Kenyatta atoa wiki mbili mahindi yaliyokwama mpakani Tanzania kuachiliwa

May 5, 2021 10:50 am · Rodgers Raphael
Share
Tweet
Copy Link
  • Aagiza watendaji wa Serikali yake kuruhusu mahindi hayo yaingie nchini mwake.
  • Mahindi hayo yalizuiliwa kwa kile kinachodaiwa kuwa yana sumu kuvu.
  • Tanzania na Kenya zafungua ukurasa mpya.

Dar es Salaam. Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta ametoa wiki mbili kwa watendaji wa Serikali yake akiwemo Waziri wa Kilimo wa Kenya Peter Munya kumaliza mgogoro wa mahindi ya Tanzania yaliyokwama katika mpaka wa Namanga jijini Arusha. 

Rais Kenyatta ametoa agizo hilo leo Mei 5, 2021 wakati yeye na Rais Samia Suluhu Hassan walipohutubia kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya lililofanyika katika hoteli ya Serena jijini Nairobi. 

“Hiyo mahindi ambayo imelala hapo mpakani, Waziri mimi nakupatia wiki mbili yote iwe imefunguliwa na hiyo maneno iishe. Hakuna haja ya kuumiza watu yetu jamani,” amesema Rais Kenyatta.

Rais huyo ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) amesema Kenya na Tanzania ni nchi jirani zenye ushirikiano wa muda mrefu, hivyo  hakuna sababu ya kuwekeana vikwazo vinavyoumiza wananchi.

Agizo hilo huenda likawapa ahueni wafanyabiashara na wakulima ambao wana hifadhi kubwa ya mahindi ambayo yamekosa soko la ndani na nje ya nchi kutokana na kuwepo mavuno mengi.

Baadhi ya wafanyabiashara waliohudhuria kongamano la wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya. Picha| Ikulu Kenya.

Machi mwaka huu, mahindi ya Tanzania yalizuiliwa kuingia nchini Kenya kwa kilichodaiwa kuwa yana sumu kuvu ambayo ina madhara kiafya na hivyo kuwaacha wafanyabiashara wengi katika njia panda ya masoko.

Baada ya majadiliano na Tanzania, Kenya iliruhusu mahindi kuingia nchini mwake kwa masharti mapya ya wadau wote wanaosafirisha mahindi kujiandikisha kwa Wizara ya Kilimo.

Pia mzigo wa mahindi unaoingia nchini humo ilitakiwa uwe na cheti kinachoonyesha kuwa kiwango cha kemikali ya “aflatoxin” hakizidi kile kinachohitajika.

Sharti lingine lilikuwa ni wafanyabiashara wanahitajika kutoa taarifa kuhusu eneo yalipo maghala yanayohifadhi mahindi hayo.

Licha masharti hayo, bado biashara baina ya nchi hizo mbili haikukaa vyema na mahindi yaliendelea kuzuiliwa katika mpaka wa Namanga.


Soma zaidi:


“Mambo ya mawaziri kungoja hadi mkutano uitwe ,tunataka mawaziri mtoke ofisini, mtembeleane mtatue shida ambazo wafanyabiashara na wakulima wanazo. Mtu asione akipata ofisi hataki kuongea na mwenzake eti anangoja kuambiwa, kama wewe unangojea kuambiwa hustahili kuwa waziri,” amesema kenyatta mbele ya Rais Samia. 

Aidha, amewataka kurahisisha shughuli za usafiri katika mipaka ya Holili na Namanga ili kuongeza kasi ya biashara malori kutembea kwa haraka katika nchi hizo mbili. 

Rais Samia afungua ukurasa mpya

Akizungumza katika kongamano hilo, Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema wafanyabiashara wa Tanzania na Kenya waache kushindana na washirikiane ili kuhakikisha uchumi wa mataifa hayo mawili unaimarika. 

“Mna bahati kwamba nchi zetu mbili upande mmoja kuna uhuru wa kufanya biashara na upande mwingine kuna suluhu ya kuondoa vikwazo vya kuendesha biashara kwa hiyo sasa mshindwe ninyi.

Enable Notifications OK No thanks