Kumpoteza mtu umpendaye ni mwanzo wa safari mpya
- Ni simulizi ya filamu ya Sing sehemu ya pili.
- Mafunzo yanayoambatana na filamu hii, ni pamoja na kutokukata tamaa hata maisha “yanapokupiga na kitu kizito”.
- Ni filamu nzuri inayoweza kumfunza mengi mtoto na hata mtu mzima.
Ni kweli. Kumpoteza mtu ambaye unampenda kunaweza kukurudisha nyuma katika kila unalolifanya.
Iwe baba, mtoto, mke, mume na hata rafiki wa karibu, kuondoka kwake maishani kunaweza kukutafakarisha endapo maisha yako yatakuwa kama yalivyokuwa awali.
Kumkosa kutakufikirisha kuhusu matembezi mliyofanya pamoja, vicheko vilivyowapatia nuru usoni na zaidi, upendo thabiti uliokuwepo kati yenu.
La muhimu kufahamu ni kuwa, hata kama mpendwa wako ameenda, maisha yako lazima yaendelee.
Hii hapa filamu ya kukufahamisha kuwa, kumpoteza mtu umpendaye, ni mwanzo wa safari mpya ya maisha.
Filamu hii inamleta tena Buster Moon, mdau wa sanaa za maonyesho ambaye kutengeneza show ya muziki inayoweza kukusanya sayari zote ni kitu kidogo sana.
Baada ya mafanikio yake kwenye filamu ya Sing 1, Moon anakutana na mlima mwingine wa kuvuka. Ni Mlima wa kupeleka vijana wake kwenye ngazi nyingine kimuziki.
Ngazi hiyo ni katika jiji la Redshore ambako muziki ni kama pumzi. Kila mwanadamu anaivuta.
Mlima anaokutana nao Moon ni kukatishwa tamaa na unasogezwa kwake na mwanadada Suki, msaidizi wa msaka talanta, Jimmy Crystal.
Ash anapata kibarua cha kumshawishi mwanamuziki ambaye alitelekeza talanta yake kwa miaka 10 kurudi stejini. Picha| Variety.
Suki anamwambia Moon tena bila kupepesa macho kuwa, hata iweje, hawezi kufika Redshore na ikitokea akafika, hawezi kufanikiwa.
Ni kama leo hii CR7 au Messi amwambie mtoto wake aachane na mpira aende tu akalime.
Hata hivyo, sisi siyo wageni kwa Moon bwana!, kama ni maneno tu, ameambiwa na wengi lakini hayakutoboa.
Siku siyo nyingi, Moon anaikusanya timu ya wanamuziki aliokuwa nao kwenye filamu ya kwanza, nazungumzia Sing 1.
Rosita, Ash, Johnny, Meena na Gunter ambao bila shaka, moto wao kivokali unaufahamu.
Anachokifanya Moon ni kukwea pipa na watu wake na kuibuka huko Redshore ambako aliambiwa hawezi kufika na akiwa huko, anacheza faulo na kunyaka nafasi ya usaili mbele ya Crystal.
Na kweli, kama alivyoambiwa na Suki, wazo la moon halikutoboa.
Hata hivyo, Gunter anaokoa jahazi baada ya kuibuka na wazo la show ambayo mandhari yake ni ya nje ya sayari.
Kwa kuongeza, Gunter anasema hata mwanamuziki maarufu aliyepoteana naye kwenye tasnia ya muziki kwa miaka 10, Clay Calloway naye atakuwepo kwenye show hiyo.
Ajabu! Crystal anafurahishwa na wazo hilo na anawapatia wiki tatu kuandaa show hiyo.
Soma zaidi:
- Filamu ya kuchangamsha sikukuu za mwisho wa mwaka
- Monster Hunter: Filamu ya kuisindikiza wikiendi yako
- Umafia na wema: Filamu ya “Raya and the Last Dragon” inavyofundisha ujasiri, umoja
Mwanzo wa tafrani
Mambo huku ni bam bam kwani wasanii hawa walitaka show na show wameipata. Kazi inabaki kwa Moon kuhakikisha mambo yanafanikiwa.
Wakati wa maandalizi, sintofahamu zinaanza kutokea. Rosita ambaye onyesho lake lilihusisha kuruka kutoka juu ya ukumbi, anapatwa na kihumwe humwe cha kuruka hivyo nafasi yake inachukuliwa na binti wa Crystal ambaye kwa kweli, haendani na onyesho hilo.
Johnny naye anayekutanishwa na mwalimu wa kucheza dansi, anahisi mwalimu wake hampendi na anamtamkia kuwa, hatoweza kufanikiwa.
Meena Mavokali naye ana mlima wake. Onyesho lake linatakiwa kuwa la kuonyesha mahaba ama kwa kizungu, “romantic scene” lakini mtu anayepangwa naye, haviumani.
Moon naye anayavuruga kwa Crystal na kuishia kuwindwa. Akiwa kwenye hali hiyo, anawaza kukimbia na kutelekeza kila kitu kama alivyowahi kufanya awali.
Huku nako, yule nguli wa muziki aliyetazamiwa kuimba kwa mara ya kwanza baada ya kupotea kwa muda mrefu, naye ndio hivyo hataki hata kusikia masuala ya kuimba.
Shabiki wameshajipanga kwenye ukumbi wa maonyesho wakisubiri burudani lakini nani atakayeitoa?
Fuatilia filamu ya “Sing 2” kupitia kumbi za filamu za Century Cinemax kwa gharama hadi Sh10,000 tu msimu huu wa sikukuu.
Kutana na nguli wa muziki kwenye filamu moja akiwemo Tory Kelly, Pharell Williams, Halsey na Bono katika filamu hii iliyoandaliwa na waandaaji walio nyuma ya filamu kama Minions, Dispicable me na pets.
Sing 2 itakuacha na mafunzo mengi yanayoweza kukusaidia kuanza upya mwaka 2022 kama kuwasaidia wengine na kuwapa moyo waliopondeka.