Wakulima wa mahindi walivyopoteza zaidi ya Sh30,000 kwa gunia Tanzania
- Bei ya zao hilo kwa mwaka mmoja unaoishia mwezi Januari imeshuka kwa zaidi ya Sh30,000
- BoT yasema hali hiyo inatokana na kuwepo kwa chakula kingi sokoni.
Dar es Salaam. Wakulima wa mahindi nchini Tanzania wamepoteza zaidi ya Sh30,000 kwa kila gunia la kilo 100 ndani ya mwaka mmoja uliopita, huku bei ya zao hilo la chakula ikishuka kidogo mfululizo kwa miezi miwili iliyopita.
Ripoti ya Mapitio ya Uchumi kwa mwezi Februari 2021 (Monthly Economic Review) iliyotolewa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa wastani wa bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la mahindi mwaka ulioishia Januari 2021 ilikuwa ShSh56,866 ikiwa imeshuka kutoka Sh92,795 iliyorekodiwa Januari 2020.
Bei hiyo ya Januari mwaka huu ipo chini kwa asilimia 38.7 ndani ya kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia mwezi Januari.
Hii ni sawa na kuwa wakulima wa mahindi wamepoteza Sh35,929 kwa kila gunia la kilo 100 mwezi Januari mwaka huu ikilinganishwa na walichouza Januari 2020.
Uchambuzi zaidi wa takwimu hizo za BoT unaonyesha kuwa bei ya zao hilo imeendelea kushuka kidogo ndani ya miezi ya miwili iliyopita kutoka Sh58,012 Novemba mwaka jana hadi Sh56,886 Januari mwaka huu kwa gunia la kilo 100.
Kushuka kwa bei hiyo ya mahindi kunawanufaisha zaidi wanunuzi hasa walaji kwa kuwa hawalazimiki kutoboa zaidi mifuko yao kupata chakula hicho muhimu na utengenezaji wa bidhaa viwandani.
Lakini wakulima ambao wamewekeza kulima zao hilo, kwao ni maumivu kwa sababu inawapunguzia faida ambayo wangepata endapo wangeuza kwa bei ya juu au sawa na ile waliouza Januari 2020.
Mahindi ni miongoni mwa mazao makuu ya chakula yanayojumuisha mchele, maharage, viazi mviringo, mahindi, mtama, uwele, ulezi na ngano ambayo hutumiwa zaidi na Watanzania.
Bei za mahindi ndani ya mwaka mmoja uliopita zimekuwa zikipanda na kushuka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko ya uzalishaji, hali ya hewa na gharama za usafirishaji.
Zinahusiana:
- Kigoma kinara usajili wa mashamba Tanzania bara
- Mnada wa Kahawa kuwanufaisha wakulima?
- Wakulima wanavyopigania bei nzuri ya mahindi Afrika Mashariki
Huenda bei ya mahindi ikaendelea kushuka miezi ijayo ikizingatiwa kuwa hivi karibuni Kenya ilipiga marufuku mahindi kutoka Tanzania na Uganda kuingia nchini humo kwa kile ilichodai kuwa yana sumu kuvu ambayo ina madhara kiafya jambo linaloweza kupunguza mahitaji sokoni.
Hata hivyo, baada ya mazungumza ya kidiplomasia, Kenya iliondoa marufuku hiyo huku ikiweka masharti mapya yanayosimamia ununuzi wa mahindi katika nchi hizo za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Miongoni mwa masharti hayo, Kenya inataka wadau wote wanaosafirisha mahindi nchini humo, kujiandikisha kwa Wizara ya Kilimo, na mzigo wa mahindi unaoingia nchini humo lazima uwe na cheti kinachoonyesha kuwa kiwango cha kemikali ya “aflatoxin” hakizidi kile kinachohitajika.
Pia wafanyabiashara wanahitajika kutoa taarifa kuhusu eneo yalipo maghala yanayohifadhi mahindi hayo.
Mbali na Kenya, Burundi nayo hivi karibuni iliweka zuio la kuingiza mahindi na unga jambo ambalo huenda likapunguza fursa kwa wakulima wa Tanzania kuuza katika nchi hiyo jirani.
Wizara ya biashara nchini Burundi ilipiga marufuku uagizaji wa mahindi na unga kutoka mataifa ya kigeni kwa muda wa miezi sita ijayo kuanzia Machi 8 mwaka 2021 kwa kile ilichodai siyo salama kwa afya za raia wake.
Hata hivyo, Taifa hilo la Afrika Mashariki halijaweza wazi nchi ambazo hazitaruhusiwa kuingia mahindi nchini humo, ikizingatiwa kuwa huagiza zaidi mahindi katika nchi za Zambia na Uganda.
Bei za mazao mengine ya chakula
Pia katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita unaoishia Januari 2021, bei za mazao yote ya chakula zilishuka isipokuwa viazi mviringo na uwele.
Bei ya jumla ya viazi mviringo hadi Januari 2021 ilikuwa Sh74,860 ikipanda kutoka Sh72,527 iliyorekodiwa Januari 2020.
Uwele ulipanda hadi Sh139,094 kutoka Sh127,849 iliyorekodiwa kipindi kama hicho mwaka jana.
“Bei za mazao ya chakula zilizochaguliwa ziliendelea kushuka mwezi Januari 2021 isipokua viazi mviringo na uwele ikilinganishwa na Januari 2020 kwa sababu ya kuwepo kwa chakula cha kutosha kwenye masoko,” inaeleza sehemu ya ripoti hiyo ambayo pia inapatikana katika tovuti ya BoT.