Fahamu aina za mitandio na matumizi yake

February 25, 2025 1:49 pm · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Miongoni mwa mitandio hiyo ni ushungi na nikabu inayopendelew akuvaliwa zaidi na wanawake.
  • Hutumika kama sehemu ya mavazi ya heshima na uaminifu kwa imani ya Kiislamu.

Dar es Salaam. Mtandio ni vazi maarufu linalovaliwa na watu wa rika na tamaduni mbalimbali duniani kwa madhumuni tofauti, ikiwa ni pamoja na urembo, heshima, na hata kujikinga na hali ya hewa.

Kwa mujibu wa Kamusi Kuu ya Kiswahili toleo la tatu, mtandio ni kitambaa kinachovaliwa na wanawake kichwani au mabegani.

Licha ya vazi hilo kutumiwa kwa muda mrefu, ni watu wachache wanaofahamu maana ya kila rangi, aina na jinsi zinavyotumiwa kuendana na mazingira au mahali mtumiaji alipo.

Ikiwa hufahamu aina za mitandio, makala hii ni kwa ajili yako ambapo tutaangazia aina hizo ili usipitwe na mitindo ya vazi hilo lililojizolea umaarufu hususani kwa watu wa dini ya kiislamu.

Hijabu 

Hijabu ni kitambaa kinachovaliwa na wanawake wa Kiislamu kwa ajili ya kufunika kichwa hadi sehemu fulani ya mikono huku nyingine zikifika hadi viganjani.

 Hutumika kama sehemu ya mavazi ya heshima na uaminifu kwa imani ya Kiislamu ikihusishwa sana na dhana ya staha, ambapo wanawake huvaa ili kujisitiri na kufuata mafundisho ya dini yao.

Mbali na umuhimu wake wa kidini, hijabu pia imekuwa sehemu ya mtindo wa mavazi kwa wanawake wengi kote ulimwenguni ikinakshiwa kwa  mitindo, maumbo na rangi mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya mtumiaji. 

Katika nchi nyingi za Kiarabu na Kiislamu, hijabu inavaliwa kwa mtindo wa kitaaluma na hata wa kisasa, huku wabunifu wa mitindo wakizidi kuitengeneza kwa muundo wa kuvutia tofauti na zamani.

Nikabu 

Nikabu ni aina ya mtandio unaovaliwa kufunika uso mzima, huku macho pekee yakiachwa wazi. Hutumiwa mara nyingi na wanawake wa kiislamu wanaotaka kujistiri zaidi kwa mujibu wa imani zao. 

Katika baadhi ya nchi za kiarabu kama Saudi Arabia, nikabu ni sehemu ya mavazi rasmi kwa wanawake, hasa wale wanaofuata maadili na maelekezo  ya Kiislamu yanayomtaka kujihifadhi.

Licha ya kuwa sehemu ya mavazi ya kidini, nikabu pia hutumika kwa madhumuni ya faragha na usiri. Wanawake wanaovaa nikabu hujihisi salama na huru kutokana na mtazamo wa watu wengine.

Hata hivyo, katika baadhi ya mataifa, vazi hili limekuwa mada ya mjadala ikihusishwa na vitendo vya kihalifu, huku baadhi ya nchi zikipiga marufuku uvaaji wake katika maeneo ya umma.

Kama ilivyo katika aina nyingine ya mavazi, nikabu pia hutengenezwa kwa rangi na nakshi mbalimbali ili kuvutia wavaaji.Picha|Local Denmark

Ushungi 

Ushungi ni kitambaa maalumu kinachomwezesha mwanamke kufunika kichwa chake kikamilifu. Hutumiwa kwa sababu za kidini, kitamaduni, au hata kama mapambo katika baadhi ya jamii.

Ushungi umeenea sana katika nchi za Afrika Mashariki, hususan Tanzania, Kenya na Uganda, ambapo huvaliwa na wanawake wa dini na tamaduni mbalimbali.

Vazi hilo linaweza kuwa la rangi tofauti na hufungwa kwa mitindo mbalimbali kulingana na matakwa ya mvaaji.

