Ufanye nini nyumba ikizingirwa na mafuriko?
- Hatua ya kwanza ni kuwasiliana na mamlaka husika kwa ajili ya kutoa msaada.
- Wataalamu wasema mafuriko ni janga la dharura linalohitaji kushughulikiwa mapema.
Arusha. Kwa wakazi wa baadhi ya maeneo nchini mafuriko ni janga linalojirudia mara kwa mara likisababisha uharibifu mkubwa wa mali na miundombinu.
Janga hilo linalotokana na sababu za kimazingira pamoja na shughuli za binadamu kama vile ukataji wa miti na ujenzi ndani ya mikondo ya maji, hupelekea mamia ya Watanzania kupoteza makazi yao ya kudumu, huku wengine kupoteza maisha.
Ndani ya miaka kadhaa iliyopita baadhi ya mikoa ikiwemo Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Manyara na Arusha imeripoti mafuriko katika vipindi tofauti tofauti na kuacha maumivu kwa wakazi wa maeneo hayo.
Huenda janga hilo likajitokeza tena mwaka huu katika baadhi ya mikoa nchini kufuatia tahadhari ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA ) iliyotangaza uwepo wa vipindi virefu vya mvua ndani ya kipindi cha masika kuanzia Machi hadi Mei, 2026.
Pamoja na kufuata ushauri wa TMA wa kuhama mabondeni, yafuatayo ni mambo matatu muhimu unayotakiwa kufanya ikiwa nyumba yako au eneo unaloishi limezungukwa na maji yatokanayo na mafuriko.
Toa taarifa kwa mamlaka husika
Baada ya kukumbwa na mafuriko Inashauriwa kutoa taarifa kwa mamlaka zinazohusika na masuala ya dharura ikiwemo Shirika la Umeme (Tanesco) au Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa ajili ya kutoa msaada.
Meneja wa Afya na Usalama Kazini kutoka Tanesco, Fredy Kayega amewashauri wananchi kutoa taarifa kwa haraka pale tu wanapobaini kutokea kwa mafuriko katika maeneo yao.
“Suala la mafuriko ni suala la dharura, tunashauri mteja awapigieTanesco ili watoe miundombinu ya umeme ili iisije ikamuathiri mteja kwa maana umeme na maji haviendani, maji yanapitsha umeme,” amesema Kayega.

Kupanda juu ya nyumba baada ya mafuriko hukufanya uwe salama wakati ukisubiri msaada kutoka kwa mamlaka husika.Picha/ Jamii Forums.
Zima vyanzo vya umeme, gesi
Wakati unasubiri msaada kutoka kwa viongozi wa Serikali na taasisi za kiusalama ni vyema kuzima vyanzo vyote vya umeme na gesi ili kuepuka majanga ya moto na mengineyo yanayoweza kujitokeza kupitia miundombinu hiyo.
“Usizime umeme ukiwa umesimama kwenye maji, na kama maji tayari yamefika kwenye mfumo wa umeme, ondoka na subiri wataalamu wakague kabla ya kuwasha tena….
…Weka mtungi ya gesi sehemu ya juu isiyofikiwa na maji. Ukihisi harufu ya gesi, usiwashe moto au taa, fungua madirisha kama si salama toka nje haraka,” imesema taarifa ya Kituo cha Udhibiti wa Magonjwa nchini Marekani (CDC).
Panda sehemu ya juu ya nyumba
Ukihakikisha miundombinu ya umeme na gesi imezimwa kikamilifu unashauriwa kupanda eneo la juu zaidi ikiwemo katika paa la nyumba ili kusubiri msaada.
Eneo hilo la juu halitakufanya uwe salama pekee bali litakusaidia kuonekana kwa urahisi na mamlaka zinazohusika na uokoaji au msaada wowote unaoweza kujitokeza kwa haraka.
Baada ya kupata msaada na maji ya mafuriko kukauka unashauriwa kuendelea kufuatilia taarifa za mamlaka za hali ya hewa na usalama kabla ya kurejea katika makazi hayo ili kuepuka hatari nyingine ziinazoweza kutokea.
Latest