Maeneo ya kujidai sikukuu ya wapendanao ukiwa Arusha

February 6, 2021 10:23 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Zipo sehemu nyingi unazoweza kutembelea zikiwemo mbuga za wanyama na sehemu za kufurahisha macho na moyo.
  • Kuogelea, kupata picha za kumbukumbu na kununua vitu vidogo vidogo kwa ajili ya nyumbani kwako ni kati ya vitu vinavyoweza kuifanya “Valentines’s day” ya mwaka 2021 ya kipekee.

Dar es Salaam. Ni msimu wa rangi nyekundu. Meseji za makopa kopa, maua ya kuchagiza upendo na kumuonyesha umpendaye kuwa mbali na yote yanayoendelea katika maisha yenu, ni yeye tu ndiye anayeushikilia moyo wako.

Licha ya kuwa mapenzi kati ya wawili huhitaji jitihada za kila siku, wengine, wamejiandaa kuonyesha mahaba yao kwa namna tofauti katika siku ya kilele cha wapendanao almaarufu kama Valentine’s Day ambayo itakuwa Jumapili (Februari14, 2021).

Endapo wewe na mpenzi wako bado hamjapanga cha kufanya katika siku hiyo, yafuatayo ni mapendekezo unayoweza kuangazia hasa kama wewe ni mpenzi wa shughuli za utalii na kwa leo tunaangazia katika jiji la Arusha.

Kuogelea katika chemichemi za Kikuletwa

Inahitaji wawili tu kuikamilisha siku ya wapendanao. Vipi mkiachana na nguo zenu za ofisini na kuvalia  nguo za kuogelea?

Uwapo Arusha, utahitaji kutembelea chemichemi za Kikuletwa ambazo utazifikia kwa umbali wa saa mbili kutokea Arusha mjini kwa usafiri wa gari.

Uzuri huu wa Tanzania ulijificha ndani ya uoto mzuri wa asili na mazingira ya kusahaulisha mafarakano yote mliyowahi kuwa nayo kati yako na mpenzi wako ni kati ya sehemu unazoweza kuzitembelea ukiwa Arusha.

Maji safi, upepo wa kusuuza moyo na samaki  wadogo wadogo ndiyo upekee wa chemichemi za Kikuletwa zilizopo katia kijiji cha Rundugai

Ni wakati wa kutengeneza kumbukumbu mpya. Picha| Landside Advventures.

Jifunzeni zaidi kuhusiana na madini ya Tanzanite

Kwa wengine, huenda madini hayo wameyaona kwenye picha ama video za bilionea Saniniu Lazier aliyepata madini hayo mara mbili mwaka jana.

Uwapo Arusha, zipo sehemu nyingi ambazo unaweza kuzitembelea na kujifunza kwa undani kuhusiana na historia ya madini hayo.

Pata nafasi ya kufahamu nani alitoa jina hilo, lini ilikua mara ya kwanza kupikana na je, nani aliyegundua madini hayo?

Wewe na umpendaye mnaweza kutembelea sehemu mbalimbali ikiwemo Blue Plaza, mtaa wa India kufahamu nje ndani juu ya madini hayo. Huwezi jua, unaweza kupata wazo la zawadi kwa ajili ya umpendaye.

Tembeleeni Soko la Masai

Kuanzia shanga zilizotengenezwa kwa umaridadi, nguo za kimasai za kutosha kuacha mdomo wako wazi, picha na michoro mbalimbali miongoni mwa kazi za sanaa na mengine mengi yanayoweza kunichukua siku nzima kutaja ni kati ya vitu unavyoweza kuvikuta katika soko hili.

Ukiwa na umpendaye, mnaweza kufurahia kupata picha za pamoja katika soko hili huku mkidumisha utalii wa ndani kwa kufurahia na kutunza cha nyumbani.

Pia mnaweza kupata vitu viwili viitatu vya kununua na kurudi navyo nyumbani kama kumbukumbu ya safari yenu.


Soma zaidi:


Endesha mtumbwi katika Ziwa Duluti

Hakuna kitu kizuri kama wawili kuwa katikati ya maji ndani ya mtumbwi mkifurahia uzuri wa asili wa Tanzania katika Ziwa hilo lililopo wilayani Meru.

Najua  tayari unajenga picha kichwani ya mangapi unaweza kufanya. Ni wakati wa kutengeneza kumbukumbu zingine mbali na picha za harusi au zozote mlizonazo kwa kukaa katika maeneo tofauti.

Itakuchukua safari ya takribani dakika 15 kufikia ziwani na ndani ya saa moja na nusu, utakuwa umemalizana na shughuli hii, ukitaka zaidi, kazi ni kwako.

Ndani ya Arusha, yapo mengi ya kufanya. Unaweza kufurahia nyama choma na chakula asilia, kutembelea mbuga za wanyama ikiwemo Ngorongoro na Hifadhi ya Taifa ya Arusha ukiwa karibu  na umpendaye.

Unashauriwa kuipanga siku hii mapema ili kufahamu gharama utakazozitumia na kuwa na uhakika wa muda ambao utautumia kutembelea sehemu mbalimbali.

Ni ajabu mambo hayo yote unaweza kuyafanya kwa muda mfupi ukiwa Arusha.

Ukiwa Ziwa Duluti, utapata raha ambazo hujapata maeneo mengine. Picha|Mtandao.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW