Zawadi unazoweza kumpatia mtoto wako msimu wa sikukuu
- Ni pamoja na zawadi za kujifunzia na kuongeza maarifa.
- Zawadi zingine ni zile za kukuza kipaji cha mtoto wako.
- Mpatie mtoto wako safari ya ndoto zake.
Dar es Salaam. Imezoeleka kuwa ni nguo mpya na viatu lakini kwa mwaka huu, unaonaje ukifanya tofati kidogo?
Msimu wa sikukuu ni kati ya misimu nadra ambayo familia nzima inaweza kupata muda wa kukaa pamoja. Watoto hufunga shule na wazazi hupata likizo zao za mwezi Desemba.
Katika kipindi hiki, sikukuu mbalimbali ikiwemo sikukuu ya Uhuru wa Tanzania Bara, Krismas na mwaka mpya huwa sehemu ya siku za mapumziko kwa wafanyakazi na watoto.
Kwa mwaka 2021, chagua kumpatia mtoto wako zawadi itakayoacha alama. Picha| iStock.
Umepanga kumpa zawadi ipi mtoto wako? Hizi ni baadhi ya zawadi unazoweza kumpatia mtoto wako ili kumuongezea morali ya kusoma na hata kumjenga kiuchumi:
Simu janja, kompyuta ya kusomea
Kwa wazazi walio karibu na watoto wao, wanafahamu mambo ambayo simu zao zinapitia punde tu wanapofika nyumbani. Watoto hupenda kutazama katuni, kucheza michezo na kufanya mambo mbalimbali kwenye simu za wazazi au ndugu na jamaa waliopo nyumbani.
Katika msimu huu wa sikukuu, unaweza kuchagua kumnunulia mtoto wako tableti maalumu kwa ajili ya kujifunzia ikiwemo kuangalizia katuni na hata kucheza michezo.
Unaweza kuzipata kwa bei kuanzia Sh150,000 katika maduka mbalimbali na gharama zinazoendana na uwezo wa uhifadhi.
Pia unaweza kumnunulia kompyuta ya mezani walau aanze kuwa na uelewa wa matumizi ya teknolojia hiyo muhimu.
Katika maduka ya vifaa vya Tehama, unaweza kupata kompyuta nzuri ya mezani kwa gharama chini ya Sh1 milioni.
Safari ya ndoto zake
Watoto hujifunza mambo mengi shuleni. Nyimbo za mbuga za wanyama za Tanzania ambazo wengine huishia kuziona kwenye picha au kusoma majina yake kwenye vitabu.
Badala ya viwalo, mwaka huu unaweza kuchagua kumpeleka mtoto wako sehemu ambapo amekuwa akikusumbua mwaka mzima kutaka kwenda.ย
Wapo ambao kiu yao ni kwenda Kigamboni kuvuka bahari kwa pantoni na wengine shida yao ni kufika sehemu za chakula tu.
Unaweza kuweka bajeti yako na kumpeleka sehemu ambapo mtoto wako ataweka tiki kwenye orodha ya sehemu za ndoto zake.
Soma zaidi
- Nishati safi ya kupikia: Zawadi ya sikukuu kwa wazazi
- Zawadi zinazowafaa wanawake sikukuu ya wapendanao
- Maoni mchanganyiko zawadi ya maua kwa wapendanao Tanzania
Vifaa vya kukuza talanta yake
Baadhi ya wazazi huchukulia poa talanta za watoto wao. Huwaona watoto wao wakichora na kuona hilo ni jambo la kawaida na wala hawajishughulishi nalo.ย
Wengine huwaona watoto wao wakicheza mpira, wakiimba, wakibuni vitu lakini hawatilii mambo hayo maanani.
Badala ya kuwanyukisha pamba mpya mwisho wa mwaka huu, unaweza kuchagua kumnunulia mtoto wako vitu vya kukuza talanta yake kama gitaa kwa mwimbaji, mpira kwa mchezaji na rangi na karatasi kwa mchoraji.
Kukuza talanta ya mtoto wako angali mdogo humfanya awe bora kadri anavyozidi kuifanyia kazi.
Wadau wa malezi wanashauri usome tabia za mtoto wako na kuvifahamu vipaumbele vyake mapema. Hiyo itakusaidia kumchagulia zawadi ambayo ataitumia na siyo ile ataipokea na kuiweka ndani.
Latest