Magufuli sasa aangazia rada kuongeza mapato Tanzania

Zahara Tunda 0401Hrs   Novemba 02, 2018 Habari

Rada inatumika katika kuangalia kwa karibu angani na kuhakikisha usalama wa anga kwa kujua ndege zinazopita kwenye anga la nchi.Picha|http://mtanzania.co.tz


  • Kwa sasa Tanzania ina rada moja inayohudumia asilimia 25 ya anga.
  • Uhaba wa rada umeikosesha nchi mapato ya tozo ya takribani Sh1.2 bilioni.
  • Kukamilika kwa rada nne kutafungua fursa mbalimbali ikiwemo ongezeko la watalii.

Dar es Salaam.  Huenda Tanzania ikaongeza kiwango kikubwa cha mapato yatokanayo na usafiri wa anga baada ya kukamilika mradi wa ufungaji rada nne za kufuatilia mwenendo wa ndege zinazopita nchini Mei 2019.

Akizungumza katika kongamano la hali ya uchumi na siasa nchini liloandaliwa na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana Novemba 1, 2018, Rais John Magufuli amesema kwa muda sasa ndege za mataifa mbalimbali zimekuwa zikitumia anga la Tanzania bila kulipa na kuikosesha nchi mapato ambayo yangetumika katika shughuli mbalimbali za maendeleo. 

“Tumenunua rada zinafungwa katika katika maeneo yote Dar es Salaam na Tanzania ili ndege zinazopita lazima zilipe,” amesema Rais.


Amebainisha kuwa kufungwa kwa rada hizo kutafungua milango ya fursa mbalimbali ikiwemo watalii wengi kuja nchini na kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

 “Mengine ambayo tumefanya ni kama hayo kununua ndege, sisi watalii tunaowapata katika nchi yetu walikuwa hawafiki milioni 1.5. Nchi ya Morocco na Egypt (Misri) watalii wanafika mpaka milioni 10 kwa mwaka, sababu kubwa ni kwasababu wana shirika la ndege zao,

“Huwezi ukategemea shirika la ndege la jirani ulete watalii katika nchi yako, tumeamua ndio maana tumenunua hizi ndege hatukukopa nchi yoyote,” amesema Rais.


Zinazohusiana: Hatua zitakazokusaidia umalize mchakato wa 'Airport' bila usumbufu

                             Mambo unayotakiwa kufanya ukifika mapema ‘Airport’


Rada iliyopo imedumu kwa takribani miaka 16 tangu ifungwe mwaka 2002, lakini ujio wa rada zingine nne huenda ukachochea ongezeko la ndege zinatazotua nchini kutokana na  kuimarika kwa usalama wa anga.

Mapema Aprili mwaka huu Rais Magufuli alipokuwa akiweka jiwe la msingi katika ujenzi wa mfumo wa rada za kuongoza ndege alinukuliwa akisema nchi hupoteza takribani 1.2 bilioni za tozo kwa mwaka kutokana na kutokuwa na rada zinazojitosheleza.

"Tanzania ina rada iliyonunuliwa mwaka 2002 na ina uwezo wa kuhudumia anga kwa asilimia 25 tu lakini  kukamilika tutarejeshewa sehemu hiyo," alinukuliwa Rais Magufuli.  

Hali hiyo imeifanya nchi kupoteza mapato mengi kutokana na kukosekana kwa usimamizi mzuri wa ndege zinazotumia anga la Tanzania na wakati mwingine kuiweka nchi katika hatari ya kiusalama.

Mradi wa kufunga rada hizo unafadhiliwa na Serikali ya Tanzania kwa asilimia 100 ambapo kiasi cha bilioni 67.3 kinatumika na unatarajiwa kukamilika Mei 2019. 

Kampuni ya M/S Thales Las France SAS ya nchini Ufaransa ilipata tenda ya kufunga rada hizo  katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam, Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mwanza na  Songwe mkoani Mbeya.

Related Post