Paul Makonda ateuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo
Arusha. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya utenguzi na uteuzi wa viongozi mbalimbali akiwemo Paul Makonda aliyeteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni Sanaa na Michezo.
Kulingana na taarifa ya Bakari Machumu, Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, iliyotolewa usiku wa Leo Januari 8, 2026, uteuzi wa Makonda unakuja ikiwa zimepita siku 53 toka ateuliwe kuwa Naibu Waziri katika wizara hiyo.
“Paul Christian Makonda ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Kabla ya uteuzi huu, Makonda alikuwa Naibu Waziri katika Wizara hiyo,” inaeleza sehemu ya taarifa hiyo.


Viongozi wengine walioteuliwa ni Patrobas Paschal Katambi, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi akichukua nafasi ya George Simbachawene ambaye ametenguliwa.
Kabla ya uteuzi huo, Katambi alikuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara.
Rais Samia pia amemteua Profesa Palamagamba Kabudi kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Ikulu (Kazi Maalum).Profesa Kabudi kabla ya uteuzi huo alikuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Aidha, Dennis Lazaroi Londo ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, ambapo awali alikuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, huku Ayoub Mohamed Mahmoud akiteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Katika ngazi ya Katibu Mkuu, Rais Samia amemteua Dk Richard Stanslaus Muyungi kuwa Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira. Dk Muyungi anachukua nafasi ya Mhandisi Cyprian Luhemeja ambaye ameteuliwa kuwa Balozi.
Kwa upande wa uteuzi wa mabalozi, Rais Samia amemteua Mhandisi Zena Said, Waziri Salum ambaye alikuwa katibu wa Rais pamoja na Meja Jenerali Mbaraka Mkeremy kuwa Balozi.
Sambamba na hao, amemteua Ally Samaje kuwa Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST), akichukua nafasi ya Dk Mussa Budeba.
Pia, Rais amemtengua Mwenyekiti wa Bodi ya Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Kaboni (NCMC), Profesa Eliakimu Zahabu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo uapisho wa viongozi hao utafanyika Januari 13,2026 Chamwino Dodoma saa nane mchana.
Latest