Maoni ya Watanzania kuelekea siku ya wapendanao Februari 14

February 12, 2021 8:48 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Wakati siku hiyo ikiadhimishwa, baadhi hutengeneza kumbukumbu nzuri huku wengine wakibaki na kumbukumbu za kurudia ubachela.
  • Wadau wafunguka kuwa mapenzi ni vigumu kuyaonyesha kwa siku moja hasa kwa wanaopendana.
  • Zawadi, mitoko na jitihada kutoka kwa mpenzi ndio hutarajiwa kwa wale waliopo ndani ya mahusiano.

Dar es Salaam. Kusikia tu kuhusu siku  ya wapendanao duniani (Valentine’s Day) inaweza kuwa ni chanzo cha msongo wa mawazo kwa baadhi ya watu hasa waliopo katika mahusiano. 

Ajabu ni kuwa, hata baadhi ya wasio katika mahusiano nao hupatwa na fikra za hapa na pale juu  ya siku hiyo inayoadhimishwa Februari 14 kila mwaka.

Katika siku hii, rangi nyekundu inayoashiria upendo hutawala kuanzia mavazi na hata zawadi ambazo hutolewa kwa wanaopendwa kwa kufungashwa kwa umaridadi zikifunikwa na vifungashio vya rangi nyekundu.

Kwa wengine, ni kuonyesha upendo kwa wapendwa wao, wengine ni kutengeneza kumbukumbu na kwa wale ambao siyo kitu kwao huendelea na shughuli zao bila kujali kama siku hiyo inaadhimishwa.

Siku ya Valentines ni nini?

Kwa mujibu wa tovuti ya history.com mwezi mzima wa Februari umekuwa ukisherehekewa kama mwezi wa mapenzi kwa muda mrefu huku kilele kikiwa siku ya Valentines ambayo imepewa jina hilo kutoka kwa Nabii Valentines.

Kisa halisi cha Nabii Valentines kinahusishwa bado ni nadharia kwani kimejadiliwa kwa namna tofauti tofauti. Wapo wanaosema Nabii Valentines alikuwa akifungisha ndoa wanajeshi ambao waliamuliwa kutokuoa na mtawala Claudius wa pili, ipo mijadala inayosema Nabii huyo  aliuliwa kwa sababu alisaidia wafungwa kutoroka katika magereza na mijadala mingie mingi.

Zawadi ndogondogo huenda zikatosha kumpatia umpendaye katika siku ya wapendanao. Picha| freepik.com

Siku hiyo ina maana gani?

Nukta Habari (www.nukta.co.tz) imekuletea maoni tofauti ya Watanzania wanavyoielewa na wanavyosherekea siku hiyo. Pia mambo yanayofanyika siku ili kudumisha upendo kwa wapendanao.

Mfanyabiashara wa mkoani Shinyanga Cassandra Hassan anasema siku ya Valentines ni siku iliyoanzishwa na Mtakatifu Valentine kwa ajili ya kutoa salamu, zawadi na kuelezea hisia kwa familia au urafiki baina ya watu.

Kwa Hassan siku hii ina umuhimu kuadhimishwa kwa sababu inakumbusha upendo zaidi na unaweza kuadhimisha na mtu yeyote umpendaye. Anaweza kuwa baba, mama, mpenzi wako na hata rafiki wa karibu.

Siku ya wapendanao inavyoyumbisha mahusiano

Licha ya kua siku ya wapendanao inatakiwa kuwasogeza wapendanao karibu zaidi, kwa baadhi imekuwa sivyo kwani katika siku hii, baadhi ya mahusiano hufikia tamati.

Mkazi wa Dar es Salaam Alma Miraji amesema, “Valentine inaletaga stress (mawazo) sana siku moja tu lakini inaweza vunja mahusiano ya watu.”

Hali hiyo mara nyingi husababishwa na matarajio ambayo baadhi ya watu wanakua nayo ikiwemo kupata zawadi za kuvutia, mlo tofauti na nyumbani (dinner) huku wengine wakitarajia hadi wapigiwe simu na wapendwa wao.

Mtaalamu wa mawasiliano Amani Mosha amesema baada ya kumaliza chuo kikuu, aliingia kwenye mahusiano na mmoja ya watu aliomaliza nao, walidumu kwenye mahusiano  hayo kwa miezi sita na aliachwa na mpenzi wake siku ya wapendanao.

“Kuanzia asubuhi tulikua tunachati kwa simu, sasa nashangaa jioni mambo yakaenda mrama, nakuja kusoma meseji, naambaiwa I don’t care (sijali) na ndiyo maana sijafanya chochote katika siku ya wapendanao.

“Niliachwa usiku wa siku ya wapendanao huku najiona, sababu ni kuwa sijapeleka zawadi wala sijamtoa kwenda kula walau chakula cha usiku. Unavyoshangaa na mimi nilishangaa hivyo hivyo,” amesema Mosha ambaye bado nadharia ya Februari 14 haijamuingia akilini na katika tarehe hiyo, anakumbuka jinsi mahusiano yake yalivyoisha.


Soma zaidi:


Mapenzi huonyeshwa kila siku

Licha ya kuwa siku maalumu au waweza kusema mwezi mzima umetengwa kwa ajili ya kuonyesha mapenzi yako kwa uwapendao, kwa baadhi, siku ya wapendanao ni siku kama zilivyo siku zingine. 

“Ni kama kusema eti umpende mama yako siku ya mama duniani na kisha umkimbie mwaka mzima hadi siku kama hiyo mwakani. Siamini katika siku moja ya kuonyesha upendo,” amesema Kennedy William, mkazi wa Morogoro.

William amesema kama ni kwenda sehemu nzuri kula, inatakiwa kuwa jambo la kawaida vivyo hivyo kwa kupeana zawadi, kumwambia mtu unampenda.

Hata kwa Alma Miraji, siku ya Valentines sio lazima.

“Sio lazıma ufanye siku moja kwenye mwaka mzima ndiyo siku ya kuonyesha upendo kwa uwapendao. Unazo siku 365/366 za kuwaonyesha uwapendao kuwa unawapenda.

“Italeta maana sana ukiwaonyesha kıla siku badala ya kuchagua siku moja sababu unaowapenda wako wengi na utaigawaje hiyo siku?” amehoji Miraji ambaye licha ya kutokusherekea siku ya Valentine’s mahusiano yake “yanadunda”.

Wataalamu wa mahusiano wanena

Kwa upande wake Mtaalamu wa mawasiliano, Moses Samora amesema hadi kufikia siku inawekwa kwa ajili ya kuadhimisha upendo, basi siku hiyo ni muhimu.

Licha ya kuwa upendo unatakiwa kuonekana kila siku, lakini inapotokea watu walitenga siku kwa ajili ya kitu hicho ni muhimu watu kuona fursa katika kitu hicho na kukiweka katika mwanga.

“Kwangu mimi Valentine ni kama fursa ya kuwasha tena moto, kuchochea kuni ama kuongeza spidi katika kile kitu ambacho kinatakiwa kuwa kinaishi kila siku,” amesema Samora.

Unaweza pia kusikiliza hapa chini, maoni waliyotoa Watanzania walipofanya mahojiano na Nukta Habari.

Enable Notifications OK No thanks