Korongo wa Tanzania kupelekwa mbuga za wanyama Kenya
- Ni baada ya Kenya kuwa na uhitaji mkubwa wa ndege hao.
- Tanzania ina korongo 4,000.
- Watasaidia kuongeza idadi ya watalii nchini humo.
Mwanza. Kutokana na uhaba wa ndege aina ya korongo nchini Kenya, Rais wa Jwa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amempa Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta ndege hao 20 kwa ajili ya kuwekwa katika hifadhi za Taifa ili kuchochea shughuli za utalii nchini humo.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Kenya ina korongo 12 tu hivyo mtalii aliyetaka kuwaona kwa urahisi inalazimu kuja Tanzania ambako kuna jumla ya korongo 4,000.
Idadi ya korongo waliopo Tanzania ni mara 48,000 zaidi ya wale waliopo nchini Kenya.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza mara baada ya kufanya mazungumzo na mgeni wake Rais Kenyatta Ikulu jijini Dar es Salaam leo Desemba 10, 2021 amesema ndege hao watapelekwa Kenya mara tu baada ya taratibu za kimaandishi kukamilika .
“Hiyo ndiyo zawadi yetu ya Krismas kwenu naomba muipokee na taratibu zikikamilika zitafika huko huko kabla ya sikukuu ya Krismas,” amesema Samia.
Rais Samia amesema anaamini korongo hao watazaliana na kuongezeka kwa wingi kadiri siku zinavyoenda.
Aidha, Rais Samia pia ametumia fursa hiyo kumuomba Rais Kenyatta kumpatia majike mawili ya faru ili waolewe Tanzania.
Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema katika hifadhi za Taifa za Ngorongoro na Serengeti wana madume ya faru na hawana majike na anapenda wapate faru wa kike wenye rangi nyeusi waje waolewe Tanzania.
Hatua hiyo itasaidia kuinua sekta ya utalii katika nchi hizo mbili hasa unaohusu wanyamapori ambao ni adimu kupatikana.
Kwa upande wake Rais Kenyatta ameshukuru kwa zawadi aliyopatiwa kwa ajili ya wananchi wa Kenya na kwamba itasaidia katika suala la utalii.
Akijibu ombi la Rais Samia, Kenyatta amesema kuwa Kenya pia imekubali kutoa hao faru wawili wa kike na atapanga siku maalum ya kuwakabidhi.
“Kama Kenya tumekubali na tutahakikisha tunarudisha mkono kwa kuwapatia hao faru jike weusi ili waje waongeze idadi katika mbuga zetu na mapato pale watalii watakapokuwa wanakuja kutalii,” amesema Kenyatta.
Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akizungumza na mgeni wake Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya alipowasili Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Desemba 10, 2021. Rais Uhuru Kenyatta yupo nchini kwa Ziara ya Kiserikali ya siku moja. Picha| Ikulu.
Amesema amefurahi kusikia Rais Samia akipendekeza faru weusi kama rangi ya watu wa Afrika na wazungu wengi wanapenda rangi ya waafrika.
Amesema Kenya wapo tayari kusaidiana na Tanzania katika kulinda na kuenzi kile ambacho kiliachwa na mababu zao ili kiendelee kudumu na kuleta manufaa baina ya pande zote mbili.
Umeanaji zawadi za wanyama umekuwa utaratibu unaotekelezwa na nchi hizo mbili ili kudumisha uhusiano na ujirani mwema.
Aliyekuwa Rais wa Tanzania, Hayati John Magufuli Julai 6, 2019 alimzawadia Kenyatta ndege wanne aina ya tausi kama kumbukumbu ya uhusiano, urafiki na ujirani mwema kati ya nchi hizo mbili za Afrika Mashariki.
“Nimeguswa, sijawahi kugawa tausi kwenye nchi yoyote kwa sababu wana historia ya nchi yetu. Kwa heshima kubwa na mahusiano yaliyopo kati ya Tanzania na Kenya, nimekubali na hili nataka kulisema wazi.
“Najua watu wataandika lakini hili limenigusa kutoka moyoni, nitatoa tausi wanne watapelekwa Kenya kwa Kenyatta,” alisema Rais Magufuli na kuongeza kuwa baada ya miaka kadhaa ndege hao watazaliana na kurejeshwa tena Tanzania.
Mambo mtambuka
Katika mazungumzo ya marais hao wawili, wamekubaliana na kuondoa vikwazo vya biashara 46 kati ya 64, kuimarisha mipaka ya nchi hizo mbili,
“Tumekubaliana kushirikiana katika kupambana na UVIKO – 19, tumewaelekeza Mawaziri wa Afya waende wakashirikiane ili tulifanyie kazi suala hili kwa sababu sote ni wahanga,” amesema Rais Samia.
Pia wamekubaliana kushirikiana katika sekta ya utalii, ambapo mawaziri wa pande zote mbili watangumza “waone changamoto gani zipo na zipi ziondolewe ili nchi zote mbili tufaidike kuleta watalii wengi na kupata mapato mengi zaidi.”
Latest