Magufuli ambana Simbachawene mafao ya polisi wastaafu
- Ashangaa wastaafu kutolipwa mafao yao, licha ya viongozi wa wizara kuwepo.
- Amtaka Waziri Simbachawene kulishughulikia suala hilo kwa haraka.
Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, John Magufuli amechukizwa na kitendo cha wastaafu wa Jeshi la Polisi kucheleweshewa mafao yao licha kuwa fedha zao zipo, huku akiibebesha lawama Wizara ya Mambo ya Ndani na kuitaka aishughulikie suala hilo haraka.
Dk Magufuli aliyekuwa akizungumza wakati akizindua majengo ya Chuo Cha Polisi kilichopo Kurasini jijini Dar es Salaam leo Februari 26, 2021 amesema anashangaa kwanini wastaafu hao ambao wameitumikia nchi kwa uaminifu wanazungushwa kupata mafao yao.
“Kuna suala limezungumzwa hapa la wastaafu wa Jeshi la Polisi kutokulipwa mafao yao, msema kweli mpenzi wa Mungu, mimi nawashangaa Wizara ya Mambo ya Ndani na nina uhakika hata raia wengine wanawashangaa yule mstaafu wako amefanya kazi nzuri katika miaka yake yote.
“Amemaliza Jeshi la Polisi bila tatizo lolote, anatakiwa kulipwa mafao yake na mafao yake yapo, Waziri utakaa ofisini bila kwenda kuwaombea kwa nini? Katibu Mkuu umekaa ofisini tu, Naibu Katibu Mkuu umekaa ofisini tu, kwanini usichukue haya majina ukatembea ukaenda Wizara ya Fedha ukasema nina wastaafu hapa nataka fedha zao ziende,” amehoji Rais Magufuli.
Soma zaidi:
- Rais Magufuli kuzuru Mwanza, Simiyu na Mara kwa siku saba
- Magufuli sasa aangazia rada kuongeza mapato Tanzania
Amesema lawama zote za kucheleweshewa mafao ya polisi waliostafu zinapaswa kuelekezwa kwa viongozi wa juu ya wizara hiyo na Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro kwa kushindwa kutimiza wajibu.
Rais amebainisha kuwa kinachokosekana kwa viongozi hasa mawaziri katika kushughulikia kero za wananchi ni kutokuwepo kwa mawasiliano mazuri baina yao.
“Huu ni wajibu wa Wizara ya Mambo ya Ndani, nikificha nitakua mnafiki, mimi nilipokuwa Waziri wa Ujenzi, tunapopata shida za wakandarasi, nilikuwa naenda kufanya fujo pale wizara ya ujenzi. Simbachawene nadhani amesikia hizo habari, wala hawakunipenda Wizara ya Ujenzi. Naenda wizara ya fedha nataka hela za makandarasi. Na nilikuwa nalipwa,” amesema Magufuli.
Kutokakana usumbufu huo kwa wastaafu, kiongozi huyo mkuu wa nchi amemuagiza Waziri Simbachawene kulishughulikia suala hilo ndani ya wiki moja ili wastaafu hao wapate mafao yao kwa sababu wamejitoa sana kwa ajili ya Taifa lao.
Latest