Lissu awasili, mamia wajitokeza kumpokea Dar es Salaam

January 25, 2023 2:43 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link

John Heche na Peter Msigwa ni miongoni mwa viongozi wa Chadema waliompokea Tundu Lissu katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Januari 25, 2023. Lissu amerejea nchini baada ya kukaa ughaibuni kwa zaidi ya miaka miwili. Picha | Chadema. 


  • Kiongozi huyo, aliyegombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita amekaa ughaibuni kwa zaidi ya siku 806 tangu aondoke nchini Novemba 10, 2020.

Dar es Salaam. Mwanasiasa machachari  wa upinzani Tanzania, Tundu Lissu amerejea nchini baada ya kuwa uhamishoni kwa zaidi ya miaka miwili ikiwa ni wiki chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuondoa zuio la mikutano ya kisiasa.

Lissu ambaye ni Makamu mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), amewasili majira ya Saa 7:30 mchana katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akitokea Ubelgiji.

Kiongozi huyo anayefahamika kwa kukosoa vikali Serikali alipokelewa na umati mkubwa wa watu waliokuwa wakimsubiri nje ya uwanja huo. Wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamebeba mabango yenye ujumbe mbalimbali na bendera za chama hicho.

Mara tu baada ya kuwasili, Lissu aliingia kwenye gari kisha kukaa juu yake huku akipunga mkono uliokuwa umeshika bendera ya Chadema kwa wafuasi wake waliokuwa wamejipanga barabarani na kufuata magari yaliyokuwa yameenda kumpokea.

Miongoni mwa viongozi waliompokea Lissu ni Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na naibu wake Benson Kigaila. 

Kiongozi huyo, aliyegombea urais katika uchaguzi mkuu uliopita amekaa ughaibuni kwa zaidi ya siku 806 tangu aondoke nchini Novemba 10, 2020.

Lissu anatarajia kuhutubia katika mkutano wa hadhara utakaofanya viwanja vya Mwembe Yanga jijini Dar es Salaam. 

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe (kushoto) akisalimiana na Makamu Mwenyekiti (Bara), Tundu Lissu katika uwanja wa Bulyaga, Temeke ambapo ulifanyika mkutano wa hadhara. Hii ni baada ya mapokezi ya Lissu katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Nyerere (JNIA). Picha | Chadema.

Baada ya kuwasili katika viwanja vya Bulyaga, Lissu aliwasalimia umati wa watu waliofika na kusalimiana na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe kabla ya kupewa nafasi ya kuhutubia wanachama waliohudhuria mkutano huo.

Lissu katika hotuba yake amesema aliishi nje ya nchi kwa kulazimishwa kwa sababu uliogopa kudhuriwa baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.

“Hii miaka takriban mitano au takriban sita haijawa miaka rahisi hata kidogo, kwangu binafsi, kwa familia yangu, ndugu zangu, kwa chama changu na kwa nchi yangu. 

“Kwa sababu ni miaka mitano ya kulazimishwa kwa kuondoka nyumbani kwako na nyumbani kwenu kwa sababu usipokimbia kuna watu wametumwa wakuue. Niseme nafurahi sana kurudi nyumbani kwangu na kurudi nyumbani kwetu,” amesema Lissu huku akishangiliwa na umati wa watu waliokuwepo uwanjani hapo.

Kiongozi huyo wa juu wa Chadema katika hotuba yake amesema kuna haja ya kushughuligikia suala la mfumo wa kisiasa nchini kwa sababu umekuwa ukichangia ugumu wa maisha wanaoupata wananchi ikiwemo kupanda kwa bei za vyakula na utitiri wa kodi zinazowaumiza. 

Amesema suluhu yake ni Tanzania kuwa Katiba Mpya itakayokidhi matarajio ya Watanzania na ambayo itawadhibiti viongozi katika shughuli zao ili watimize wajibu wa kuwatumikia wananchi na kuendeleza rasilimali za nchi.

“Tatizo la maisha magumu ni tatizo la kisiasa na tatizo la kikatiba, kama mmechoka tutafute suluhu ya kisiasa ambayo ni Katiba Mpya,” amesema Lissu.

Baada ya kumaliza hotuba yake, Mwenyekiti Mbowe alisimama na kutoa hutuba fupi huku akisisitiza kuendelea kusimama na wananchi na kuwataka wanachama wa Chadema kuendeleza ajenda ya Katiba Mpya mpaka ipatikane.

Mbowe alitumia fursa hiyo kuahirisha mkutano huo huku Lissu akikabidhiwa zawadi ya mbuzi kama ishara ya kumkaribisha nyumbani.

Follow Us on TikTok

FOLLOW NOW

Subscribe to Our YouTube Channel

SUBSCRIBE NOW