Kwanini wanawake wa kiislamu huchora piko, hina wakati wa sikukuu za Eid?
- Kuchora hina ni ishara ya usafi, furaha, urembo katika matukio maalum kama sikukuu za Eid pamoja na harusi.
Arusha. Katika kusherehekea sikukuu za Kiislamu ikiwemo Eid al-Fitr na Eid al-Adha, ni kawaida kwa wanawake wa dini hiyo kujipamba kwa mavazi, michoro na vito vya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na bangili, hereni na mikufu.
Mbali na mavazi mapya na aina nyingine za urembo, wanawake wa Kiislamu hujichora piko ama hina ikiwa ni sehemu ya kuboresha muonekano wao katika kusherehekea sikukuu hizo za kidini.
Hina ni rangi ya asili inayotokana na aina fulani ya majani ya mimea maalum inayotumika kupaka au kuchora ngozi katika mitindo mbalimbali katika mwili wa mwanamke.
Miongoni mwa sehemu hizo ni viganjani, sehemu za juu za mikono, miguuni na pembeni ya unyayo na sehemu nyingine za mwili, huku wengine wakiongeza nakshi kwa kuichanganya na piko ili kuchora maua yenye muonekano mbalimbali ikiwa ni namna ya kunogesha zaidi sikukuu.
Miongo kadhaa iliyopita, hina ya majani na ya kupika ndio iliyokuwa ikitumika zaidi, ingawa kwa sasa watu wengi pia hutumia hina za kisasa maarufu kama ‘red henna’.
Hata hivyo, hina pamoja na piko hazipakwi katika sikukuu pekee bali hupakwa kwa utaratibu maalum na katika sherehe mbalimbali ikiwemo harusi, hakika na nyinginezo kwa mujibu wa sheria za dini ya kiislamu.
“Kupaka hina, rangi ya midomo na aina nyingine za urembo ni miongoni mwa mambo ambayo Mtume Muhammad (S.A.W) aliyakataza, wanaoruhusiwa ni wanawake walioolewa pekee…
…Anayepaswa kuona hizo hina na aina nyingine za urembo katika matukio hayo muhimu ni mume wake tu ila mwanamke akitoka nje ni sharti ajistiri zile sehemu za mikono na miguu zisionekane,” amesema Ostadh Hafidh Ngoisa kutoka Arusha.
Pamoja na miongozo hiyo ya dini, bado mamia ya wanawake wa Kiislamu wanapaka hina au piko katika siku au matukio maalum kutokana na sababu zifuatazo:

Kuchora hina humuongezea mwanamke kujiamini na furaha katika kusheherekea matukio ya muhimu ikiwemo sikukuu za Eid.Picha|Flickr.
Ishara ya usafi, urembo
Katika uislamu, usafi na unadhifu ni msingi muhimu wa maisha ya kila siku. Hili linaungwa mkono na mafundisho ya Quran na hadithi, ambapo waumini wanahimizwa kuwa wasafi kimwili na kiroho huku wanawake wakisisitizwa kujipamba kwa ajili ya waume zao.
Kwa mfano, katika Quran (Surah Al-A’raf 7:31) Waumini wanahimizwa kuvaa vizuri katika kila ibada “Enyi wanadamu! Chukueni mapambo yenu (kwa kuvaa nguo zenu safi) huku mkiswali…”
Aya hii mara nyingi hutafsiriwa kama wito wa kujipamba kwa staha na uzuri hasa katika nyakati za ibada na sikukuu kama Eid. Hivyo basi, kupaka hina wakati wa Eid si suala la urembo pekee, bali ni mwendelezo wa mafundisho ya dini yanayohimiza usafi.
Ni sunna kwa mujibu wa taratibu za kidini
Matumizi ya hina au piko kwa wanawake katika uislamu mara nyingi huchukuliwa kama sunna (jambo ambalo ukilifanya unapata malipo mema na ukiliacha haupati dhambi) kwa mujibu wa mafundisho ya dini, hasa kupitia hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W).
Wanazuoni wengi wa Kiislamu wanaeleza kuwa kupaka hina ni sehemu ya kujipamba kwa wanawake kwa njia inayokubalika, na ni katika mambo yaliyokuwa yakifanywa na wanawake katika zama za Mtume.

Hina huweza pia kupakwa katika nywele ili kuzipa rangii na mwonekano wa kuvutia.Picha|Sakamia cleaners.
Kwa mujibu wa vitabu vya hadith kama Sunan Abu Dawud na Sunan an-Nasa’i, kuna simulizi zinazoonesha kuwa Mtume alihimiza wanawake kutumia hina mikononi ili kujitofautisha na wanaume, suala ambalo wanazuoni wa kiislamu hulitafsiri kama ishara ya kuruhusiwa kwa urembo huo.
Kudumisha umoja na mshikamano katika jamii
Utamaduni wa kupaka hina huchangia kudumisha umoja na mshikamano katika jamii. Katika baadhi ya maeneo, wanawake hukutana kwa pamoja kupakana hina, wakishirikiana maandalizi ya sikukuu na kuimarisha uhusiano wao wa kijamii.
Wengine huutumia ujuzi huo wa kupaka hina kujiingizia kipato suala ambalo linachangia katika kukuza uchumi wa wanawake hao.
Latest