 Katika baadhi ya jamii, ushungi unahusishwa na heshima na ustaarabu wa mwanamke huku wengine wakiutumia kama fasheni au kufunika kichwa ikiwa nywele au mtindo wa kusuka umeanza kufumuka.

Ukaya

Ukaya ni kitambaa chepesi kinachovaliwa kwa ajili ya kuziba kichwa na uso ambacho mara nyingi hutumiwa na wanawake kama sehemu ya mavazi ya kila siku au katika mazingira rasmi kulingana na tamaduni zao.

Kitambaa hiki ni chepesi na mara nyingi hutengenezwa kwa hariri au pamba laini, hivyo kufanya iwe rahisi kuvaliwa kwa muda mrefu bila kusababisha usumbufu.

Katika jamii mbalimbali, ukaya unavaliwa kwa mtindo wa kupendezesha mavazi, huku wanawake wakichagua rangi zinazolingana na nguo zao. 

Ukaya pia hutumika kama njia ya kujikinga na vumbi au jua kali, hasa katika maeneo ya joto kali.

Barakoa 

Barakoa ni kitambaa kinachovaliwa kuanzia kwenye paji la uso hadi kufunika mdomo.Mara nyingi, hutumiwa na wanawake waliovaa buibui, hasa katika maeneo yenye jamii zinazofuata mavazi ya Kiislamu. 

Barakoa ina umuhimu mkubwa katika jamii, kwani husaidia wanawake kujikinga na vumbi, jua, au hata baridi kali.

Zaidi ya hayo, barakoa hutumika kwa madhumuni ya faragha na usalama, katika baadhi ya jamii, huvaliwa na wanawake wa hadhi ya juu ili kujilinda dhidi ya macho ya watu wasiowajua.

Pia, barakoa imetumika katika historia kama sehemu ya mavazi ya kifalme au ya kiutawala katika baadhi ya tamaduni za Kiarabu.

Hata hivyo, vazi hili halivaliwi tu na wanawake lakini pia hutumiwa na jinsia zote hasa pale linapokuja swala la kutunza afya na kujikinga kwa vumbi na wadudu wanao sambaa kwa njia ya hewa. 

Aina hi ya mtandio husaidia wanawake wanaopenda kujistiri au wenye aibu kujifunika nyuso zao wakati wakizungumza na watu wa jinsi nyingine au waliowazidi umri.Picha|Modernalisa.

Dusumali 

Dusumali ni kitambaa chenye rangi mbalimbali kinachovaliwa kichwani na wanawake kwa madhumuni ya urembo au kitamaduni. 

Dusumali hupendwa sana maeneo ya Pwani kama Zanzibar, Lamu, na Mombasa, ambako wanawake wanathamini mitindo yenye rangi zinazong’aa na za kuvutia.

Mbali na kutumika kama urembo, dusumali pia hutumika katika hafla maalum kama harusi, sherehe za jadi, na matukio ya kifamilia. 

Wanawake huvaa mitandio hii kwa namna ya kupendezesha mavazi yao, huku wakitengeneza mtindo wa kipekee unaoendana na vazi wanalovaa.

Kilemba 

Kilemba ni kitambaa cha rangi yoyote kinachofungwa kichwani kwa mtindo maalum.

 Kinavaliwa na watu wa jinsia zote kwa madhumuni ya kitamaduni, kidini, au hata kama sehemu ya mtindo wa mavazi. 

Kilemba kina historia ndefu katika jamii nyingi za Kiafrika, Kiasia, na hata Kiarabu, ambapo hutumika kama ishara ya hadhi au heshima katika jamii.

Katika baadhi ya tamaduni za kiafrika, wanaume huvaa vilemba ili kuashiria uongozi au hadhi fulani.

Pia, katika nchi kama India, vilemba huvaliwa na wanaume katika harusi na sherehe nyingine za kifamilia kama alama ya heshima na hadhi.

Kila aina ya mtandio ina historia na matumizi yake maalum, yanayoifanya kuwa sehemu muhimu ya maisha ya watu wengi duniani.

Enable Notifications OK No thanks