakini ndiyoo hivyo unajikuta unakumbuka shuka wakati kumekucha.
Unahisi mwisho wa filamu hii utakuaje? Je kuna mtu ambaye atabahatika kunusurika? Na vipi kuhusu Bom ambaye alishakwaruzwa na yule zombie?
Uhondo wote upo kwenye filamu hii ya muendelezo ya Happiness ambayo utaipata katika jukwaa la filamu la mtandaoni la Netflix.