Magufuli atoa mwelekeo mpya ushirikiano nchi za Afrika, Nordic

November 8, 2019 8:13 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Ameshauri ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afrika na Nordic unapaswa kubadilika.
  • Amesema ubadilike kutoka katika kutoa na kupokea misaada na kujikita katika diplomasia ya kukuza uchumi.
  • Tanzania ni mnufaikaji mkubwa wa misaada ya Nordic hasa ya elimu. 

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ameshauri ushirikiano uliopo kati ya nchi za Afrika na Nordic ubadilike kutoka katika kutoa na kupokea misaada na kujikita katika diplomasia ya uchumi itakayochochea uzalishaji wa bidhaa na biashara baina ya nchi hizo.

Nchi za Nordic zinajumuisha Denmark, Finland, Iceland, Norway na Sweden.

Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza leo (Novemba 8, 2019) jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Afrika na Nordic, amesema viongozi wa Afrika wametambua mstakabali wa bara lao ni kuachana na utegemezi wa kiuchumi ili kuwa na uhuru wa kujiamualia mambo yao. 

“Kwa muda mrefu ushirikiano wetu umejikita katika kutoa na kupokea misaada. Ushirikiano wa aina hii siyo endelevu na wala hauhitajiki katika mazingira ya sasa,” amesema Rais.

Amesema kutafuta ukombozi wa kiuchumi, ndilo jukumu la viongozi wa sasa wa Afrika ili kuwaletea wananchi maendeleo ambapo uhuru wa kisiasa hauwezi kuwa na maana kama hauleti matunda ya kiuchumi. 

“Hivyo basi ni lazima tubadilishe mwelekeo na kuingia katika uhusiano wa kisasa baina ya mataifa ambao unajikita kwenye ushirikiano wa kiuchumi kupitia biashara na uwekezaji,” amesema. 

Aidha, Rais amesema uwezo na fursa za kuingia kwenye ushirikiano mathubuti wa kiuchumi ipo kwa sababu nchi za Afrika zina rasilimali nyingi ambazo zikitumiwa vizuri zitasaidia kuinua uchumi wa bara hilo. 

Lakini hilo halitawezekana kama Afrika haitajifunza kutoka nchi za Nordic zenye watu takriban milioni 27 ambazo zimepiga hatua kubwa ya maendeleo kwa rasilimali zao.

“Pato lao kwa mwaka 2018 lilikuwa na thamani ya dola za Marekani trilioni 1.7. Kwa upande wetu, bara la Afrika lina kilomita za mraba milioni 30.37 na idadi ya watu wapatao bilioni 1.2.

“Hata hivyo kwa mwaka jana 2018, pato lote la nchi za Afrika lilikuwa na thamani ya dola za Marekani trilioni 2.334.  Sisi Waafrika tuna jambo kubwa la kujifunza,” amesisitiza Rais Magufuli.


Zinahusiana: 


Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Afrika na Nordic utakuwa na ajenda kuu mbili; kujadili hali ya amani na usalama katika nchi za Afrika na jinsi ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara utakaochochea ukuaji wa uchumi wa nchi hizo.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof Palamagamba Kabudi amesema ajenda hizo zitajadiliwa kwa kina na kutoka na mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha na kuendeleza uhusiano huo. 

Mkutano huo wa 18 unafanyika Tanzania kwa mara ya kwanza na mwaka 2020 utafanyika nchini Finland.

Tanzania ilivyofaidika na nchi za Nordic

Hata wakati Rais Magufuli akishauri ushirikiano wa Afrika na nchi za Nordic ubadilike, amesema nchi hizo zina mchango mkubwa katika ukombozi wa bara la Afrika na utekelezaji wa miradi ya maendeleo. 

“Uhusiano wa nchi za Afrika na Nordic ni wa muda mrefu ulianza kabla ya uhuru wa nchi nyingi za Afrika kupatikana. Na kwa kusema kweli nchi za Nordic zilisaidia sana katika harakati za ukombozi kwenye nchi mbalimbali hususan Kusini mwa Afrika,” amesema.

Akizungumzia Tanzania, Rais amesema  imenufaika na miradi mingi ya maendeleo ikiwemo kituo cha Elimu cha Kibaha (Kibaha Education Centre) cha mkoani Pwani  na Kituo cha utafiti wa kilimo cha Uyole kilichopo mkoani Mbeya.

Nchi za Nordic zilisaidia kujenga vyuo vya ufundi na kwenye kampeni ya kufuta ujinga yaani (Literacy campaign program) iliyotekelezwa katika miaka ya 1970 na kuiwezesha Tanzania kufuta ujinga kwa asilimia 98 na hivyo kuwa miongoni mwa nchi za kwanza Afrika kufikia kiwango hicho.

“Na mimi kwa leo nataka niwashukuru kwa sababu na mimi pia ni product (mnufaika) ya nchi za Nordic. Degree (shahada) yangu ya pili kwa miaka yote mitatu nikifanya thesis na research (utafiti), zilizotolewa fedha na nchi ya Norway kwa kupitia shirika la Norad (Shirika la maendeleo la Norway),” amesema Rais Magufuli katika hotuba yake. 

Follow us on TikTok

Nukta Habari

FOLLOW NOW
Subscribe to our channel

Nukta TV

SUBSCRIBE NOW
🔴LIVE: RAIS SAMIA ANAZINDUA MELI YA KWANZA YA UVUVI WA BAHARI KUU

🔴LIVE: RAIS SAMIA ANAZINDUA MELI YA KWANZA YA UVUVI WA BAHARI KUU

Nukta TV

Kwa nini wanawake wako katika hatari zaidi kupata magonjwa ya akili?

Kwa nini wanawake wako katika hatari zaidi kupata magonjwa ya akili?

Nukta TV

🔴LIVE: HOMERA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA BUNGENI

🔴LIVE: HOMERA AKIWASILISHA HOTUBA YA BAJETI YA WIZARA YA KATIBA NA SHERIA BUNGENI

Nukta TV

BENEFIT FROM
Nukta ADS
Advertise with us to reach a wider audience with high conversion rates.
Other Nukta Africa Products
Nukta Habari
Stories that matter
Topics
Inuldge yourself with the topics in Nukta
All
Business
Africa
Contact
Tel
+255 750 881 888
Mail
newsroom@nukta.co.tz
Address
Mwananyamala kwa Kopa Dabe House Dar es Salaam TZ, 14108
Social Media

© 2024 Nukta Africa. All Rights Reserved.